Header Ads

DC CHIRUKILE : PEMBEJEO ZISAMBAZWE MAPEMA KUONGEZA TIJA KATIKA MAZAO YA WAKULIMA

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile akizungumza na wananchi wa wa Mji Mdogo wa Laela waliojitokeza katika uzinduzi wa msimu wa kilimo 2025, Disemba 30, 2024.
..........................................

Na Neema Mtuka, Rukwa

MKUU wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia  Chirukile amefungua msimu wa kilimo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na kuwataka wananchi kupanda miti ya parachichi kwa lengo la kuimarisha afya zao. 

Hafla hiyo iliyofanyika leo Desemba 30/2024 katika Mji mdogo wa Laela na kuhudhuriwa na Wakulima, viongozi wa Chama na Serikali Kampuni za pembejeo za kilimo, Wadau na Wananchi. 

Akizungumza katika hafla hiyo Chirukile amesema ili wakulima waongeze tija kwenye mazao yao wasambazaji wa mbolea waziwaishe ili mkulima apandie na kukuzia kwa wakati. 

“Serikali imekuwa ikitoa pesa nyingi kwa lengo la kuimarisha na kuboresha sekta ya kilimo ili kumuongezea mkulima thamani katika mazao na kuleta tija sasa akikisheni mnasambaza mbolea kwa uaminifu na kuacha ujanja ujanja kwani mnawarudisha nyuma wakulima.” alisisitiza Chirukile. 

Pia amewataka Mawakala na wasambazaji wa pembejeo kusambaza mbegu bora za mpunga ili kuongeza thamani ya zao hilo. 

Amesema hali ya uzalishaji imeongezeka kutoka asilimia 60 hadi 75 ambapo wilaya hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa. 

Aidha amewataka wawekezaji kuja kuwekeza kwa kujenga viwanda vikubwa vya kukoboa mpunga na kuuongezea thamani mchele unaotoka katika ukanda huo. 

“Inashangaza kuona mchele unatoka hapa Rukwa unaenda Shinyanga na kuongezewa thamani na unauzwa kama mchele unaotoka huko ili hali sisi ndio tunalima mpunga.”alisema Chirukile. 

Katika hatua nyingine Chirukile amezindua kampeni ya upandaji miche 2000 ya miti ya parachichi na kukabidhi kwa wananchi na wadau mbalimbali huku akieleza kuwa miti ya matunda inafaida kubwa kwa afya ya binadamu na utunzaji wa mazingira na lengo hasa ni kuhamasisha nishati safi ya kupikia. 

" Kupanda miti ya matunda ni muhimu na wajibu wa kila mmoja ili kutunza mazingira na kuimarisha afya na lishe na kuondokana na changamoto ya udumavu," alisema Chirukile. 

Sambamba na hilo Chirukile amewataka wataalamu wa kilimo kuwasaidia wakulima kupima udongo ili kujua aina za mbegu wanazotakiwa kupanda kulingana na ukanda wao. 

Amesema kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa mvua ya msimu huu itakuwa juu ya wastani hadi chini ya wastani hivyo wakulima wapande mbegu zinazostahimili ukame na mabadiliko ya tabia ya nchi huku akiwataka wataalamu kuwasaidia wakulima ili kuondokana na changamoto hasi za hali ya hewa na mpaka kufikia mwaka 2030 kilimo kichangie pato la taifa kwa asilimia 100. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga,  Kalolo Ntilla amewataka wananchi wa ukanda huo kuachana na mila potofu pindi wataalamu wanapoenda kupima udongo. 

“ Baadhi ya wakulima wamekuwa na imani potovu kuwa mtaalamu akichukua udongo kwa ajili ya kwenda kuupima wao wanadai  anaenda kufanya mambo mabaya ya ushirikina jambo ambalo sio la kweli, ” alisema Ntilla.

Wakulima walioshiriki katika hafla hiyo akiwemo Steveni Kusaya na Ombeni Wangao wamesema kuwa ili kukifikia kilimo cha kisasa na chenye tija ni lazima maafisa kilimo waache kukaa ofisini badala yake waende kwa wakulima kushirikiana nao. 

Wakulima hao wamesema moja ya changamoto kubwa ni ukosefu wa pembejeo za kilimo na ushiriki hafifu wa wataalamu wa kilimo ambao muda mwingi wanautumia kukaa maofisini. 

“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mpango wa mbolea na mbegu za ruzuku ambao unasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao hali inayopelekea kuongezeka kwa kipato kwa mwananchi mmoja mmoja kuanzia ngazi ya kaya na taifa kwa ujumla na kukuza uchumi wa nchi,”. alisema Ombeni Wangao. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Kalolo Ntilla akizungumza na wakazi wa Mji Mdogo wa Laela wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo 2025.

Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye uzinduzi wa msimu huo wa kilimoWafanyabiashara wakionesha bidhaa za kilimo na pembejeo wakati wa uzinduzi huo.Picha ya pamoja baada ya uzinduzi huo wa msimu wa kilimo. 

No comments

Powered by Blogger.