NFRA YAJIVUNIA MAFANIKIO YA UTENDAJI MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA
............................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
WAKALA wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula nchini
(NFRA) umesema kuwa unajivunia mafanikio uliyoyapata katika kipindi cha miaka
minne ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza uwezo wa uhifadhi
wa chakula cha akiba na ziada kuuza nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Andrew Komba
amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, taasisi hiyo
imefanikiwa katika maeneo mbalimbali ya utendaji, ikiwemo kuongeza uwezo wa
uhifadhi wa chakula cha akiba na kuuza takribani tani 600,000 za
mazao katika masoko ya kimataifa .
“Katika miaka ya nyuma, NFRA ilikuwa na uwezo
wa kuuza kati ya tani 50,000-60,000 katika masoko ya kimataifa,”
“Lakini baada ya Serikali ya Rais Dkt Samia
kutuwezesha, uhifadhi wa akiba ya chakula hapa nchini ili kukabiliana na
upungufu utakapojitokeza umeongezeka,”
“Lakini pia tumeweza kuuza nje ya nchi chakula
cha ziada na hii imesaidia kuinua maisha ya wakulima wetu na nchi kupata faida
kutokana na mauzo hayo ya nafaka ya nje ya nchi,” amesema Dkt Komba.
Dkt. Komba amesema kuwa katika kipindi
cha mwaka wa fedha 2023/2024 NFRA ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi shehena ya
takribani tani 351,000, lakini hadi kufikia sasa, uwezo wa taasisi hiyo
umeongezeka hadi kufikia kuhifadhi tarkiban tani 776,000.
Pia amesema kuwa kupitia mauzo ya nafaka, NFRA
imekusanya takribani bilioni 540 ya mauzo ambapo fedha hizo zimekuwa zikitumika
katika kupanua maeneo mbalimbali ya utendaji, ikiwemo ukarabati wa miundombinu
na maghala.
“Mafanikio haya yanatokana na mizunguko ambayo
Rais Samia amekuwa akiifanya katika nchi tofauti tofauti , akitumia nafasi hiyo
kuinadi NFRA na kusaidia kupata masoko ya uhakika kwa nchi zenye uhitaji
wa chakula,” amesema Dkt Komba.
Ameongeza kuwa kupitia Wizara ya Kilimo,
Serikali imeiwezesha taasisi hiyo kuwa na maghala yenye uwezo wa kutunza jumla
ya tani 48,000.
“Rais Samia akiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani Ruvuma mwaka jana alitukabidhi jumla ya maghala 28 yenye uwezo wa
kuhifadhi takribani tani 28,000,”
“Hivyo serikali kupitia wizara,
imetusaidia ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani takribani 76,000
za chakula” alisema Dkt Komba.
Katika kutanua wigo wa utendaji, NFRA Katika
kipindi cha mwaka wa fedha uliopita ilifanikiwa kuzindua maghala mengine mawili
ambayo yalijengwa katika mikoa ya Katavi na Sumbawanga ili kuongeza uwezo wa
maeneo ya uhifadhi wa akiba ya chakula.
“Ili kuhakikisha nchi inakuwa na hifadhi ya
chakula cha kutosha, Rais Dkt Samia aliiwekea NFRA malengo ya kuwa na uwezo wa
kuhifadhi tani 3,000,000 ifikapo mwaka 2030,”
“Hivyo, Rais Samia , Waziri wa Wizara ya
Kilimo Hussein Bashe pamoja na viongozi wengine wamekuwa mstari wa mbele katika
kuhakikisha NFRA inafikia malengo haya ” alisema Dkt Komba
Amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi
Novemba mwaka 2024, NFRA imeweza kununua tani 479,000 kutoka kwa wakulima na
manunuzi haya hayajawahi kufanyika katika taasisi hiyo katika miaka ya nyuma.
NFRA ina jumla ya tani 776,000 katika maghala
yake ambapo kati ya hizo tani 400,000 zitauzwa katika masoko ya ndani na nje
na tani 300,000 zitabakishwa katika maghala kwa ajili ya kulinda usalama wa
chakula nchini.
Endapo uzalishaji wa chakula kutoka kwa
wakulima utapungua, Dkt Komba amesema NFRA itakuwa na uwezo wa kuilisha
nchi kwa mwaka mzima.
“Kwa sasa NFRA inashehena yakutosha ambayo
itaiwezesha nchi kufanya biashara ya kuuza mazao katika masoko ya ndani na nje
pia itaendelea kuwa na shehena ambayo itasaidia kulisha nchi endapo
majanga ya njaa au maafa yatatokea”.alisema Dkt Komba.



No comments