BASHE AWATAKA WAKULIMA NA WAFUGAJI KUISHI KWA AMANI
NIRC Songea.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewaasa wafugaji wa jamii ya Wasukuma
wanaoishi katika kata ya Ndalila Wilayani Songea, kuhakikisha kuwa wanaishi kwa
amani na wakulima wa jamii zingine wilayani humo.
Bashe amesema hayo akiwa katika kata ya Njalila Wilayani Songea wakati wa mwendelezo wa ziara
yake kukagua miradi ya kilimo katika
mikoa mbalimbali nchini ambapo amezungumza na wananchi kuhusu kero zao na
mipango ya serikali katika kutatua kero hizo. Alielekeza viongozi wa taasisi za
serikali kuchukua hatua na kufanya usanifu wa barabara na bwawa kwa ajili ya
kumwagilia hekari 6000, pamoja na kujenga zahanati na kituo cha afya.
“Mkurugenzi wa Umwagiliaji na
mhandisi wa Umwagiliaji mkoa pia yupo hapa, Kwa mwaka huu tutaanza na usanifu
ambapo wataalamu watakuja kwa ajili ya kujua gharama, na masuala mengine muhimu
kabla ya Kuanza utekelezaji”, alisema Bashe.
Mhe.Bashe ameelekeza viongozi mbalimbali wa taasisi za serikali
zinazohusika na kero zilizo ibuliwa na wananchi hao kuchukua hatua.
”Serikali ifanye usanifu wa bara bara kwa ushirikiano wa TARURA na Tume ya
Taifa ya Umwagiliaji tutaanza usanifu kujua gharama, za bwawa, barabara na
ujenzi wa miundombinu ya shamba”, alisema Bashe.
Aidha amebainisha mpango wa wizara
kununua mazao kutoka kwa wakulima, kwa lengo la kuwaepusha wakulima na hasara
za kuuza mazao yao kwa bei ya chini,”Mwenyekiti wa Skimu kasema mnauza mpunga
kwa elfu sitini kwa gunia, serikali itafanya itauangalia mpunga mliovuna na
tutanunua gunia moja la kg 90 kwa
shilingi 81,000 na serikali itaununua wote” alisema Bashe.
Pia, alitembelea shamba la uzalishaji wa kahawa Avivi katika Kata ya
Kilagano, wilaya ya Songea, na kuwasihi wawekezaji kuchangia maendeleo ya jamii
kwa kuwachimbia visima vya umwagiliaji.
Ziara ya Waziri Bashe inaendelea
katika mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kukagua hatua zilizofikiwa katika
uibuaji, ujenzi, na uendelezaji wa miradi ya kilimo.
Mkoani Ruvuma, waziri Baahe
anaendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya kilimo, ikiwa ni pamoja na
kutembelea wakulima wa mpunga katika Kata ya Njalila.
Bonde la mto Njalila lipo wilaya ya Songea, kata ya Kilagano, kijiji cha
Kilagano na limepakana na wilaya ya Mbinga upande wa mashariki mwa bonde,
linapatikana umbali wa kilometa 93 kutoka manispaa ya Songea, ambalo linatumika
kwa shughuli za kijamii na kiuchumi kama kilimo cha mazao mchanganyiko (mpunga,
mahindi, ndizi, miwa, mbogamboga) na ufugaji.
Kilimo hufanyika zaidi wakati wa masika, lakini hupungua wakati wa kiangazi
kutokana na uhaba wa maji ya umwagiliaji.
Barabara ya kwenda bonde hilo ina urefu wa km 93 kutoka Manispaa ya Songea,
lakini kipande cha km 35 kina changamoto za madaraja/makalavati 5 na sehemu
tatu zenye miinuko na udongo wa utelezi wakati wa masika. Barabara hii ipo
chini ya TANROAD na TARURA na imeingizwa katika mpango wa maendeleo. Mradi huu
unahitaji barabara za mashambani ili kuiunganisha skimu na barabara ya Njalila
na Ndatila kwa ajili ya kufikisha mazao sokoni na miji Jirani.
No comments