Header Ads

WAKULIMA 350 WILAYA YA MERU ARUSHA WANUFAIKA NA MAFUNZO YA KILIMO CHA ALIZETI


 Wizara ya Kilimo, kupitia Mradi wa Kuwezesha Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Inputs Support Project-TAISP) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru imefanya maadhimisho ya Siku ya wakulima katika Shamba darasa la Alizeti lililoanzishwa na Mradi wa TAISP katika Kijiji cha Olkung’wando kata ya Ngarenanyuki Mkoa wa Arusha tarehe 8 Julai 2025.

Maadhimisho hayo yamewakutanisha wakulima zaidi ya 350, Maafisa ugani 10 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meru na Viongozi wa Vijiji kutoka Kata ya Ngarenanyuki.

Mratibu wa Mradi wa TAISP, Bi. Kissa Chawe amewashauri wakulima hao kuzingatia elimu waliojifunza na kuitumia katika mashamba yao katika msimu wa kilimo wa 2025/2026.  Amewahamasisha wakulima kujitokeza kushiriki katika mafunzo yanayotolewa na wataalam wa kilimo ikiwemo mashamba darasa ili waweze kujifunza kwa vitendo juu ya kanuni bora za mazao ya kilimo, hususan zao la Alizeti. 

Pia, amewataka wakulima hao wawe walimu wazuri kwa wakulima wengine ambao bado hawajapata elimu hiyo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa zao Alizeti na hatimae nchi kujitosheleza kwa mafuta ya kulima.

Naye Afisa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Michael Lufungulo ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea na zoezi la upimaji wa afya ya udongo ili kujua hali ya rutuba ya udongo na kutoa ushauri sahihi juu ya matumizi ya udongo, kiwango na aina sahihi ya mbolea inayofaa kutumika na aina ya mazao yanayofaa kulimwa katika eneo husika kwa kuzingatia aina na kina cha udongo. 

Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Aminika, Bw. Jafason Stephano Nkoo amesema mbegu aina ya hysun 33 waliowezeshwa ni mbegu bora ukilinganisha na mbegu walizowahi kutumia hapo awali kwani wanatarajia kuvuna zaidi magunia 10 kwa ekari tofauti na mwanzo.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa kikundi cha Aminika, Bi. Happy Saanya ameeleza kuwa kupitia shamba darasa la Alizeti, wamewezeshwa kujifunza mbinu bora za kilimo cha zao la Alizeti ikiwemo matumizi ya mbegu bora na mbolea katika kilimo cha zao hilo.

No comments

Powered by Blogger.