JIFUNZE KILIMO BORA CHA BAMIA NA MIONGOZO YAKE
Kilimo cha bamia
nchini Tanzania kimekuwa ni nyenzo muhimu kwa wakulima kujipatia kipato, lakini
mafanikio hayapatikani bila ujuzi na mipango sahihi. Likiwa kama zao lenye
lishe nzuri na matumizi mengi, bamia ina uwezo wa kuleta manufaa makubwa kwa
wakulima na walaji.
Bamia ni zao lenye
mchango mkubwa katika afya ya mwanadamu na ni chanzo muhimu cha vitamini na
madini ya potasiam na chokaa ambayo ni muhimu kwa afya ya mifupa, meno na
husaidia ufanyaji kazi mzuri wa misuli. Wakulima walio wengi hususan wakulima
wadogo, hutegemea zao hili kama chanzo cha kipato kutokana na kutumiwa na
watanzania walio wengi.
Hata hivyo, ni muhimu
kujua hatua zote zinazohitajika kufanya kilimo cha bamia ili kiwe na mafanikio.
Kwenye mwongozo huu, tutadurusu vipengele muhimu vya kilimo cha bamia nchini
Tanzania, ikijumuisha: maandalizi ya shamba, jinsi ya kupanda, mahitaji ya
udongo, mahitaji ya mbolea, udhibiti wa wadudu na magonjwa, na mbinu za kuvuna.
Kupitia somo hili,
natumai utajifunza maarifa mahsusi yatakayokuwezesha kufikia mavuno ya bamia
yenye mafanikio na kuongeza kipato chako. Endelea …
Bamia aina ya
Emerald green
Eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia
Bamia ni zao
linalolimwa katika maeneo mengi nchini. Baadhi ya maeneo yanayolima zao la bamia kwa Tanzania ni pamoja na mikoa ya
Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani na Mbeya.
Ni muhimu kuchagua
eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia kabla ya kuanza uzalishaji. Ni vyema eneo
litakalotumika katika kilimo cha bamia liwe na urahisi wa upatikanaji maji
kurahisisha umwagiliaji.
Vilevile shamba liwe
lenye kufikika kwa urahisi ili kufanya wepesi katika kuhudumia shamba na
usafirishaji wa mazao kwenda sokoni au kufikiwa kwa urahisi na wanunuzi
wanaofuata mazao shambani.
Zao la bamia
hushambuliwa sana na minyoo fundo (nematodes). Hivyo usichague eneo ambalo
limetoka kutumika katika kilimo cha mazao yanayoweza kushambuliwa na minyoo
fundo kama vile viazi vitamu, nyanya, bilinganya na pilipili hoho.
Kwa tahadhari unaweza
kulima zao hili katika eneo ambalo limetoka kutumika kwa kilimo cha mazao ya
nafaka kama vile mahindi na mtama kwa kuwa mazao haya
hayashambuliwi na minyoo fundo.
Mazingira yanayostawisha bamia vizuri
Hali ya Hewa na Mwinuko
Bamia ni zao
linalopendelea hali ya joto hivyo hustawi katika maeneo yenye hali joto kuanzia
nyuzi joto za sentigredi 21 hadi 35. Ustawi mzuri zaidi huonekana katika maeneo
yenye joto la nyuzi za sentigredi 21 mpaka 30. Hali joto zaidi ya nyuzi za
sentigredi 42 huweza kusababisha kudondoka kwa maua. Bamia hustawi vizuri
katika maeneo ya mwinuko tofauti hadi mita 1000 kutoka usawa wa bahari yenye
mvua za wastani.
Udongo
Zao la bamia hustawi
katika udongo wa aina nyingi wenye rutuba, kina, uwezo wa kuifadhi maji vizuri
na usiotuamisha maji. Hata hivyo zao hili hufanya vizuri zaidi linapolimwa
katika udongo wa tifutifu yenye kichanga wenye rutuba ya kutosha na tindikali
kuanzia Ph 5.8 hadi 6.5. Mbegu za bamia hushindwa kuota kabisa pale joto la
udongo linapokuwa chini ya nyuzi za sentigredi 16.
