WMA YAELEZA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA YA KILIMO

...................................
Veronica Simba na Paulus Oluochi – WMA
KAIMU Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo Tanzania
(WMA), Albogast Kajungu, amesema WMA ina mchango mkubwa katika sekta ya kilimo
hususani katika mazao ya kimkakati ambayo ni korosho, ufuta, kahawa, tumbaku na
pamba.
Amebainisha hayo Agosti 3, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari
katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo maarufu kama NaneNane yanayoendelea katika
viwanja vya Nzunguni jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa kazi kubwa ya Wakala wa Vipimo katika sekta hiyo ndogo ya
mazao ya kimkakati ni kuhakikisha Mizani zinazotumika katika ununuzi wa mazao
hayo zinahakikiwa ili kujiridhisha kuwa ziko sahihi.
“Lengo ni kuhakikisha kwamba mkulima anapouza mazao yake anapata thamani ya
pesa sawasawa na mazao aliyouza,” amefafanua Kajungu.
Akieleza zaidi, Mkurugenzi huyo wa Huduma za Ufundi amesema zoezi la
kuhakiki Mizani hufanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza huhusisha
uhakiki wa mizani kabla ya msimu wa kila zao kuanza ilhali awamu ya pili
huhusisha ukaguzi wa kushtukiza wakati wa msimu kwa kila zao ili kujiridhisha
kama vipimo vilivyohakikiwa awali vinatumika kwa usahihi.
“Kwahivyo kabla ya msimu tunapita kuhakiki mizani zote zinazotumika
kununulia mazao na wakati wa msimu tunapita kujiridhisha kama zinatumika kwa
usahihi.”
Aidha, Kajungu ameeleza kuwa, mbali na zoezi la ukaguzi, Wakala wa Vipimo
pia hutoa elimu kwa wakulima na wananchi kwa ujumla ili wafahamu sifa za mizani
ya kununulia mazao iliyohakikiwa.
Ametaja mojawapo ya sifa za mizani iliyohakikiwa kuwa ni uwepo wa stika ya
Wakala wa Vipimo inayoonesha tarehe ambayo mizani husika ilihakikiwa pamoja na
tarehe ya mwisho ambayo stika hiyo itakuwa imekoma matumizi yake.
“Kwahiyo mwananchi akiiona ile stika inampa uhakika kuwa mizani hiyo
imehakikiwa na Wakala wa Vipimo,” amesisitiza Kajungu.
Vilevile, akizungumzia kuhusu ufungashaji wa mazao ya shamba, ameeleza kuwa
kwa mujibu wa sheria, kufungasha mazao ya shamba kwa uzito unaozidi kilo 100
unatafsiriwa kama lumbesa ambayo ni kosa kisheria.
Amesema, kumekuwa na mkanganyiko wa tafsiri ya neno lumbesa ambapo baadhi
huitafsiri kama kufungasha mazao ya shamba kwa kuongeza kishungi, ambapo
tafsiri hiyo siyo sahihi.
Kajungu ametoa wito kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kufahamu kwamba
mazao yote ya shamba ni lazima yafungashwe kwa uzito unaokubalika kisheria
ambao ni kilo 100.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya vipimo, Kajungu
amesisitiza umuhimu wa kuwepo vituo vya kununulia mazao ambavyo ni rahisi
kuweka mizani iliyohakikiwa na WMA ili itumike kwa wakulima kuhakiki mazao yao
na kujiridhisha kwamba yamefungashwa katika uzito wa kilo 100 bila kuzidi ili
kupata faida stahiki kwa pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi.
Wataalamu wa Wakala wa Vipimo wanashiriki katika Maonesho ya NaneNane
kitaifa jijini Dodoma na kikanda katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la
kutoa elimu kwa wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) Albogast
Kajungu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Wakala hiyo,
wanaoshiriki katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima NaneNane (2024)
yanayoendelea jijini Dodoma.WMA inatoa elimu kwa wadau wa kilimo na wananchi
kwa ujumla kuhusu matumizi ya vipimo sahihi.
Afisa Vipimo Mwandamizi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA) akitoa elimu kuhusu
umuhimu wa kuhakiki dira za maji katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane
(2024) yanayoendelea jijini Dodoma.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Wakala wa Vipimo (WMA), Veronica Simba
akitoa elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi katika Maonesho ya Kitaifa ya
Kilimo NaneNane (2024) yanaoendelea jijini Dodoma.Afisa Vipimo Mwandamizi kutoka Wakala wa Vipimo (WMA), Said Ibrahim akitoa elimu kuhusu
umuhimu wa kuhakiki dira za maji katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane
(2024) yanayoendelea jijini Dodoma.

No comments