Header Ads

TFRA YAWEKA MKAZO MPYA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

Afisa Udhibiti Ubora wa Mbolea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Henerico Renatusi, kutoka TFRA, akizungumza wakati wa mafunzo ya uanzishaji wa biashara ya mbolea yaliyofanyika katika Ukumbi wa Neema Craft Manispaa ya Iringa,

Na Godwin Myovela

IRINGA – Katika juhudi za kuimarisha tija ya kilimo na kuongeza uelewa sahihi wa matumizi ya mbolea nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa vyama vya ushirika kufungua vituo vingi vya usambazaji mbolea vijijini, ili kuwafikia wakulima walio mbali na huduma hizo za msingi.

Mafunzo ya uanzishaji wa biashara ya mbolea yaliyofanyika katika ukumbi wa Neema Craft Manispaa ya Iringa, yamewakutanisha washiriki 97, hatua inayoonesha mwamko mpya wa sekta binafsi kushiriki katika kuongeza uelewa na kuboresha ubora wa huduma za kilimo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Udhibiti Ubora wa Mbolea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Henerico Renatusi, alisema TFRA inaendelea kuwekeza nguvu kubwa katika ushirikiano na vyama vya ushirika kwa lengo la kuhakikisha vituo vya kusambaza mbolea bora vinaongezeka maeneo ya vijijini ambako ndiko wakulima wengi wanapoishi na kufanya shughuli zao.

Alisema biashara ya mbolea ni biashara nyeti inayokwenda sambamba na huduma, hivyo kunahitaji watu wenye uelewa, uadilifu na weledi, ili kuhakikisha mbolea inayowafikia wakulima ni ile sahihi yenye viwango vya virutubisho vilivyokusudiwa kutoka kiwandani na isiyo na udanganyifu au uchakachuaji.

Renatusi alibainisha kuwa mafunzo hayo yanaangazia misingi mikuu ya uelewa—kuanzia kujua mbolea ni nini, aina za virutubisho, jinsi ya kuitunza ili isiharibike, hadi utambuzi wa sheria zinazoongoza biashara hiyo, ikiwemo makosa yanayoweza kufanywa na adhabu zake.

“Tunataka mfanyabiashara wa mbolea ajue anapokosea anawajibika kwa sheria gani, faini ipi inamhusu, na kwa kiwango gani,” alisema, akisisitiza umuhimu wa mafunzo kama njia ya kuimarisha uwajibikaji.

Alisisitiza kuwa matokeo sahihi ya matumizi ya mbolea kwa mkulima hutegemea sana elimu anayoipata kutoka kwa mfanyabiashara, kwani ndicho chanzo chake cha kwanza cha taarifa.

Katika hatua ya upandaji, alieleza kuwa mbolea yenye phosphorus ndiyo sahihi kwa ajili ya kuimarisha mizizi, kisha nitrogen hutumika siku 21 baada ya kupanda kwa ajili ya ukuaji wa majani, na baadaye potassium siku 42 kwa ajili ya utungaji wa maua, mimba na punje.

Alisema huu ndio msingi wa lishe linganifu ya mimea, ambapo hatua moja inaiandaa nyingine ili hatimaye mkulima aweze kupata mavuno yenye tija na ustawi wa mazao kwa ujumla.

Pamoja na hilo, alikumbusha kuwa kanuni nne za matumizi sahihi ya mbolea (4Rs)—mbolea sahihi, sehemu sahihi, kiwango sahihi na muda sahihi—ndizo dira kuu za kuongeza uzalishaji na kupunguza hasara kwa mkulima.

Renatusi alisisitiza kuwa Sheria ya Mbolea inamtaka kila mfanyabiashara anayeanzisha biashara hiyo kupitia mafunzo rasmi ambayo yatamsaidia kuelewa huduma anayoitoa, ili aweze kutoa ushauri sahihi na weledi kwa wakulima.

Akifafanua dhamira ya mamlaka hiyo, alisema TFRA imekuwa mstari wa mbele si tu katika udhibiti wa ubora wa mbolea, bali pia katika kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na wakulima, ili kuhakikisha uelewa sahihi unawafikia wadau wote katika mnyororo wa thamani.

Kwa sasa, TFRA inaendesha kampeni maalumu inayojulikana kama “Mali Shambani Silaha Mbolea”, ikilenga kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa kuzingatia weledi na tahadhari, kama ilivyo kwa silaha inayohitaji ustadi mkubwa ili isije ikamdhuru mtumiaji.

“Mbolea ni silaha ya shambani. Ikitumika vibaya inaweza kuharibu mazao, lakini ikitumika kwa usahihi inaweza kumkomboa mkulima kutoka kwenye umasikini,” alisema Renatusi kwa msisitizo.

Kwa Malengo ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Renatusi alisema shabaha ni kuhakikisha mkulima anayefanya kilimo cha tija anapata kati ya magunia 25 hadi 30 kwa ekari, akisisitiza kuwa eneo hilo limebarikiwa mvua za kutosha na hali nzuri ya hewa.

Alieleza kuwa baada ya miaka mingi ya kutoa mafunzo kwa mfululizo, hatimaye mabadiliko makubwa yameanza kuonekana, kwa eneo la Nyanda za Juu Kusini sasa kuwa kinara nchini kwa matumizi sahihi ya mbolea, uelewa wa wakulima umeongezeka, na wafanyabiashara wengi wameimarika kitaaluma—ishara ya mafanikio ya kazi ya pamoja kati ya TFRA na wadau wa ushirika.Mafunzo yakiendeleaa.Taswira ya mafunzo hayo.Wahitimu wa mafunzo hayo wakionesha vyeti vyao. 

No comments

Powered by Blogger.