WAKALA WA VIPIMO ZANZIBAR WAJIFUNZA KUTOKA WMA BARA
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai
(katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa Mussa Kongola, Msimamizi wa Mtambo
wa kuchakata gesi asilia wa Kampuni ya Maurel & Prom, Madimba Mtwara
(kushoto). Kulia ni Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara (WMA), Saad
Haruna. Simai alitembelea Mtwara Agosti 16 na 17, 2024 kujifunza namna WMA
mkoani humo inavyotekeleza majukumu yake.Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai amefanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara kwa lengo la kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) ambapo amekiri kunufaika zaidi ya alivyotarajia.
Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake, Agosti 17, 2024 Simai amesema lengo hasa la ziara hiyo lilikuwa kutembelea eneo linalotumiwa na Wakala wa Vipimo Mtwara kwa ajili ya ukaguzi na uhakiki wa magari ya kusafirishia mafuta ili ZAWEMA ikatumie teknolojia hiyo na kuboresha zaidi huko Zanzibar.
“Hata hivyo, ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa kwetu kwa sababu tumepata zaidi ya kile tulichokusudia,” amesema.
Akifafanua, Simai ameeleza kwamba mbali na kujionea na kujifunza kuhusu uanzishaji wa mtambo wa ukaguzi na uhakiki wa magari ya kusafirishia mafuta, amepata fursa ya kutembelea maeneo mengine ambako WMA hutekeleza majukumu yake ikiwemo Bandari ya Mtwara na katika eneo ambalo gesi asilia huvunwa na kuchakatwa huko Madimba.
Amesema, matarajio yake ni kwenda
kuibua miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa eneo la ukaguzi wa magari ya
mafuta ambao utaenda sanjari na ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa dira
za maji kwa njia ya kielektroniki. “Hata hivyo kwa nilichokiona huku WMA
Mtwara, iko haja kutumia mtambo wa kawaida pia pamoja na uwepo wa huo wa
kielektroniki,” ameeleza.
Simai amemshukuru Mtendaji Mkuu wa WMA Tanzania Bara, Alban Kihulla kwa
ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa ZAWEMA katika kuhakikisha wanatimiza
matarajio yao ya kutekeleza majukumu ya uhakiki vipimo kwa ufanisi na tija kwa
manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Awali, akieleza kuhusu majukumu yanayotekelezwa na WMA mkoani Mtwara,
Meneja wa Mkoa wa Wakala hiyo, Saad Haruna amesema ni pamoja na uhakiki wa
vipimo ambavyo hutumika katika sekta za kilimo, biashara, mazingira pamoja na
usalama.
Katika sekta ya kilimo, Haruna amesema WMA huhakiki mizani zinazotumika
wakati wa kununua mazao pamoja na wakati wa kuyasafirisha.
Aidha, kwa upande wa biashara amesema WMA inawajibika kuhakiki vipimo
vinavyohusiana na sekta hiyo ambapo ametoa mfano wa mafuta yanayosafirishwa
kutoka nchi za nje kuletwa nchini kupitia Bandari ya Mtwara.
“WMA hufanya uhakiki kuanzia Bandarini mafuta yanaposhushwa na kupita
kwenye kipimo maalum kijulikanacho kama ‘flow meter’ kwa lugha ya kigeni, zoezi
ambalo huendelea kufanyika katika matenki ya kuhifadhi mafuta, vituo vya mafuta
na katika pampu zinazotumika kujaza mafuta katika magari.”
Vilevile, Haruna amesema jukumu lingine ambalo hutekelezwa na WMA mkoani
humo ni kuhakiki dira mpya za maji ambazo hutumika kuwafungia wateja maji
pamoja na zile ambazo zilikwishaanza kutumika.
Pia, katika sekta ndogo ya gesi asilia, amesema WMA huwajibika kuhakiki
vipimo vyote vinavyotumika kupima kiwango cha nishati hiyo kuanzia inapovunwa
hadi kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili
ya kuzalisha umeme, kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) na hata kile kinachopelekwa kwa Kampuni kubwa ya kuzalisha
saruji ya Dangote.
