MKOA WA SINGIDA WAVUNA ZAIDI YA TANI 334.9 ZA MAZAO YA NYUKI
Muonekano wa nyuki wakiwa kwenye masega yao
.......................................
Na Jumbe Ismailly Singida
MKOA wa Singida umevuna tani 334.99 za mazao ya nyuki zikiwemo tani 296.4 za
asali na tani 38.95 za nta katika cha kipindi cha kuanzia mwaka 2024 na 2025
huku Mkoa huo unakadiriwa kuwa na mizinga ya kienyeji ipatayo 151,022 na
mizinga ya kisasa 12,076.
Akitoa taarifa za ufugaji nyuki katika Mkoa wa Singida, Afisa maliasili wa Mkoa wa Singida, Charles Kidua amesema sekta hiyo imejikita katika kukuza uchumi kwa kuimarisha na kuongeza upatikanaji wa mazao ya nyuki ikiwemo asali pamoja na nta.
Kuhusu mazingira na mabadiliko ya taibianchi,Bwana Kidua ameweka bayana kwamba Mkoa wa Singida kama ilivyo mikoa mingine haujaachwa katika kupata madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Afisa maliasili huyo Mkoa umekumbwa na ongezeko la joto pamoja na mtawanyiko mbaya wa mvua,hali inayopelekea kupata upungufu wa chakula na magonjwa yatokanayo na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi yakiwemo magonjwa ya mtoto wa jicho na mengine mengi.
Hata hivyo afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya
maliasili amebainisha kuwa Mkoa huo umejaaliwa kuwa na madini ya aina mbali
mbali yakiwemo dhahabu,chumvi,shaba,jasi,madini ya ujenzi na vito
vikiwemo quarts na Amethysts.
Akizungumzia sekta ndogo ya wanyamapori amesema Mkoa una mapori
ambayo ni makazi mazuri ya wanyamapori na mapori hayo yamegawanyika katika
sehemu kuu mbili,ambayo ni mapori ya akiba yanayomilikiwa na serikali kuu na
mapori ya hifadhi ya ardhi za vijiji.
Hata hivyo Bwana Kidua ameyataja mapori hayo kuwa ni pamoja na
Rungwa,Muhesi na Kizigo yaliyopo katika wilaya ya Manyoni ambayo yana idadi
kubwa ya tembo ukilinganisha na mapori mengine ndani ya nchi na yanatumika kwa
uwindaji wa kitalii,yakiwa na vitalu vya uwindaji ndani yake.



No comments