NAIBU KATIBU MKUU ATOA SIKU 14 MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI WA KITUO CHA MAFUNZO YA WAKULIMA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo. Mha. Athumani Kilundumya ametoa siku 14 kwa mkandarasi MACRO TECH anayefanya kazi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Kituo cha Mafunzo kwa Wakulima cha Mkindo, Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro kiwe kimekamilika kama mikataba inavyosema.
Amesema hayo tarehe 8 Januari 2026 na kusisitiza kuwa mkandarasi huyo yuko katika hatua ya awali katika ujenzi kwa asilimia 10 na endapo tashindwa kukamilisha ujenzi ndani ya siku hizo 14, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake kama mkataba unavyoelekeza.
‘’Nasikitika sana kuona kazi hazijatekrlezwa kwa mujibu wa makubaliano, na kwa upande wa Serikali tumekamilisha kila kitu lakini mkandarasi wetu umetuangusha huna sababu yoyote ya kueleza kazi ipo asilimia 10 na unapaswa kukabidhi kazi hii Januari 2026, huku dalili ninazoziona huwezi kufika’, amesema Naibu Katibu Mkuu Mha. Kilundumya.
Amesema kuwa Serikali inaelekeza kazi wapatiwe wakandarasi wa ndani lakini baadhi yao wanashindwa kutoa matokeo hali ambayo inakatisha tamaa kwa Serikali na jamii kwa ujumla.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu ameelekeza wahandisi wa Wizara ya Kilimo kuanza kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha mradi huo unajengwa vizuri ili wakulima waanze kupata mafunzo kama dhamira ya Serikali inavyotaka.
Mradi huo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo kwa wakulima 70 hadi 100 ambao watakuwa na uwezo wa kulala hapo hapo.
Aidha Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 653,398,555.20 utakuwa na darasa, mabweni, uzio pamoja na kibanda cha mlinzi, vyoo na ukarabati wa majengo mengine ya utawala.



No comments