WORLD VISION TANZANIA YAGAWA MICHE YA MATUNDA KWA SHULE ZA MSINGI SHINYANGA
Matukio mbalimbali katika picha yakimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mjini, Wakili Julius Mtatiro alipokuwa akigawa miche ya miti ya matunda na mbegu za mbogamboga kwa shule za msingi katika kata za Pandagichiza, Iselamagazi, na Itwangi, wilayani Shinyanga Januari 16, 2025.
......................................
Na Mwandishi Wetu - Shinyanga
Shirika la World Vision Tanzania, kupitia mradi wake wa Grow-ENRICH,
limekabidhi miche ya miti ya matunda na mbegu za mbogamboga kwa shule za msingi
katika kata za Pandagichiza, Iselamagazi, na Itwangi, wilayani Shinyanga, kwa
lengo la kuboresha lishe ya watoto na kuchangia juhudi za utunzaji wa
mazingira.
Hafla ya makabidhiano imefanyika leo, Januari 16, 2025, ambapo Shukrani
Dickson, Meneja wa Mradi wa Grow-ENRICH, amekabidhi miche ya mipera 520,
mipapai 470, na pakiti 195 za mbegu za mbogamboga kwa Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro.
Wakili Mtatiro pia amekabidhi miche hiyo kwa maafisa wa kilimo na elimu wa
wilaya, pamoja na wataalamu wa kata za Pandagichiza, Iselamagazi na Itwangi.
Shukrani ameeleza kuwa miche ya matunda ya mipera na mipapai inagawiwa kwa
shule zilizoshiriki katika mradi wa awali na kuonyesha uhitaji mkubwa wa
kuongezewa miche.
Aidha, mbegu za mbogamboga kama sukumawiki, spinach, na Chinese cabbage
zitatumika kuboresha lishe ya watoto na jamii kwa ujumla.
"World Vision Tanzania tunahamasisha kilimo cha mboga za majani na
matunda ili kuboresha afya za watoto shuleni na kupunguza utapiamlo,"
amesema Shukrani.
“Mradi wa Grow-ENRICH unaotekelezwa katika halmashauri za Shinyanga na
Kishapu umeweza kununua jumla ya miche 1,215 ya matunda, ikiwa ni mipera 665 na
mipapai 550, kwa shule za msingi. Hii ni hatua ya pili ya ugawaji wa miche
baada ya miche ya awali kugawiwa kwa shule za kata sita, pamoja na mbegu 2,350
za mbogamboga,” amesema Shukrani.
Amefafanua kuwa shule zilizoshiriki katika mradi na kuonyesha uhitaji wa
miche zaidi, hasa zile zenye vyanzo vya maji vya kudumu, zitapata miche hii ili
kuendeleza shughuli za kilimo cha matunda na mbogamboga, kwa lengo la kuboresha
lishe ya watoto.
“Mradi wa Grow-ENRICH unalenga kuboresha afya na lishe ya watoto, akina
mama wanaonyonyesha, na jamii kwa ujumla. Shukrani amesema kuwa kupitia miche
ya matunda na mbegu za mbogamboga, World Vision Tanzania inaunga mkono juhudi
za serikali katika kutokomeza utapiamlo na kuhakikisha upatikanaji wa chakula
cha lishe kwa watoto na familia zao”,ameongeza Shukrani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro,
amelishukuru shirika la World Vision Tanzania kwa msaada wake mkubwa katika
kuboresha lishe na afya ya watoto akisema hatua hii inatekeleza Ilani ya Chama
Cha Mapinduzi na sera za serikali kuhusu lishe.
“Mbegu hizi za mbogamboga na miche ya matunda zitasaidia sana jamii yetu.
Tunashukuru kwa msaada huu ambao unalingana na agenda ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupambana na utapiamlo
na kuboresha afya ya wananchi,” amesema Wakili Mtatiro.
Aidha, amehimiza wananchi na wadau wa kilimo kutumia kwa wingi mboga za
majani na matunda katika kila mlo ili kuboresha afya zao na za watoto wao.
“Watumishi, hakikisheni mnasimamia kwa karibu miche hii ili iweze kutoa
matunda na kuboresha lishe katika jamii. Nitahitaji ripoti ya maendeleo ya miti
na bustani za mbogamboga ndani ya siku 90,” ameongeza Wakili Mtatiro.
Pia, Wakili Mtatiro amewaasa wafanyakazi wa serikali na wa shirika la World
Vision Tanzania kuzingatia ulaji bora na kupima afya zao kwa manufaa yao
wenyewe, akisisitiza kuwa ulaji bora utasaidia kuboresha afya za jamii nzima na
kuwezesha taifa kuwa na nguvu kazi yenye afya.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya miche ya miti ya matunda na mbegu za mbogamboga kwa shule za msingi katika kata za Pandagichiza, Iselamagazi, na Itwangi, wilayani Shinyanga
Meneja wa Mradi wa Grow-ENRICH, Shukrani Dickson (kulia) akikabidhi miche ya miti ya matunda kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro (kushoto) akikabidhi miche ya miti ya matunda kwa maafisa wa kilimo na elimu wa wilaya, pamoja na wataalamu wa kata za Pandagichiza, Iselamagazi na Itwangi.






No comments