Maandalizi ya shamba la Bamia
Muda wa Kuandaa
Shamba la bamia
liandaliwe mapema mwezi mmoja kabla ya kupanda ili kuruhusu magugu na mabaki ya
mazao kuoza vizuri. Kwa kilimo cha kutegemea mvua ni vyema maandalizi yaanze
mapema kabla ya kuanza kwa mvua za masika. Inashauriwa kuanza maandalizi mapema
mwezi Januari. Kwa kilimo cha umwagiliaji unaweza kuanza maandalizi muda wowote
kulingana na mahitaji na soko unalolilenga.
Namna ya Kuandaa shamba
Shamba huandaliwa kwa
kufyeka nyasi, kung’oa visiki na kulima kabla ya kupima na kuweka matuta.
(i) Kulima
Shamba hulimwa kwa
kutumia jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers au
matrekta. Matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers na matrekta
hurahisisha shughuli ya kulima na kuifanya iwe na ufanisi kwani hukatua udongo
vizuri na kuufanya uwe tifutifu.
Unapotumia jembe la
mkono katika kulima hakikisha unakatua udongo katika kina cha kutosha sm 20
mpaka sm 30 na kulainisha mabonge. Udongo uliokatuliwa vizuri hupitisha hewa
inayohitajika na mmea, hurahisisha ukuaji wa mizizi na kuifadhi maji vizuri.
(ii) Kupima shamba (field layout)
Ni muhimu kuanza
kupima shamba kabla ya kuanza kuandaa matuta ili kupata matuta yaliyo katika
mpangilio mzuri na mistari ya mimea shambani iliyonyooka vizuri. Kabla ya
kupima matuta ni muhimu pia kujua nafasi ya kupandia utakayo tumia ili kupata
ukubwa sahihi wa kila tuta.
Kwa mfano kwa nafasi
ya kupandia ya sm 60 × sm 40 kwa matuta makubwa unaweza kutengeneza kila tuta
katika upana wa sm 1.2 na urefu wowote. Acha nafasi ya m 1 kuzunguka
shamba na njia kila baada ya tuta upana wa sm 50. Tumia Tape measure au
kamba yenye vipimo kupima shamba huku ukiweka alama za matuta na njia kwa kuchomeka
mambo (pegs) katika kila kona ya tuta na kuzungushia kamba.
(iii) Kuweka matuta
Inashauliwa kupanda
bamia katika matuta ili kusaidia mizizi kukua vizuri na udongo kuhifadhi maji.
Wakati wa kiangazi, tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya maji
yaweze kukaa kwenye udongo na wakati wa masika matuta yainuliwe kidogo toka
kwenye usawa wa ardhi ili kuzuia maji yasituame.
Matuta yanaweza kuwa
makubwa au madogo kulingana na matakwa ya mkulima. Matuta makubwa hupandwa
mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari mmoja. Tengeneza matuta kwa
kufuata alama zilizowekwa wakati wa kupima shamba.
Jinsi ya Kupanda Bamia
Zao la bamia huweza
kupandwa moja kwa moja shambani au kwa kuanzia kitaluni. Hata hivyo kama mbegu
zako zinauwezo mzuri wa kuota, ni bora ukapanda mbegu moja kwa moja ili
kupunguza gharama zisizo na msingi. Na ikiwa utaamua au kulazimika kuanzia
kitaluni hakikisha unafuata taratibu zote za uandaaji na utunzaji wa kitalu. Na
Upandikize miche pindi inapokua na majani halisi matatu hadi manne.
Maandalizi ya Mbegu za bamia
Unahitaji mbegu za
bamia kiasi cha kilo moja (kg 1) mpaka moja na nusu (kg 1.5) kupanda eneo la
ekari moja. Hata hivyo kiasi hiki kinaweza kuathiriwa na nafasi ya kupandia na
uotaji wa mbegu.
