KIJUE KILIMO BORA CHA NYANYA NA DONDOO ZAKE
Dondoo muhimu za kilimo cha nyanya
Nyanya ni zao la mboga
linalolimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama
zao la biashara. Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana duniani.
Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na
kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika
kila mlo.
Kulingana na umuhimu
wa zao la nyanya kama chakula na pia kama zao linalomwingizia mkulima kipato,
kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa nyanya.
Maeneo yanayolima nyanya
Inadhaniwa kuwa asili
ya nyanya ni nchi ya Peru au Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza
kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine
za ulimwengu.
Nchi zinazolima nyanya
kwa wingi duniani ni pamoja na USA, Italia na Mexico. Kwa upande wa Africa ni;
Malawi, Zambia na Botswana. Zao hili hulimwa pia katika nchi za Africa
Mashariki, ikiwemo Kenya, uganda na Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania
mikoa inayolima nyanya kwa wingi hasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na
biashara ni pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro (Hai, Moshi na Rombo), Arusha
(Arumeru), Morogoro (Mgeta), Iringa (Ilula), Tanga (Lushoto), Mbeya (Mbeya
vijijini) na Singida.
Nyanya bora zilizoiva tayari kwa kuvunwa na matumizi
Mazingira yanayofaa kwa kilimo cha nyanya
Hali ya Hewa:
Nyanya hustawi vizuri
zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti.
Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa).
Tuna Mwongozo wa
kilimo biashara wa zao hili, kwanini usiupate ili upate maelezo mengi yenye
kina zaidi?
Kwenye mwongozo
utapata mapendekezo maalum kutoka kwetu juu ya aina bora na kiasi sahihi cha
mbegu, mbolea na viuatilifu. Pamoja na uchambuzi wa gharama za uzalishaji
katika kila hatua na faida utakayopata.
Kupata mwongozo wa zao
hili, tafadhali bofya hapa.
Udongo:
Nyanya hustawi kwenye
aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo
wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiosimamisha/tuamisha
maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 – 7.0.
Mwinuko:
Nyanya hustawi vizuri
kutoka sehemu za mwambao hadi kwenye mwinuko wa mita 400-1500 kutoka usawa wa
bahari; yaani nyanda za chini, kati hadi za juu kutoka usawa wa bahari. Nyanya
zinazopandwa nyanda za juu sana hukumbwa na mvua za mara kwa mara ambazo huambatana
na magonjwa ya jamii ya
ukungu; kama Bakajani
chelewa (Late Blight).
Mbegu bora za nyanya
Kutokana na tabia ya
ukuaji, mbegu za nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:
1. Nyanya ndefu (indeterminate) kwa mfano ANNA F1,
Tengeru 97, Marglobe (M2009). Aina hizi za nyanya hufanya vizuri zaidi
zinapopandwa ndani ya greenhouse. Uvunaji wake ni wa muda mrefu; zipo ambazo
zinavunwa hata zaidi ya miezi 6, yaani hiyo miezi 6 ni ya uvunaji.
2. Nyanya fupi (determinate) kwa mfano Tanya, Cal J,
Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa)
Kulingana na
uchavushaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:
1. Nyanya za OPV (Open Pollinated Variety) – Hizi ni aina
za kawaida
2. Nyanya Chotara – hybrid: Hizi ni nyanya zilizoboreshwa,
aina hii zina mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.
Hata hivyo katika
karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile
zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazo zaa sana, na zenye ganda gumu ili
kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika
mapema. Nyanya zinazoonyesha kuwa na sifa ya kuhifadhika bila kuharibika mapema
ni kama:
a) Tengeru’97 ambayo
ina sifa vifuatazo:
·
Huzaa sana kutokana na
wingi wa matunda na muda mrefu wa kuvuna, ambao hufikia michumo mikubwa kati ya
6-7 kuanzia kuvuna hadi mwisho wa mavuno.
·
Aina hii ina sifa ya
kuwa na ganda gumu, hivyo haziharibiki haraka wakati wa kusafirisha au
kuhifadhi (wastani wa siku 20)
·
Zina sifa ya kuvumilia
baadhi ya magonjwa kama vile ugonjwa wa kunyauka.