Akizungumzia malengo ya kuhakiki vipimo, Haruna amesema ni jukumu la
Serikali kupitia Wakala wa Vipimo, kuhakikisha pande zote zinalindwa yaani
mlaji apate bidhaa kadri alivyolipia bila kupunjwa ilhali muuzaji apate malipo
stahiki kulingana na kiwango alichouza.
Kwa upande wake, mmoja wa Wasimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia
katika Kiwanda kilichoko Madimba, Mussa Kongola ameipongeza Serikali kwa
kuanzisha Wakala wa Vipimo akisema inatekeleza majukumu muhimu sana
yanayozinufaisha pande zote.
“Uwepo wa jicho la tatu ni muhimu sana ili kuhakikisha pande zote
zinanufaika kwa kupata kilicho stahiki na kwakweli nimewafahamu WMA kwa muda
mrefu, kazi yao ni njema sana,” amesisitiza.
Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa takwimu kutoka TPDC, asilimia 60 ya umeme
unaozalishwa nchini kupitia TANESCO hutokana na gesi asilia. Aidha, korosho
ambazo huzalishwa kwa wingi mkoani Mtwara ni moja ya mazao ya kimkakati
yanayolimwa nchini. Vilevile, uwepo wa Bandari ya Mtwara pamoja na maeneo
mengine mbalimbali ambayo yanatumia vipimo, vyote vinadhihirisha umuhimu wa
uwepo wa Wakala wa Vipimo kwa manufaa ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa
ujumla.
Utendaji mzuri wa wataalamu wa Wakala wa Vipimo Tanzania Bara umekuwa
ukivutia nchi mbalimbali kuja kujifunza namna bora ya kuendesha sekta hiyo.
Ziara ya mafunzo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar
imefanyika mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam au Mkoa mwingine kulingana na
ukubwa wa kazi zinazotekelezwa na ZAWEMA ambao unaelezwa kuwiana na majukumu
yanayotekelezwa na WMA Mtwara.
Mojawapo ya Mita zinazopima kiwango cha gesi asilia inayovunwa na
kuchakatwa katika kiwanda kilichoko Madimba, Mtwara, ikiwa na nembo/alama ya
Wakala wa Vipimo (WMA) kuthibitisha kwamba Mita hiyo imehakikiwa na Wakala
hiyo. Taswira hii ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga
kujifunza namna WMA Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta
mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai
(mwenye fulana nyeusi-kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo Bandari ya
Mtwara. Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza namna majukumu yanayotekelezwa na
Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta mbalimbali.
Mojawapo ya Mita zinazopima uzito wa magari yenye makaa yam awe kutoka
katika Bandari ya Mtwara, ikiwa na nembo/alama ya Wakala wa Vipimo (WMA)
kuthibitisha kwamba Mita hiyo imehakikiwa na Wakala hiyo. Taswira hii
ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala
wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga kujifunza namna WMA
Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai
(mwenye fulana nyeusi-kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo Bandari ya
Mtwara. Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza namna majukumu yanayotekelezwa na
Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta mbalimbali.
Gari lililobeba makaa ya mawe likipimwa uzito katika Bandari ya Mtwara kwa
kutumia Mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo (WMA). Taswira hii
ilichukuliwa Agosti 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala
wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai, ilyolenga kujifunza namna WMA
Mtwara inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai
(katikati), akisisitiza jambo kwa Mussa Kongola, Msimamizi wa Mtambo wa
kuchakata gesi asilia wa Kampuni ya Maurel & Prom, Madimba Mtwara (kushoto)
na Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara (WMA), Saad Haruna. Simai
alitembelea kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia Agosti 17, 2024 kujifunza
namna WMA mkoani humo inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai
(kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo katika kiwanda cha kuchakata gesi
asilia kilichoko Madimba, Mtwara, Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza
majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta
mbalimbali.

No comments