Mbegu za bamia ni
ngumu kidogo katika kuota hivyo ni vyema ziandaliwe ili kurahisisha uotaji
wake. Mbegu za bamia huandaliwa kwa kuziloweka katika maji ya vuguvugu kwa muda
wa masaa ishirini na nne ili kuchochea uotaji. Mbegu za bamia huchukua muda wa
siku 5 hadi 10 kuota.
Aina ya mbegu za bamia
Kuna aina tofauti za
mbegu za bamia zinazopatikana Tanzania kama vile Clemson Spineless, Emerald
Green, White Velvet, Perkins Mammoth na Dwarf Prolific. Mbegu ambazo hutumika
na wengi ni
·
Clemson spineless: mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa mita 1 hadi 1.5 na kuzaa
bamia za kijani zenye urefu karibu sm 15. Huchukua siku 55 hadi 58 kuanza
kuvuna.
·
Emerald green:
mbegu hii ina tabia ya kukua hadi urefu wa m 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye
urefu wa sm 18 hadi 20. Huchukua siku 58 hadi 60 kuanza kuvuna.
·
White velvet:
mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa m 1.5 hadi 1.8 na kuzaa bamia ndefu,
nyembamba, zilizochongoka na zenye urefu wa sm 15 hadi 18.
Bamia
aina ya Clemson spineless
Nafasi ya Kupandia bamia
Bamia huweza kupandwa
katika nafasi tofauti kuanzia sm 60 hadi 80 kati ya mstari na mstari na sm 30
hadi 50 kutoka shimo hadi shimo. Hakikisha unafuata maelekezo ya mbegu husika
juu ya nafasi pendekezwa.
Hatua za Upandaji wa bamia
Unaweza kufuata hatua
zifuatazo katika upanzi wa mbegu za bamia shambani:
1. Mwagia maji mengi shambani masaa kumi na mbili
kabla ya kupanda mbegu ili kulainisha udongo na kurahisisha upanzi.
2. Chimba mashimo ya kupandia yenye kina cha sm 2
hadi 3 katika nafasi iliyopendekezwa kwa mbegu itakayotumika mistari miwili
miwili kila tuta kwa kutumia kamba iliyowekwa vipimo.
3. Weka viganja viwili vya mkono vya samadi
iliyoiva katika shimo la kupandia kisha changanya na udongo kupata mchanganyiko
mzuri. Kwa mbolea ya kupandia kama DAP weka kizibo kimoja cha soda katika kila
shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupanda
mbegu. Kiasi cha kilo hamsini za mbolea ya DAP kinatosha kutumika katika eneo
la ekari moja.
4. Panda mbegu mbili katika kila shimo, fukia kwa
udongo mwepesi, shindilia na kisha mwagia maji.
Utunzaji wa bamia baada ya kupanda
Matunzo ya shamba ni
muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza kupata kutoka
shambani. Shamba ambalo halipati matunzo mazuri hata kama mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado
yatakuwa hafifu.
Matunzo ya shamba
hujumuisha mambo yafuatayo …
Umwagiliaji
Kuna njia tofauti za
umwagiliaji ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji wa bustani ya bamia
kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip irrigation), wa njia ya mifereji
na umwagiliaji wa kutumia can.
Maamuzi ya njia ya
kumwagilia utakayoichagua nashauri yazingatie tija ya mradi husika. Usipoteze
pesa uliyowekeza kwenye shamba lako kwa kulimwagilia kwa njia duni; badala yake
weka miundombinu mizuri itakayokuletea tija katika uzalishaji wako.
Ratiba ya umwagiliaji
izingatie mambo yafuatayo: aina ya udongo, hatua ya ukuaji wa mimea yako na
msimu wa uzalishaji.
Udongo wa kichanga
unapoteza maji kwa haraka sana; bamia zinahitaji maji mengi zikiwa katika hatua
ya kutoa maua na matunda; na wakati wa kiangazi upotevu wa maji ardhini ni
mkubwa sana. Hivyo basi ni muhimu sana kuhakikisha shamba lako linapata maji
kwa wakati stahiki kwa kuzingatia sababu kama hizi.