·
Tengeru’97 hustahimili
mashambulizi ya minyoo fundo (Root knot nematodes)
b) Tanya
·
Sifa kubwa ya Tanya ni
kwamba nayo huzaa sana
·
Huwa na ganda/ngozi
ngumu ambayo inazuia kuoza au kuharibika kwa urahisi wakati wa kusafirisha au
wakati wa kuhifadhi kwa muda mrefu.
·
Tanya nayo ina ladha
nzuri inayopendelewa na walaji wengi
Zingatia: Tatizo la Tanya na T97 ni kwamba si
kubwa sana kama marglobe 2009. Lakini ukubwa ni karibu unge karibiana,
haujapishana sana. Kwa ujumla, ukubwa na wingi wa mazao hutegemea sana matunzo,
udongo, hali ya hewa na mazingira kwa ujumla.
Maandalizi ya shamba la nyanya
Shamba la nyanya
liandaliwe mwezi mmoja au miwili kabla ya kupanda miche. Mara baada ya kulima
choma nyasi juu ya udongo au ondoa magugu yote yanayoweza kuhifadhi wadudu na magonjwa ya nyanya.
Siku moja au mbili
kabla ya kuhamishia miche ya nyanya shambani, mwagilia sehemu iliyoandaliwa kwa
ajili ya kuhamishia miche ya nyanya.
Andaa mashimo ya
nyanya kutegemeana na idadi ya miche uliyonayo, nafasi na aina ya nyanya.
Nafasi ya kupandia nyanya ni wastani wa sentimita 50 – 60 kwa 50 – 75
kutegemeana na aina au zao litakalo changanywa na nyanya.
Jinsi ya kupanda nyanya
·
Weka samadi viganja viwili
au gram 5 za mbolea ya kupandia kwenye shimo kabla ya kupanda mche.
·
Hamisha miche toka
kitaluni pamoja na udongo wake
·
Sambaza mizizi vizuri
kwenye shimo bila kukunja.
·
Fukia miche kina kile
kile ambacho shina lilikuwa limefukiwa kitaluni.
·
Mwagilia maji ya
kutosha kulingana na unyevunyevu uliopo kwenye udongo kisha weka matandazo na
kivuli ili kupunguza uharibifu unaosababishwa na mionzi ya jua.
Miche ya nyanya iliyohamishiwa shambani
Jinsi ya kutunza nyanya shambani
Umwagiliaji wa nyanya
Nyanya, kama ilivyo
kwa mazao mengine, zinahitaji maji mengi ili kuzaa matunda yenye afya.
Kutegemeana na aina ya udongo, unaweza kumwagilia nyanya mara mbili kwa wiki.
Hakikisha unapanga
ratiba maalum ya kumwagilia na unaifuata ili kuepuka kumwagilia kiholela holela
kwani umwagiliaji usio na mpangilio huathiri afya ya matunda ya nyanya na
kupelekea nyanya kuoza kitako
(tomato blossom end rot).
Unapotumia vifaa kama
water can au mpira jitahidi sana usimwagilie kwenye majani ya mmea au matunda
kwa sababu kulowesha mmea kunavutia wadudu na magonjwa ya ukungu
unaoharibu nyanya.
Zingatia: usituamishe
maji kwenye bustani au shamba la nyanya.
Palizi: Kudhibiti magugu
Hakikisha shamba ni
safi wakati wote, palilia shamba na hakikisha magugu yote hasa yale ya jamii ya
nyanya yamelimiwa chini. Palilia shamba lako wiki ya pili au ya tatu baada ya
kupandikiza miche, lakini unaweza kupalilia kila unapoona magugu kwani shamba
linatakiwa kuwa safi muda wote. Unaweza kuondoa magugu kwa kutumia dawa za kuua
magugu au jembe la mkono.
Magugu ni hatari kwa
sababu tatu:
Kwanza: magugu
yanashindana na mimea katika kuchukua nafasi na hivyo mimea kushindwa
kujitanua.
Pili: magugu huzuia
mimea ya nyanya kupata mwanga wa jua wakutosha hivyo kuifanya mimea kushindwa
kujitengenezea chakula cha kutosha.
