Header Ads

TMA YATOA USHAURI KWA WAKULIMA, WAFUGAJI WAKATI WA MVUA ZA MASIKA

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang'a ,akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka wakati akizungumza na waandishi wa habari.jijini Dar es Salaam, Januari 23, 2025.

......................................................................

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa ushauri kwa wakulima na wafugaji ili kukabiliana na matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa yatakayoweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.

Ushauri huo umetolewa Januari 23, 2025 jijini, Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika zitakazoanza Machi hadi Mei 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka kwa waandishi wa habari.                                            

Akizungumzia kuhusu ushauri wakati wa kipindi hicho kwenye sekta ya Kilimo na Usalama wa Chakula alisema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani. Vilevile, wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea yanayoendana na hali ya ongezeko la unyevu kama vile ukungu yanatarajiwa kuongezeka na kuathiri mazao kama ndizi, mahindi,mpunga, mihogo na maharage. Hata hivyo hali ya upungufu wa unyevu inaweza kujitokeza hasa katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.

Alisema Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, kuhifadhi maji shambani, kuzuia mmomonyoko na upotevu wa rutuba kutokana na kutuwamisha maji kwa muda mrefu au mafuriko. Aidha, inashauriwa kuimarisha miundombinu ya kilimo na kudhibiti kwa wakati magonjwa ya mimea na wadudu waharibifu ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

“ Wakulima wanashauriwa kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa msimu wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi. Aidha, wakulima na maafisa ugani wanashauriwa kuendelea kutumia utabiri wa siku na siku kumi ili kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa utabiri wa msimu, “ alisema Chang’a.

Dkt. Shang’a akizungumzia kuhusu Mifugo na Uvuvi alisema hali hiyo inaweza kupelekea athari katika ukuaji wa mazao ya kilimo hivyo kama hali hiyo itajitokeza inapaswa kutolewa taarifa haraka kwa vyombo vinavyohusika

Alisema katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani, wafugaji nawavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki. Hata hivyo, milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na midomo, na kuzaliana kwa wadudu wadhurifu kunaweza kujitokeza.

Aliongeza kuwa upungufu wa maji unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani na hivyo unaweza kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo na kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Alisema Wafugaji wanashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo. Aidha, wafugaji na wavuvi wanashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri unaotolewa na maofisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza na kuendelea kunufaika na hali ya hewa inayotarajiwa wakati wa msimu.

No comments

Powered by Blogger.