MAELEKEZO KWA TUME YA UMWAGILIAJI
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepokea maelekezo ya utekelezaji ya Miradi ya Umwagiliaji kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo (anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo) Mhandisi Athumani Juma Kilundumya kuhusu Tume kuhakikisha inasimamia wahandisi na watendaji katika kutekeleza miradi kwa kuzingatia weledi, sheria, miongozo na uzalendo ili kuleta tija.
Naibu Katibu Kilundumya amesema hayo tarehe 9 Julai 2025 wakati wa kikao cha kumkaribisha katika ofisi za Tume Makao Makuu, jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa anatarajia kufanya mkutano na wasimamizi wa miradi ya Umwagiliaji nchi nzima, ambao ni wahandisi wa umwagiliaji wa Mikoa, kwa lengo la kubadilishana uzoefu kupata taswira halisi ya utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
“Ninatazamia kukutana na mameneja wa miradi ya umwagiliaji ili pia kujadili fursa zilizopo ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji,” amesisitiza Naibu Katibu Mkuu Kilundumya.
Naye Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa amesema Tume inaendelea vema na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji kwa kadiri ya upatijanaji wa rasilimali fedha. “Mchakato wa uchimbaji wa visima kwa ajili ya umwagiliaji umeanza na lengo ni kuhakikisha uchimbaji wa visima katika miradi ya Vijana wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) Mkoani Dodoma, ambapo inakamilika kabla ya kuendelea na Mikoa mingine”, ameongeza Mkurugenzi Mkuu Mndolwa.
Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Athumani Juma Kilundumya, aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 23 Juni 2025.
No comments