Header Ads

NAIBU WAZIRI WA KILIMO ASISITIZA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI


 Wakulima wa Kata ya Nyida, Wilaya ya Shinyanga wamepata fursa mpya ya kuimarisha kilimo chao kupitia mradi wa umwagiliaji wa Nyida, mradi unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao kama Mpunga, na kuboresha maisha ya kaya zaidi ya 1,500.  Mradi unatekelezwa na Serikali Kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC).

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo tarehe 8 Januari 2026, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amewataka wakulima kuutunza mradi huo kwa manufaa yao wenyewe huku akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kumkomboa mkulima kutoka kilimo cha kutegemea mvua na kuhimiza kilimo cha uhakika kupitia umwagiliaji.

"Niwaombe wananchi, huu mradi ni wenu na wenye jukumu la kuutunza ni ninyi wenyewe. Hivyo, mkiuharibu mradi mtakaoteseka ni ninyi," amesisitiza Mhe. Silinde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema kuwa Mkoa huo unaendelea kuimarisha Sekta ya Kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi.   Amefafanua kuw katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, Mkoa wa Shinyanga umepanga kulima hekta 661,236 za mazao ya chakula na hekta 99,814 za mazao ya biashara, huku umwagiliaji ukiwa nguzo muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akiwasilisha taarifa ya mradi, Mhandisi Ebenezer Kombe amesema bwawa la umwagiliaji la Nyida lina uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 7.8 za maji, likihudumia hekta 800 za mashamba na kuongeza eneo la umwagiliaji hadi hekta 1,500 katika maeneo jirani. 

Nao wakulima wanufaika kupitia Skimu ya Umwagiliaji Twende Pamoja Nyida wameeleza kuwa mradi huo utawawezesha kulima mwaka mzima, kuongeza mavuno, kipato cha kaya, ajira na usalama wa chakula, huku wakipunguza utegemezi wa mvua zisizotabirika.

No comments

Powered by Blogger.