ZIARA YA WAJUMBE WA KAMATI YA USIMAMIZI PSC NA PTC
Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi (Project Steering Committee-PSC) na Kamati ya Kitaalam (Project Technical Committee-PTC) ya Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Inputs Support Project- TAISP), wamefanya ziara ya kutembelea maeneo yanayotekelezwa na Mradi huo tarehe 23 Juni 2025.
Katika ziara hiyo wajumbe hao wametembelea Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Makao Makuu na mashamba ya Mbegu ya kilangali na Msimba yaliyopo katika Mkoa wa Morogoro ambapo wamepokea taarifa kuwa Mradi wa TAISP umeiwezesha ASA kununua malori matatu (3) ya kusambaza mbegu yenye uwezo wa kubeba tani 10 za mbegu kwa kila moja, Pikipiki tatu (3) zimenunuliwa kwa ajili ya maafisa ugani , mitambo miwili ya kuchakata mbegu (Processing Plant) ambayo itasimikwa katika mashamba ya mbegu ya Mbozi (Songwe) na Namtumbo Ruvuma.
Katika hatua nyingine,TAISP imenunua Mtambo wa kuvunia mbegu (Combine harvester) na Mtambo wa kukaushia mbegu (Seed dryer) katika shamba la mbegu la Kilangali. Pia TAISP imewezesha uzalishaji wa mbegu za daraja la msingi za zao la Alizeti katika eneo lenye hekta 120 katika shamba la Msimba.
Kadhalika, TAISP inaweka miundombinu ya umwagiliaji katika Hekta 100 kwa ajili ya uzaishaji wa mbegu. Mitambo hiyo itachangia kupunguza gharama za uzalishaji wa mbegu kupitia ASA na hivyo kuchochea upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima nchini.
Mradi wa TAISP unatekelezwa katika Halmashauri 56 za Mikoa 14 ya Tanzania Bara katika mazao makuu matatu (3): Alizeti, Ngano na Mpunga. TAISP inatekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI); Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI); Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA); na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
No comments