Header Ads

RAIS SAMIA: YAJAYO YANAFURAHISHA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehutubia wananchi wa Mkoa wa Simiyu katika viwanja vya stendi ya zamani, wilayani Bariadi tarehe 18 Juni 2025 na kupongeza miradi ya maendeleo huku akiwatia moyo kuwa yajayo yanafurahisha.  

“Ni lazima maendeleo yetu tujidhatiti wenyewe.  Kwenye Serikali tumejipanga vema kujenga nchi, kutoa huduma kwa wananchi na kuleta uchumi wenye amani na utulivu,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia. 

Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa katika ziara ya siku nne Mkoani Simiyu ambapo pia amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo vikiwemo viwanda vingine vya kuchakata Pamba vya Moli Oil Mills Ltd. katika wilaya ya Bariadi; na BioSustain Tanzania Limited katika Wilaya ya Meatu.

Awali, Mhe. Raia Dkt. Samia amezindua kiwanda cha kuchakata Pamba cha Shree Rajendra Agro Industry Limited kilichopo Wilaya ya Maswa.

Kiwanda hicho kimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 12.4 ambacho kina uwezo wa kuchakata kilogram 350,000 za pamba mbegu sawa na tani 350 kwa siku.

Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia pia amezungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Maswa katika uwanja wa Chama cha Mapinduzi, amesema kuwa ziara hiyo imekuwa na mafanikio ambapo amezindua shughuli mbalimbali za maendeleo, hususan viwanda vya kuchambua Pamba.  “Tuendelee kulima kwa wingi, soko lipo na viwanda vipo ambapo leo nimezindua kiwanda cha Shree Rajendra Agro Industry Limited,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Ziara hiyo imehusisha viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo na inahitimishwa tarehe 19 Juni 2025 katika Mkoa wa Simiyu ambapo miradi ya kimkakati ya maji itazinduliwa ili kuondoa tatizo la maji kwa wananchi wa Mkoa huo.

No comments

Powered by Blogger.