Header Ads

NAIBU WAZIRI WA KILIMO DAVID SILINDE AFUNGUA KIWANDA CHA KUUNGANISHA MATREKTA MOROGORO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amefungua rasmi Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta cha TATDC kilichopo Mvomero, mkoani Morogoro Juni 16, 2026.

Ufunguzi huo umeashiria mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshmiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kuleta mageuzi makubwa ya kilimo nchini kupitia uwekezaji wa viwanda na teknolojia ya kisasa.

Mhe. Silinde amebainisha kuwa kiwanda hiki kinaenda kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa zana za kilimo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa jangwa la Sahara (EAC na SADC), huku akiongeza kuwa wakulima wanaenda kupata matrekta bora, vipuri, na huduma za matengenezo kwa urahisi na kwa bei nafuu kabisa.” 

Kiwanda hiki kina mchango mkubwa katika kufikia Ajenda ya Kilimo 10/30 (kukuza Sekta ya Kilimo kwa 10% ifikapo 2030).  Naibu Waziri Silinde ameeleza kuwa ni dhahiri mapinduzi ya kilimo hayawezi kupatikana kwa jembe la mkono kama nchi na kwamba tunahitaji mitambo ya kisasa, mbegu bora, na umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji kwa ekari na kupunguza gharama za kilimo kwa mkulima.

Uwekezaji huu unaenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuchochea uchumi wa Taifa kwa kuwa kiwanda kitasaidia kuhamisha teknolojia kwa wahandisi wazalendo, kukuza viwanda vidogo vya vipuri, na kuzalisha mamia ya fursa za ajira na biashara kwa vijana wetu nchini.

Akihitimisha, Mhe. Silinde ametoa wito kwa taasisi za kifedha kutoa mikopo nafuu ya zana hizi, na kuwataka wakulima pamoja na sekta binafsi kuchangamkia fursa hii adhimu. Na ameipongeza TATDC kwa hatua hii muhimu. 

No comments

Powered by Blogger.