Header Ads

RAIS SAMIA KUZINDUA KIWANDA CHA MBOLEA ITRACOM


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi kiwanda cha mbolea kiitwacho ITRACOM Fertilizers Limited kilichopo Nala, jijini Dodoma, tarehe 28 Juni 2025.

Amesema hayo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo wakati wa Mkutano wake na Wanahabari uliofanyika tarehe 11 Juni 2025 katika Ukumbi wa Wizara ya Kilimo, jijini Dodoma.

Amesema ITRACOM Fertilizers Limited ni kiwanda cha pili kuzalisha mbolea nchini; na cha kwanza kwa ukubwa kuliko viwanda vyote vya uzalishaji mbolea katika Afrika Mashariki chenye uwekezaji wa Dola za Marekani Milioni 180.   ITRACOM ina uwezo wa kuzalisha tani 1,000,000 ya mbolea kwa kutumia teknolojia inayozalisha mbolea za FOMI ambazo zina mchanganyiko wa virutubisho vya asili na vya chumvichumvi kitaalamu iitwayo “organo-mineral fertilizer”.  Kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi na mpaka sasa kimezalisha ajira 1,805.

Aidha, Waziri Bashe amesema kuwa ili kulinda viwanda vya ndani ya Tanzania, Serikali imepanga kununua mbolea tani 200,000 na tani 50,000 zitanunuliwa za chokaa kilimo kwa ajili ya shughuli za kilimo na kusambazwa kwa wakulima ambao hawatumii mbolea kwa msimu ujao wa kilimo kwa lengo la kuongeza matumizi ya mbolea za viwandani zinazozalishwa ndani ya nchi na kuvifungulia viwanda hivyo masoko ya ndani na nje ya nchi.

Uzinduzi wa kiwanda cha ITRACOM Fertilizers Limited unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi mbalimbali akiwemo Mheshimiwa Rais wa Burundi na Mawaziri wa Kilimo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani “East African Community (EAC)” na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika yaani “Southern African Development Community (SADC)”.

No comments

Powered by Blogger.