Kupandikiza na Kupunguzia miche
Kagua uotaji wa mbegu
siku 10 hadi 14 tangu kupanda. Pandikiza mashimo yote ambayo hayakuota, mapema
kadri utakavyoweza.
Unaweza kung’oa miche
iliyozidi kwenye shimo moja na kupandikiza kwenye mashimo ambayo hayakuota.
Hatahivyo hili lifanyike anagalau wiki tatu tangu kupanda wakati mimea imefikia
urefu wa sm 10 mpaka 15.
Mahitaji ya mbolea za kupandia na kukuzia
Kwa mbolea ya kupandia
kama DAP: Kiasi cha kilo 50 za mbolea ya DAP kinatosha kutumika katika eneo la
ekari moja. Weka kizibo kimoja cha soda katika kila shimo la kupandia kisha
fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupanda mbegu.
Kwa mbolea ya kukuzia
tunayoshauri utumie NPK kiasi cha kilo 50 kwa ekari. Mbolea ya NPK hutoa
virutubisho vitatu muhimu vya Naitrojeni, Fosfeti na Potash. Mbolea hii iwe na
uwiano wa 1:1:2 kwani zao hili huhitaji uwiano mzuri wa potasiam na virutubisho
vingine ili kupata matunda. Endapo naitrojeni itazidi, mmea utazalisha majani
mengi pasipo matunda na kusababisha mavuno hafifu.
Weka mbolea ya kukuzia wiki sita tangu kupanda kwa kiwango cha kifuniko kimoja cha soda kuzunguka shina sm 5 kutoka shina lilipo na kurudia kuweka tena kila baada ya wiki mbili hadi mwisho wa kuvuna.
Kupiga Dawa za wadudu na magonjwa
i. Dawa za ukungu
Uchaguzi wa dawa za
ukungu hufuatana na magonjwa yanayoshambulia zao husika hivyo ni vema kujua
magonjwa yanayoshambulia zao la bamia kabla ya kuchagua dawa za kutumia kama
kinga au tiba pale magonjwa yanapojitokeza. Unaweza kuanza kupiga dawa ya
ukungu wiki moja hadi mbili tangu miche kuota na kurudia kila baada ya wiki
moja hadi mbili kutegemeana na maelekezo ya dawa husika.
ii. Dawa za kuua
wadudu
Nyunyizia dawa ya kuua
wadudu baada ya kuona wadudu waharibifu katika shamba lako ili kuweza kuchagua
dawa sahihi ya kudhibiti aina ya wadudu waliovamia bustani yako.
Kudhibiti Magugu
Palizi ifanyike
kuanzia wiki ya nne tangu kupanda na kurudia kila baada wiki mbii hadi tatu.
Hakikisha hakuna magugu bustanini katika kipindi cha kutoka maua na
kutengenezwa kwa matunda ili kuepusha ushindani wa mazao na magugu katika
kupata maji, rutuba, hewa na mwanga. Magugu pia hutoa fursa kwa vimelea vya
magonjwa na wadudu kujificha na kufanya mashambulizi kwa mazao.
Unaweza kudhibiti
magugu kwa kutumia matandazo (mulch), au kwa kupalilia kutumia jembe la mkono
au dawa za viuagugu. Ni muhimu kuondoa magugu na kuweka shamba katika hali ya
usafi kila wakati.
Kuweka Matandazo
Matandazo husaidia
kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika udongo. Kwa matokeo
mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka matandazo kwa kuyatandaza
katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15 maeneo yote ya tuta kuzunguka
mashimo ya miche.
Matandazo ya asili
kama mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao yanaweza kuwekwa
kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya kupandia au baada ya
kupandikiza. Matandazo ya plastiki huwekwa mapema kabla ya kupandikiza baada ya
kuandaa matuta.