Na tatu: magugu
hushindana na mimea ya nyanya kufyonza virutubisho/chakula ardhini kitu ambacho
kinapelekea mimea kuwa dhaifu. Pia magugu yanahifadhi wadudu na magonjwa na hivyo
kuhatarisha zaidi usalama wa nyanya.
Mahitaji ya mbolea kwenye nyanya
Mbolea za kupandia nyanya
Tumia mbolea ya DAP au
Minjingu wakati wa kupandikiza miche shambani. Kiasi cha gram 5 ambayo ni sawa
sawa na kifuniko kimoja cha soda inatosha kwa kila shimo lenye mche mmoja.
Tanguliza mbolea kwanza kwenye shimo kisha funika na udongo kiasi ili mbolea
isigusane moja kwa moja na mizizi ya nyanya.
Mbolea za kukuzia nyanya
Tumia mbolea kama vile
CAN, NPK, au SA kukuzia mimea ya nyanya. Mbolea ya kukuzia iwekwe kipindi cha
wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza nyanya shambani. Tumia kifuniko kimoja
cha soda kwa shina. Mbolea hii iwekwe kuzunguka shina la nyanya kwa umbali wa
sentimeta 5 kutoka kwenye shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara mbili kabla ya
mvuno wa kwanza.
Ili kurefusha kupindi
cha uzaaji wa zao la nyanya (na hata mazao mengine yatoayo matunda kama vile
nyanya chungu, biringanya, na pilipili hoho) inapaswa kuongezea mbolea katika kipindi cha
uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi
na mbolea kama vile NPK.
Hii inasaidia mmea
kuendelea kutoa maua bila kuchoka. Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma”
huweza kuzaa na kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu. Lakini kama utakuwa
unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya shambani (hasa usafi wa shamba na
kumwagilia maji ya kutosha), nyanya zinaweza kuendelea kuzaa kwa muda mrefu zaidi.
Hii ni tofauti na
mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo kuzaa huduma za palizi na
usafi wa shamba huachwa na kutilia maanani kazi ya kuvuna pekee. Hii
inajitokeza zaidi kwenye aina ya nyanya fupi.
Kuweka matandazo
Matandazo ni nini?
Matandazo ni nylon, majani au takataka za mimea zinazowekwa shambani au
bustanini kwa lengo la kutunza unyevu na kuzuia au kupunguza kasi ya uotaji wa
magugu, pia yakioza huongeza rutuba kwenye udongo.
Mfano wa matandazo
yanayoweza kutumika katika shamba la nyanya ni: nylon/turubai (plastic mulch),
majani makavu, majani ya migomba, pumba za mazao, takataka za mbao.
Plastic mulch inawekwa
kabla ya kupandikiza miche shambani lakini matandazo mengine yawekwe baada ya
kupandikiza miche. Na inafaa yawekwe kuzunguka eneo la shimo la mmea au katika
shamba zima. Hivyo ni vizuri matandazo ya aina hii yawekwe mara tu baada ya
kupandikiza (kama shamba halina magugu) au baada ya palizi ya kwanza.
Kupogolea matawi
Punguza matawi na
vikonyo ili kuongeza mwanga wa kutosha kwenye nyanya pamoja na kuruhusu
mzunguko wa kutosha wa upepo na kusababisha mazingira magumu ya wadudu maadui
kwenye nyanya, hasa wale wanaopenda kiza na magonjwa yanayopendelea
unyevunyevu.
Kwa nyanya fupi ni
vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda
mengi zaidi. Hivyo usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya. Kwa nyanya
ndefu zenye kuhitaji uegemezi, unashauriwa kukuza nyanya kwa tawi moja lisilo
na vichipukizi pembeni au matawi mawili na kuacha mnyanya urefuke.
Kupogolea majani
Kupunguza majani ni
muhimu pia katika kupunguza maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa
nafasi ili mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Kwa nyanya ndefu,
majani ya chini ya matunda huondolewa kadiri unavyo endelea kuvuna.
