NAIBU KATIBU MKUU DKT. OMAR AZINDUA HUDUMA ZA MAGARI YA KAMPUNI YA TFC NA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA KUSAMBAZA MBOLEA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (anayeshughulia Mazao na Usalama wa Chakula), Dkt. Hussein Mohamed Omar amezindua magari matatu yatakayotumika katika shughuli za usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa wakulima kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Bw. Samuel Mshote katika
Makao Makuu ya Ofisi za Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), tarehe 24 Desemba
2024, ambapo Dkt. Omar amesema kuwa uwepo wa magari hayo ni jitihada
zinazoendelea kufanywa na Serikali ili kuhakikisha huduma za usambazaji wa
mbolea za ruzuku zinaimarika na kuwafikia wakulima wote nchini.
“Magari haya yataweza kuwafikia wakulima kule walipo, jambo ambalo
litapunguza gharama kwa mkulima kuja mjini na kuongeza upatikanaji wa mbolea
kwa wingi”, ameeleza Dkt. Omar. Aidha,
amesisitiza magari hayo yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhudumia
usafirishaji wa mbolea kwa wakulima hadi walipo ili wanufaiike na kuongeza
uzalishaji.
Pamoja na uzinduzi wa magari hayo, Dkt. Omar amezindua mfumo wa
kieletroniki utakaowezesha TFC kupata taarifa zake za uuzaji na uzambazaji wa
mbolea katika maeneo yote nchini kwa wakati.
Ameeleza kuwa mfumo huo utaongeza ufanisi wa kazi kwani matumizi ya
teknolojia ni njia rahisi na ya haraka katika upataji wa taarifa za kila siku
za usambazaji na mauzo ya mbolea.
Aidha, Dkt. Omar alikutana na Watumishi wa TFC na kuwaeleza kuwa Serikali
imeiamini TFC na kuipa mtaji hivyo ni jukumu la watumishi kufanya kazi kwa
bidii ili imani hiyo ionekane kwa matokeo mazuri. Amewataka watumishi kuwa timu moja, kufanya
kazi kwa ushirikiano, kutimiza wajibu na kila mmoja katika majukumu yake
kuhakikisha anakuwa na mchango wa kukuza na kuendeleza kampuni.
Pia ameitaka TFC kuendelea kushirikiana na wadau wengine katika kusaidia
wakulima kufahamu afya ya udongo ya maeneo yao hatua itakayowezesha kufahamu ni
aina gani ya mbolea mkulima atumie kulingana na afya ya udongo.



No comments