JIFUNZE KILIMO BORA CHA MAPAPAI
PAPAI ni tunda lenye ladha nzuri, na rahisi kuliwa. Aina hii ya tunda ni
chanzo cha virutubisho muhimu mwilini, ambavyo husaidia kujenga mwili.
Zao hili asili yake ni ukanda wa kitropiki ambao hauna baridi kali na joto
kiasi.
Udongo
pawpaw 2Mipapai hustawi vizuri kwenye udongo usiotuhamisha maji. Endapo
maji yakituama kwenye eneo lililopandwa mipapai kwa muda wa siku mbili, mpapai
unaweza kuoza kwa haraka na kufa. Kwa kuwa mipapai haina mzizi mkuu, inahitaji
udongo wenye rutuba ya kutosha. Halikadhalika, zao hili halihitaji udongo wenye
kina kirefu, hivyo ni muhimu kumwagilia mipapai wakati wa kiangazi. Wakati wa
mapapai kuiva kama kuna ukame basi hali hiyo huongeza ubora wa papai ikiwamo
kutooza mapema baada ya kuvunwa.
Kupanda
Mipapai ipandwe sehemu ambazo hazina upepo mkali. Hii itasaidia mipapai
kukua vizuri bila kuvunjika kwani mti wa mpapai huvunjika kirahisi. Inashauriwa
kupanda miti ya kukinga upepo kuzunguka shamba la mipapai. Ili kuwa na tija
zaidi, unaweza kupanda aina nyingine ya miti ya matunda kama vile miparachichi,
na miembe.
Hakikisha miti ya kukinga upepo inakuwa mirefu kuzidi mipapai. Miti hiyo
inaweza kutangulia kupandwa miezi kadhaa kabla ya kupanda mipapai.
Mbegu
Kusanya mbegu toka kwenye mapapai makubwa na yaliyo komaa na kuiva, kisha
kausha mbegu vizuri kabla ya kupanda. Inashauriwa kununua mbegu kutoka kwa
wazalishaji wanaoaminika na waliothibitishwa, ili kuwa na mazao bora zaidi na
yanayoweza kukabiliana na magonjwa.
Mbegu aina ya red royal F1, inasifika zaidi kwa kuwa na uwezo mkubwa wa
kukabiliana na magonjwa yanayoshambulia mipapai, na huanza kuvunwa mapema
zaidi, kati ya miezi 6 hadi 12. Aina hii huvunwa mfululizo kwa miaka 5 hadi 7.
Uandaaji wa shamba
Inashauriwa kuandaa shamba vizuri kwa kuondoa visiki na magugu yote. Shamba
lilimwe vizuri, na kuhakikisha udongo umelainika vizuri.
Mashimo
• Chimba shimo kwa ajili ya kupanda mpapai, liwe na kina cha sentimita 60
na upana wa sentimita 60.
• Weka mboji debe moja kisha changanya na nusu ya udongo uliotoa kwenye
shimo, kisha rudishia kwenye shimo.
• Mwagilia maji kwa kipindi cha wiki mbili kabla ya kuotesha.
Kuotesha
Sia miche kwenye kitalu, kasha hamishia shambani inapokuwa na urefu wa
sentimita 30. Chomeka mche kwenye ardhi kina cha kati ya sentimeta 1 – 2 chini
ya udongo kwenye shimo uliloandaa. Hii itasaidia mche kupata joto la wastani na
kuepuka mche kuoza na kufa. Baadhi ya wakulima hupenda kuotesha mipapai moja
kwa moja shambani.
Endapo unapenda kufanya hivyo, zingatia haya;
• Kabla ya kupanda mbegu weka mchanganyiko wa majivu na mbolea ya kuku au
mboji sehemu unayokusudia kupanda. Mbolea husaidia ukuaji haraka na jivu
husaidia kukinga mipapai na magonjwa.
• Panda mbegu 3 – 4 kila shimo, hii ni kwa sababu miche mingine inaweza
kufa kutokana na magonjwa, kuliwa na wadudu au ikaota mipapai dume.
Nafasi
Shimo hadi shimo, liwe na nafasi ya mita 3, na mstari hadi mstari mita 3.
Hii itasaidia miche ya mipapai kukua vizuri bila kusongamana.
Punguza miche
Baada ya miezi 3 – 5 tangu kupanda, mipapai itaanza kutoa maua na hapo
jinsia ya mipapai itajulikana. Inapofikia wakati huo inabidi kupunguza mipapai
mingine hasa midume.
Mipapai yenye jinsi zote isizidi asilimia 10 – 20 ya miche yote iliyopo
shambani, na midume ibaki mmoja katika kila majike 25.
Utunzaji
• Weka kilo 2 – 5 za samadi kwenye kila mpapai kwa mwaka ili kuongeza
ukuaji na uzalishaji.
• Mabaki ya mimea yanaweza kuwekwa kama matandazo. Hii ni muhimu zaidi
kipindi cha kiangazi ili kuzuia unyevu usipotee.
• Chunguza mipapai mara kwa mara ili kuangalia kama kuna magonjwa,
ing’olewe na kuchomwa au kufukiwa chini endapo itabainika kuwa na maonjwa.
• Unaweza kunyunyiza dawa zisizo na madhara za kukinga au kukabiliana na
magonjwa ya ukungu na virusi.
Kupogoa
• Kata matawi yote yatakayojitokeza pembeni ya mpapai. Hili lifanyike
mapema kabla ya tawi kuwa kubwa.
• Ondoa mipapi yote ambayo hayakuchavushwa vizuri na ubakize yenye afya tu.
Palizi
• Mipapai inapopandwa tu inaweza kuwekewa matandazo kuizunguka ili kuzuia
uoataji wa magugu.
• Magugu yang’olewe yakiwa machanga.
• Epuka kuchimbua sana wakati wa palizi kwa kuwa mizizi ya mipapai huwa juu
juu.
Magonjwa
Zao la papai halina magonjwa mengi sana yanayoshambulia endapo litatunzwa
vizuri. Hata hivyo kuna baadhi ya magonjwa ambayo yamezoeleka kwenye zao hili
kama vile Ugonjwa wa madoa kwenye majani (Papaya spot) na Ugonjwa wa virusi
unaojulikana kama Mozaic virus. Mimea yenye magonjwa inaweza kung’olewa na
kufukiwa ili kudhibiti ueneaji kwenye mimea mingine.
Taarifa hii ni kwa hisani ya Blog ttps://mjasiriamaliapp.blogspot.com/.
No comments