URUSI NA TANZANIA WAJADILIANA MASHIRIKIANO SEKTA YA KILIMO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amefanya majadiliano ya uwili (bilateral consultation) kwa njia ya mtandao na Manaibu Waziri wa Kilimo wa Shirikisho la Urusi, Mhe. Markovich Maxim pamoja na Mhe. Afonina Marina tarehe 24 Juni 2025, kuhusu kushirikiana katika Sekta ya Kilimo.
Majadiliano hayo yamelenga ushirikiano katika nyanja ya biashara za bidhaa za kilimo, uingizwaji wa bidhaa za kilimo za Urusi katika soko la Tanzania, usambazaji wa mbolea pamoja na ushirikiano wa kisayansi na teknolojia katika Sekta ya Kilimo.
Katibu Mkuu Mweli ameainisha maeneo ambayo Tanzania inahitaji kushirikiana na Urusi kuwa ni masuala ya tafiti na uhaulishaji wa teknolojia; mafunzo, zana za kilimo; uongezaji thamani; uzalishaji mbegu ikiwemo OPV na chotara; uzalishaji wa mbolea; mazao ya mafuta; pamoja na ngano.
Majadiliano hayo yanatokana na ushiriki wa Wizara ya Kilimo katika mikutano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi katika uchumi na biashara, ukiwemo mkutano wa tarehe 28 -29 Oktoba 2024 uliofanyika jijini Dar es Salaam; na mkutano wa pili uliofanyika tarehe 12-13 Mei 2025, jijini St. Petersburg, nchini Urusi.
Washiriki wengine katika majadiliano hayo ni Bw. Thomas Bwana, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Bi. Irene Mlola, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bw. Samuel Mshote, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Dkt. Japhet Mkangaga. Mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; pamoja na Wakurugenzi kutoka Wizara ya Kilimo. Majadiliano hayo yaehitimishwa kwa ahadi za kutoa ushirikiano wenye tija na maendeleo kwa pande zote.
No comments