Header Ads

RC MTWARA AIPONGEZA WIZARA YA KILIMO KWA ZOEZI LA UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa zoezi la upimaji wa afya ya udongo katika Mkoa wa Mtwara pamoja na Mkoa wa Lindi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Kitaifa wa kuimarisha Sekta ya Kilimo.

Mhe. Kanali Sawala ametoa pongezi hizo tarehe 9 Januari, 2026 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika mkoani Mtwara, ambapo amesisitiza kuwa upimaji wa afya ya udongo ni nguzo muhimu ya uzalishaji wa kilimo chenye tija na endelevu.

Amesema kuwa zoezi hilo litawasaidia wakulima kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya udongo wao, jambo litakalowezesha matumizi sahihi ya pembejeo na kuongeza uzalishaji wa mazao. 

Aidha, ametoa rai kwa Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Maafisa Ugani pamoja na viongozi wengine wa Serikali za mitaa kuhakikisha wanawapokea na kushirikiana kikamilifu na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo watakaokuwa na jukumu la kutekeleza zoezi hilo mkoani Mtwara.

Ameongeza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kudijitalisha Sekta ya Kilimo, sambamba na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwajali wakulima, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Wizara ya Kilimo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo, Mha. Godliver Mosha, amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha zoezi la upimaji wa afya ya udongo linafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Mtwara.  Ameeleza kuwa upimaji huo utasaidia kubaini kiwango cha rutuba ya udongo, hali itakayowawezesha wakulima kutumia mbolea na virutubisho kwa kiasi sahihi.

Aidha, Mha. Mosha  amesema kuwa katika mkoa wa Mtwara jumla ya Sampuli profile pits 172 na sampuli mchanganyiko 1,746 za udongo zitachukuliwa, hivyo kuchochea maendeleo ya Sekta ya Kilimo kwa ujumla. 

No comments

Powered by Blogger.