SAIMON SIRILO KUZINDUA KITABU CHA UJASIRIAMALI ITIGI, SINGIDA
Na Dotto Mwaibale, Singida
JINA la Saimon Sirilo kwa wadau wa ujasiriamali wa Mkoa wa
Singida na ya jirani siyo geni kutokana na jinsi anavyojitoa kwa hali na mali
kufundisha makundi ya watu katika kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali
ili kujikomboa kiuchumi.
Sirilo ni mkufunzi mbobezi wa masuala ya ujasiriamali ambaye
makao makuu yake yapo Itigi mkoani Singida.
Ni watu wachache mno wenye moyo wa kujitolea kama alionao Sirilo
wakati wote amekuwa ni mwalimu wa kutoa elimu hiyo tena kwa gharama zake
akishirikiana na wadau wengine wa maendeleo.
Licha ya kujitolea kwa kiasi hicho ameona haitoshi hivyo
ameandika kitabu maalumu kinachoelezea masuala mbalimbali ya ujasiriamali lengo
likiwa ni kuwasaidia wajasiriamali wakongwe na chipukizi kujifunza mbinu za ujasiriamali.
Kitabu hicho anatarajia kukizindua rasmi Disemba 13, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Sirilo alisema watu wengi
wamekuwa na shauku ya kujua ndani ya kitabu hicho alichokipa jina la “MJASIRIAMALI
WA LEO, TAJIRI WA KESHO” kutakuwa na mambo gani.
Sirilo alisema ndani ya kitabu hicho kuna mambo mengi ya
msingi yanayohusu masuala ya ujasiriamali na mbinu za kutengeneza
pesa kupitia kazi hiyo ambayo haimbagui mtu kwa umri wake.
“ Napenda kuwajulisha wadau wangu kuwa mada zote ambazo huwa
nawafundisha wajasiriamali, sasa nimeziweka katika maandishi ili yaendelee kuwa
msaada wakati wote hata kama sitakuwepo,” alisema Sirilo.
Sirilo aliyataja masomo yaliyopo katika kitabu hicho kuwa ni
Fursa adhimu zilizopo mkoani Singida, Ufugaji wa Kuku, Kilimo cha Matikiti,
Bajeti, Mauzo na Masoko, Huduma kwa wateja na Elimu ya fedha.
Alitaja masomo mengine kuwa ni baadhi ya Biashara zinazoweza
kumtoa mtu haraka kiuchumi na bidhaa za viwanda vidogo ikiwemo, Sabuni aina
zote, karanga za mayai, klipsi, batiki, keki na kadhalika.
Aidha, Sirilo alisema Kitabu hicho kitakuwa ni mkombozi kwa
wajasiriamali, hivyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote pamoja na wajasiriamali kufika kushiriki kwenye uzinduzi huo ili waweze kujipatia nakala ya kitabu
hicho kwa bei ya Sh.10000 tu.
Alisema uzinduzi huo utafanyika kuanzia saa 6:00 mchanna Ukumbi
wa Penda- Meri uliopo Mjini Itigi.
Kwa mawasiliano zaidi kuhusu uzinduzi huo unaweza kuwasiliana
na Saimon Sirilo Mwandishi wa kitabu kwa namba ya simu 0744445060.



No comments