Uvunaji wa Bamia
Kiwango cha mavuno
Ekari moja ya bamia
hutoa mavuno ya wastani wa tani tano mpaka nane.
Hata hivyo kiwango cha
mavuno ya bamia kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba, uwezo wa kuzaa
wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba. Mbegu za aina tofauti
zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa tofauti. Vilevile mashamba
tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na kupata matunzo ya viwango tofauti
huwa na kiwango tofauti cha mavuno.
Muda wa Kuvuna
Bamia huchukua siku 50
hadi 60 kuanza kuvuna. Huwa tayari kuvunwa siku tano tangu kutoka kwa maua
zikiwa bado changa na zenye urefu wa sm 5 hadi 10 kutegemeana na aina ya mbegu.
Hivyo basi inashauriwa kuvuna bamia kila baada ya siku tatu tangu mvuno wa
kwanza wakati wa asubuhi. Uvunaji wa bamia unaweza kuendelea kwa muda wa siku 30
hadi 40 tangu mvuno wa kwanza.
Bamia tayari kwa
kuvuna
Jinsi ya kuvuna bamia
1. Andaa vifaa na vyombo vya kuvunia kama vile
kisu, mkasi na ndoo au chombo chochote cha plastiki kwa kuvisafisha kwa maji
safi na sabuni.
2. Andaa sehemu utakayokuwa unaweka bamia wakati
wa kuvuna iliyo kivulini karibu na shamba na utandike turubai.
3. Wakati wa kuvuna kata kikonyo cha bamia karibu
na tawi linaloshikilia tunda kisha weka tunda kwenye ndoo. Hakikisha unavuna
bamia na kikonyo chake ili zisiharibike kwa urahisi.
4. Ndoo inapojaa bamia beba ukazitandaze katika
turubai lililo tandikwa karibu na bustani ili zipate hewa na zipoe kutoka
katika joto la shamba (field heat) kabla ya kuzipakia.
5. Safisha vizuri vyombo vya kuvunia kwa maji
safi na sabuni kila baada ya kumaliza siku ya kuvuna ili kuzuia vimelea vya
magonjwa.
Mambo ya kuzingatia wakati wa uvunaji
Usiache bamia zikomae
kabla ya kuvuna kwa sababu bamia zilizokomaa huwa ngumu na zenye nyuzi nyuzi na
hivyo hazina soko kwa matumizi ya nyumbani. Vilevile kuacha bamia zikomae
katika mmea husababisha mmea kuacha kuzaa mapema na hivyo mavuno huwa madogo.
Tumia kisu au mkasi
wakati wa kuvuna ili kuepuka kuathiri shina na kusumbua mizizi ya mmea.
Vilevile usivune bamia zinazoonyesha dalili ya kuoza au kuathiriwa na wadudu.
Kwa baadhi ya watu bamia huweza kusababisha muwasho wa ngozi hivyo hakikisha
unavaa suruali ndefu na shati la mikono mirefu wakati wa kuvuna.
Bamia zilizochumwa
Soko la Bamia na Bei zake
Bamia ni moja ya mazao
ya mboga yanayozalishwa na kuliwa kwa wingi nchini Tanzania. Zao hili
linapatikana katika maeneo mengi ya nchi na linauzwa katika masoko mengi
yaliyopo kote nchini. Soko la bamia Tanzania linategemea mahitaji ya ndani na
nje ya nchi.
Katika soko la ndani,
bamia huliwa na watu wengi kutokana na ladha yake nzuri na kustawi kwa zao hilo
katika maeneo mengi ya Tanzania. Wachuuzi wa mboga na matunda huuza bamia
kwenye masoko ya miji mikubwa, maduka ya mboga na matunda, na kwenye vituo vya
mabasi. Bei ya bamia inategemea na msimu, ugumu wa upatikanaji wake, na eneo la
soko.
Mfano kwa mwezi Oktoba
2023, kiroba cha kilo 50 cha bamia kilikuwa kinauzwa kati ya TZS 10,000 na TZS
25,000 katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Morogoro.
