Header Ads

ELIMU ZAIDI INAHATAJIKA ILI KUKABILIANA NA UTAPIAMLO TANGA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, yatakayofanyika kitaifa mkoani Tanga. 

....................................

Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga.

WANANCHI wanakabiliwa na changamoto za utapia mlo hasa  kwa watoto wadogo na hii inasababishwa na ukosefu wa lishe bora, ili kukabiliana na hili inahatajika elimu zaidi  kwa jamii ya ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, yatakayofanyika kitaifa mkoani Tanga  na yanatarajia kuanza Oktoba10 na kuhitimishwa Oktoba 16, 2026 katika Viwanja vya Usagara.

Akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo, Dk. Burian amesema kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha matumizi ya sayansi, teknolojia, utafiti na maarifa ya kisasa katika kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

“Kaulimbiu hii inahimiza matumizi ya ubunifu, sayansi, teknolojia, utafiti na maarifa ya kisasa katika kuongeza uzalishaji na tija ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha, salama na chenye virutubisho kwa jamii ya sasa na kizazi kijacho,” amesema.

Amesema maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa wakulima, wafugaji na wadau wengine kujifunza teknolojia zinazoweza kuboresha uzalishaji, uhifadhi na upatikanaji wa chakula bora na salama.

Pia Dk .Burian amewataka wananchi kuzingatia ulaji wa makundi yote ya vyakula, yakiwemo mboga za majani, matunda, nafaka, nyama na jamii ya mikunde, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga jamii yenye afya na kupunguza changamoto za lishe.

Amesema shughuli mbalimbali zitafanyika ndani na nje ya uwanja, zikiwemo maonyesho ya teknolojia za kuongeza uzalishaji na tija, pamoja na kuboresha uhifadhi wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Mazao na Usalama wa Chakula katika Wizara ya Kilimo, Theoford Ndunguru, amesema kiwango cha utoshelevu wa chakula cha asilimia 133 kinaonesha kuwa uzalishaji nchini umezidi mahitaji, lakini bado kuna umuhimu wa kuhakikisha chakula hicho kina virutubisho vya kutosha.

Amesema Wizara ya Kilimo na taasisi za utafiti zinaimarisha matumizi ya teknolojia ya biofortification, inayolenga kuzalisha aina za mazao yenye virutubisho zaidi, pamoja na industrial fortification, ambapo virutubisho huongezwa kwenye vyakula wakati wa uchakataji, kama vile unga wa mahindi, ili kusaidia kukabiliana na utapiamlo.

Mpaka sasa uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini umeendelea kuimarika na kufikia kiwango cha utoshelevu wa asilimia 133 katika msimu wa kilimo wa 2025/2026, kutoka asilimia 130 katika mwaka uliotangulia, hatua inayoonesha kuongezeka kwa uwezo wa Taifa kujitosheleza kwa chakula.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, akisisitiza jambo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji wa Mazao na Usalama wa Chakula katika Wizara ya Kilimo, Theoford Ndunguru, akizungumza.


 

No comments

Powered by Blogger.