Majani yapunguzwe
kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo kisu kwani kinaweza kueneza
magonjwa kutoka mche hadi mche. Ondoa majani yote ambayo yana dalili za
magonjwa, yaliyozeeka, yaliyobadilika rangi na kuwa njano au kuanza kukauka.
Wakati wa utoaji majani kuwa makini kutojeruhi shina kwani maambukizi yanaweza
kuanzia hapo.
Kumbuka: Matawi
na majani ya chini ya mmea wowote huwa hayana msaada sana katika uzaaji wa
matunda na zaidi ni kwamba kwa kiasi kikubwa yamepoteza uwezo wake wa
kutengeneza chakula. Hivyo kuendelea kubaki kwake kutapunguza chakula ambacho
kingeenda kuongeza wingi na ukubwa wa matunda.
Kusimikia miti (staking)
Nyanya ziwekewe
miti/mambo ili kuzuia zisianguke au kutambaa kwenye udongo, jambo ambalo
linaweza kusababisha madhara mengi kwa nyanya. Nyanya zinazotambaa zinahitaji
kusaidiwa kuonyeshwa njia ili zisiguse chini.
Miti iliyosimikwa kwenye shamba la nyanya
Nyanya zinapotambaa
ardhini au kugusa chini zinaweza kuambukizwa wadudu na magonjwa ya ardhini kwa
urahisi sana na pia wakati wa jua kali nyanya huchomwa na joto kali la ardhini.
Hivyo basi shindilia
mti mmoja (pigilia chini mambo) kando ya kila mmea wa nyanya na tumia kamba
kufunga shina la mmea kwenye mti huo. Simika miti wiki mbili baada ya
kupandikiza miche. Miti iwe imara na isiyooza haraka. Iwe na urefu wa mita moja
hadi mbili na unene usiopungua sm 2.
Changamoto za kilimo cha nyanya
Kilimo cha nyanya,
kama ilivyo kwa mazao mengine ya bustani, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali
kulingana na uwezo wa mbegu kustahimili wadudu, magonjwa na hali za hewa. Kwa ujumla nyanya zinakumbwa na changamoto za wadudu na
magonjwa na kutokana na ukubwa wa matatizo haya, nimekuandalia makala zifuatazo
ili usisome kwa upana wake.
·
Magonjwa ya nyanya na
jinsi ya kuyatibu
·
Wadudu waharibifu wa zao
la nyanya na namna za kuwadhibiti
·
Ugonjwa wa nyanya kuoza
kitako
Mavuno ya nyanya kwa ekari
Mavuno ya nyanya
yanatofautiona kulingana na aina ya mbegu iliyotumika, na matunzo ya yake.
Lakini kwa ujumla mbegu chotara (hybrid) zinatoa mavuno makubwa zaidi
ukilinganisha na mbegu za kawaida (OPV).
Nyanya aina ya Assila F1 inatoa mpaka tani 25 kwa ekari, Eden F1 inatoa mpaka tani 45 kwa ekari na Anna F1 inatoa mavuno yanayofikia tani 74
(greenhouse) kwa ekari moja. (Ref)
Nyanya zilizovunwa
Uvunaji wa nyanya
Nyanya zinachukua siku
70 mpaka 90 kuwa tayari kuvuna tangu kupandikizwa. Nyanya zinatakiwa kuvunwa
zinapokuwa zimekomaa lakini bado zikiwa na rangi ya kijani. Wakati wa kuvuna
nyanya, tenganisha tunda na kikonyo chake na sio kikonyo na shina ili kuepuka
kuujeruhi mmea kitu ambacho kinaweza hurahisisha maambikizi ya magonjwa kwa
mimea.
Wakati mzuri wa kuvuna
ni asubuhi na jioni. Inatakiwa nyanya ziwekwe kwenye vyombo vinavyopitisha
hewa, na vyombo maarufu ni matenga. Matenga ya nyanya yanaweza kuwa
yametengenezwa kwa mbao au mianzi. Mara tu baada ya kuvuna/kuchuma nyanya
inashauriwa zikusanywe chini ya kivuli kwa muda ili ziweze kutoa joto la
shambani kabla ya kuzifungasha kwenye matenga.







No comments