TAASISI 16 ZA KILIMO HAI IKOLOJIA KUSHIRIKI MAONESHO YA NANENANE JIJINI DODOMA
Na Mwandishi Wetu
WADAU wa kilimo ikolojia hai kutoka taasisi 16 nchini wanatarajia kushiriki
katika maonesho ya kitaifa ya nanenane 2024 ambayo yaanza Agosti 1 hadi 8,
mwaka huu mkoani Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Kikosi Kazi cha Mbegu Asili nchini, Abdallah
Mkindi wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam.
Mkindi amesema wanashiriki maonesho ya mwaka huu, ikiwa ni utekelezaji wa
mkakati wa kilimo hai ambao umezinduliwa hivi karibuni na serikali.
Ametaja taaasisi za kilimo ikolojia hai ambazo zinashiriki nanenane 2024,
ni Mtandao Baionuai Tanzania (TABIO), Taasisi ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM),
Biovision Africa Trust (BVAT), SwissAid Tanzania, Floresta, na Shirikisho la
Vyama vya Wakulima Wadogo Tanzania (SHIWAKUTA).
Nyingine ni Agroecology Hub-SUA, Kijani Hai, IDP, We Effect, VI
Agroforestry, Farm Radio International, Taasisi ya Kilimo Endelevu Tanzania
(SAT), Safari Organic Co Ltd na MC Donald Organic Products.
“Mwaka huu tumeandaa mabanda yasiyopungua sita ambayo yataonesha teknolojia
na bidhaa mbalimbali, mbegu za asili, pembejeo za kilimo kama mbolea na dawa za
kuuwa wadudu wasumbufu,” amesema Mkindi.
Mratibu huyo amesema wao kama wadau wakuja pamoja kuhakikisha mkakati huo
unafanikiwa na kuleta mabadiliko kwenye sekta ya kilimo hasa kilimo ikolojia
hai.
Mkindi ambaye pia ni Mratibu wa TABIO, amesema katika maonesho hayo
watakuwa na wakulima zaidi ya 20 ambao wanazalisha mazao mbalimbali kama
mahindi, maharage, mpunga, viazi na mengine kwa njia ya asili.
Amesema pia kupitia maonesho hayo watakuwa na kauli mbiu ya mbegu ni uhai
hali ambayo itasaidia watunga sera na wananchi kutambua faida ya mbegu za asili
kwa watumiaji na nchi.
Mratibu huyo amesema katika kuhakikisha dhana ya mbegu ni uhai inafikia
jamii kubwa wameandaa mabango na midahalo kwa wadau wa sekta ya kilimo hasa
kilimo ikolojia.
“Hizi siku nane za maonesho ya nanenane tumejipanga kutoa elimu kwa
wananchi, kuhusu faida za kutumia vyakula ambavyo vimetokana na mbegu asili,
lakini pia tutaonesha bidhaa zote ambazo zina faida katika kilimo,” amesema.
Mkindi amesema faida ya mbegu asili ni urithi wetu, zina virutubisho,
wakulima wanazimiliki, zinatunza na kulinda baionuai, zina ustahimilivu na
mabadiliko ya tabianchi na mazingira kwa ujumla.
Mratibu huyo amesisitiza kuwa iwapo wakulima watajikita katika kilimo
ikolojia hai watahakikishia jamii usalama wa chakula na afya kwa watumiaji.



No comments