Katika soko la nje,
Tanzania ina fursa ya kuuza bamia nchi za nje kutokana na ubora wake na
mahitaji ya kimataifa. Bamia huuza hasa katika nchi jirani kama vile Kenya,
Uganda, Rwanda, na Burundi. Pia, Tanzania ina fursa ya kuuza bamia nchi za
Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati.
Hata hivyo, changamoto
za soko la bamia Tanzania ni pamoja na ukosefu wa teknolojia bora ya kuhifadhi
na usafirishaji wa zao hilo, uzalishaji mdogo na usimamizi duni wa ubora wa
zao. Serikali inajitahidi kusaidia wakulima wa bamia kupitia sera zinazolenga
kuinua uzalishaji na ubora wa zao hilo, kuboresha mifumo ya masoko, na kutoa
mafunzo kwa wakulima juu ya mbinu bora za uzalishaji na usimamizi wa ubora.
Faida za bamia mwilini
Bamia ina faida nyingi
kwa afya ya binadamu kutokana na virutubisho na madini ambayo inayo. Baadhi ya
faida za bamia kwa mwili ni pamoja na:
1. Kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo: Bamia
ina kiwango kikubwa cha nyuzinyuzi na madini ya potassium ambayo husaidia
kudhibiti shinikizo la damu na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
2. Kuimarisha mfumo wa kinga: Bamia ina kiwango
kikubwa cha vitamini C na antioxidants ambazo husaidia kuimarisha mfumo wa
kinga wa mwili na kupambana na magonjwa mbalimbali.
3. Kuimarisha afya ya ngozi: Bamia ina vitamini
C, A na antioxidants ambavyo husaidia kudumisha afya ya ngozi na kuzuia
uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua na uchafu.
4. Kupunguza hatari ya kisukari: Bamia ina
nyuzinyuzi nyingi na sukari ya kawaida, ambayo inasaidia kudhibiti viwango vya
sukari kwenye damu na kupunguza hatari ya kisukari.
5. Kusaidiakupunguza uzito: Bamia ina karoli
kidogo sana.
6. Kusaidia katika umeng’enyaji wa chakula: Kwa
kuwa bamia ina nyuzinyuzi nyingi.
7. Kusaidia kuzuia upofu wa usiku: Bamia ina
kiwango kikubwa cha vitamini A ambayo ni muhimu kwa afya ya macho na inaweza
kusaidia kuzuia upofu wa usiku.
8. Kupunguza hatari ya ugonjwa wa figo: Bamia ina
potassium ambayo husaidia kudhibiti kiwango cha sodium kwenye damu na kupunguza
hatari ya ugonjwa wa figo.
9. Kusaidia katika afya ya ubongo: Bamia ina
virutubisho vinavyosaidia afya ya ubongo kama vile folate, vitamini B6 na B12,
ambavyo husaidia katika kuboresha kumbukumbu na kazi za utambuzi.
Hitimisho
Kwa kumalizia, kilimo
cha bamia nchini Tanzania kina uwezekano wa kuwa mradi wenye faida kubwa,
lakini kinahitaji mipango makini, maandalizi na utekelezaji.
Ukifuata mbinu
zilizoainishwa kwenye mwongozo huu utajiongezea nafasi ya kufaulu na kuzalisha
mazao yenye ubora wa hali ya juu yanayokidhi matakwa ya walaji.
Kumbuka kuandaa shamba
lako vizuri, kuchagua wakati sahihi wa kupanda, kutumia mbolea za kupandia na
kukuzia, kudhibiti wadudu na magonjwa, na kutumia mbinu sahihi za uvunaji.
Kwa kujitolea na
kufanya kazi kwa bidii, unaweza kuanzisha biashara ya kilimo cha bamia na
kuleta matokea chanya kwenye afya na uchumi wa jamii yako.
Hivyo basi, kunja mikono ya shati lako, vaa buti zako za shamba, uanze safari ya mafanikio ya kilimo cha bamia!







No comments