Header Ads

BIOTEKNOLOJIA NA UMWAGILIAJI KUPAISHA KILIMO TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakivuta pazia kuashiria uzinduzi wa Maabara ya Rufaa ya Taifa ya Kilimo Agosti 8, 2025 iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.

 ...........................

Na Dotto Mwaibale 

Katika historia ya maendeleo ya kilimo nchini Tanzania, Agosti 8, 2025 itaendelea kukumbukwa kama siku ya uthibitisho wa dhamira ya kweli ya Serikali ya Mapinduzi ya Kisekta.

 Ni siku ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisimama mbele ya wakulima, watafiti, wanasayansi na wadau wa kilimo katika viwanja vya Nane Nane Nzuguni, Dodoma na kutoa kauli ya matumaini.

Alitangaza mustakabali mpya wa kilimo cha umwagiliaji kama mustakabali unaojengwa juu ya sayansi, teknolojia na bioteknolojia ya kilimo ili kulinda uhakika wa chakula na kuongeza thamani ya mazao.

Rais Samia alisema kwa msisitizo: “Natamani kuona Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikiendelea kufanya kazi, kuchochea uzalishaji, na kuhakikisha huduma hizi zinamfikia mkulima wa kila ngazi — mdogo, wa kati, na mkubwa.”

Kauli hii haikuwa tu mwito wa kisera, bali ni tangazo la mapinduzi ya uzalishaji wa chakula, yanayounganisha teknolojia ya umwagiliaji na bioteknolojia ya kisasa katika kuzalisha mbegu bora, kustahimili mabadiliko ya tabianchi, na kuleta tija.

Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya umwagiliaji ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025 pekee, zaidi ya hekta 700,000 zimewekewa miundombinu ya umwagiliaji na kuanza kutumika.

Hatua hizi ni pamoja na ujenzi wa skimu mpya 63 na ukarabati wa skimu 48, ujenzi wa mabwawa 114 na miundombinu katika mabonde 22 ya kimkakati, sambamba na uanzishaji wa mashamba makubwa ya pamoja sita.

Aidha, imefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi 527 ambayo inaendelea mpaka sasa.

Na baada ya miradi hiyo kukamilika, eneo la umwagiliaji litaongezeka kutoka hekta 727,000 za sasa hadi hekta 1.2 milioni.

Kwa muktadha huo, hiyo ni hatua ambayo si tu inapunguza utegemezi wa mvua, bali pia inaleta fursa ya kupanua matumizi ya mbegu bora za kibioteknolojia zinazohitaji usimamizi sahihi wa maji ili kutoa mavuno ya juu.

Maonesho ya Nane Nane mwaka huu yalionesha sura mpya ya Tanzania katika teknolojia ya kilimo.

Kuanzia mifereji ya kisasa, mifumo ya kunyunyizia maji (sprinklers), umwagiliaji wa matone (drip irrigation), hadi mitambo mikubwa ya centre pivot — yote yalitoa taswira ya taifa linalokimbizana na wakati.

Lakini kilichobeba uzito zaidi ni ujumuishaji wa teknolojia hizi na bioteknolojia.Matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame, mbegu zinazokua kwa muda mfupi, na mazao yanayoboreshwa kimaumbile ili kuongeza virutubisho.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alibainisha kuwa mashamba ya mbegu ya serikali yenye zaidi ya hekta 13,000 tayari yanatumia mifumo ya umwagiliaji pamoja na mbegu za kisasa zinazozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Benedict Kahemele wa Ilula mkoani Iringa ni mfano wa mabadiliko haya. alianza kulima nyanya na mahindi kwa mvua, alikumbwa na hasara mara kwa mara. Lakini tangu aanze kutumia skimu ya umwagiliaji na mbegu bora kutoka TARI na matumizi ya teknolojia za bioteknolojia, hali imebadilika.

“Sasa nalima misimu yote bila hofu ya ukame, nyanya zangu zinavumilia magonjwa, na kipato changu kimenipatia nyumba yangu na wapangaji wangu,” anasema Kahemele huku akionesha kufurahia kilimo.

Hadithi yake ni kielelezo cha jinsi sayansi na bioteknolojia zinavyobadilisha maisha ya kila siku ya Watanzania kupitia kilimo chenye tija.

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, chini ya uongozi wa Raymond Mndolwa, imekuwa kiungo cha kufanikisha mabadiliko haya.

Kupitia ufadhili wa serikali, tume imenunua pampu 2,000, mitambo ya kuchimba visima, na vifaa vya kusambazwa nchi nzima.

Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeongeza mtaji wake kutoka shilingi bilioni 60 hadi bilioni 442, na kutoa mikopo ya pembejeo, ikiwemo zile za bioteknolojia kama mbegu bora na viuatilifu salama kwa mazingira.

Katika kilele cha hafla hiyo, Rais Samia alizindua Maabara ya Rufaa ya Taifa ya Kilimo jijini Dodoma. Maabara hii, chini ya TARI, ni injini ya mapinduzi ya 'agricultural biotechnology' nchini kwa utambuzi wa magonjwa ya mimea na visumbufu.

Pia kazi nyingine ya maabara hiyo ni mahsusi kwa uchunguzi wa afya ya udongo, ubora wa mbegu, utafiti wa viini lishe ili kuboresha thamani ya mazao na udhibiti wa sumukuvu (aflatoxin).

Kwa maabara hiyo, sera na maamuzi ya kilimo yatajengwa juu ya ushahidi wa kisayansi.

Hii inamaanisha Tanzania sasa inaweza kuzalisha mbegu zilizoboreshwa kitaalamu (improved seeds), kustahimili ukame, magonjwa na hata kuongeza mazao yenye lishe bora kwa afya ya jamii.

Ongezeko la eneo la umwagiliaji na uwekezaji katika bioteknolojia linaashiria:

Kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao kwa zaidi ya asilimia 50 katika miradi ya umwagiliaji.

Ajira mpya zaidi ya laki mbili vijijini kupitia kilimo na mnyororo wa thamani.

Mapato ya wakulima kuongezeka maradufu kutokana na mbegu bora na mavuno thabiti.

Hii siyo tu takwimu, bali ni uhakika wa heshima, kipato, na maisha bora kwa jamii ya wakulima vijijini.

Kwa hatua hizi, Tanzania sasa inajipanga sambamba na mataifa yanayotumia bioteknolojia ya kilimo kama India, Brazil na Afrika Kusini.

Uwekezaji wa umwagiliaji unaounganishwa na mbegu bora za kisayansi unaipa Tanzania nafasi ya kuwa ghala la chakula la Afrika Mashariki na mshindani katika soko la kimataifa.

Rais Samia amesisitiza kuwa ifikapo mwaka 2030, sekta ya kilimo lazima iwe imara, shindani, na yenye kipato cha uhakika.

Pia alisisitiza Dira ya Taifa 2025-2050 pia imezingatia kwa uzito masuala haya ikiwemo uzalishaji wa chakula wa kutosheleza taifa na ziada ya kuuza nje.

Pia mauzo ya mazao yenye thamani kubwa na bora kiafya (biofortified crops),

ajira endelevu kwa vijana na wanawake vijijini na uchumi wa kilimo unaotegemea sayansi na ubunifu.

Mapinduzi haya si jukumu la serikali pekee. Ni mwaliko kwa kila mdau — kutoka mtafiti wa maabara, mzalishaji wa mbegu, mhandisi wa umwagiliaji, taasisi za fedha, hadi mlaji wa mwisho.

Kama alivyoeleza Rais Samia: “Mnyororo wote wa kilimo lazima ukae vizuri.” Ni wakati wa kuhakikisha kila kiungo kinang’aa — kwa msaada wa umwagiliaji wa kisasa na bioteknolojia ya kilimo — ili Tanzania ifikie uhuru wa chakula na ustawi wa Taifa zima.

Na katika kufanikisha hilo, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ni ya msingi kwa mtazamo wa kisera na kiutekelezaji, ndio kiungo kikuu cha kuratibu tafiti zote za bioteknolojia ya kilimo nchini.

 Pia COSTECH ni injini ya kisayansi nyuma ya maono ya Rais Samia kuhusu kilimo cha kisasa – ikihakikisha kuwa uwekezaji wa umwagiliaji, mbegu bora na utafiti wa kisayansi vinaunganishwa katika mnyororo wa thamani wa kilimo Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Maabara ya Rufaa ya Taifa ya Kilimo Agosti 8, 2025 iliyopo Mtumba Jijini Dodoma.

Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wakifurahia moja ya kazi za usindikaji zinazofanywa na taasisi hiyo kwa kunyanyua chupa yenye mvinyo uliotengenezwa kwa 'Bibo la Korosho' , kwenye maonesho ya nanenane kitaifa mwaka 2020 yaliyofanyika eneo la Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Muonekano wa Jengo la Makao Makuu ya  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo  ndio kiungo kikuu cha kuratibu tafiti zote za bioteknolojia ya kilimo nchini. 

No comments

Powered by Blogger.