UCHUMI JUMUISHI WAPEWA MSUKUMO: ECONOMIC SOCIAL RESEARCH FOUNDATION NA FANRPAN WAKUTANA DODOMA KUJADILI MRADI WA MNYORORO WA THAMANI

Na Dotto Mwaibale, Dodoma
TAASISI ya Economic and Social Research Foundation (ESRF),
inayojihusisha na tafiti za kisera na kutoa mapendekezo kwa taasisi za serikali
na binafsi katika utekelezaji wa sera za nchi, kwa kushirikiana na FANRPAN,
zimekutana jijini Dodoma kujadili mradi wa uchumi jumuishi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi wa
Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt. Yasinta Nzogela,
ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema
uchumi jumuishi ni mradi unaoratibiwa na FANRPAN, taasisi ya kikanda barani
Afrika inayojihusisha na utafiti wa sera, huku ESRF ikiwa mratibu wa utekelezaji
nchini Tanzania.
Alisema lengo kuu la mradi huo ni kuangalia namna ya kuwa na
uchumi wa mzunguko ambapo hakuna rasilimali itakayopotea katika mnyororo wa
thamani kuanzia uzalishaji shambani hadi kufika kwa mlaji.
“Maana yake ni kwamba kila kitu kiongezwe thamani na
kutumika. Kwa mfano, mmea hutumia virutubisho kutoka kwenye udongo na kuzalisha
chakula; binadamu na wanyama tunakula, kisha mabaki yanarejeshwa tena shambani
kama mbolea, na mzunguko unaendelea,” alisema Dkt. Nzogela.
Alifafanua kuwa mzunguko huo unaohusisha matumizi ya maji,
mbolea na uongezaji thamani mdogo mdogo ndiyo unaoitwa uchumi jumuishi, ambao
pia umepewa kipaumbele katika dira ya maendeleo ya mwaka 2050, inayosisitiza
utunzaji wa mazingira na uchumi endelevu.
Aidha, alisema kuwa kufikia uchumi wa kati kunahitaji
kuimarisha dhana ya uchumi jumuishi, kwani inafungua fursa nyingi za ajira
katika mnyororo wa thamani.
“Tukiangalia uchafu unaotokana na uzalishaji shambani, siyo
uchafu bali rasilimali. Tukitumia teknolojia kuuchakata, tunaweza kupata mbolea
ya asili (organic) yenye thamani kubwa kwa uzalishaji,” aliongeza.
Dkt. Nzogela alisisitiza kuwa utekelezaji wa dhana hiyo
kuanzia uzalishaji hadi matumizi utasaidia kuinua uchumi wa wananchi na kulinda
mazingira.
Kwa upande wake
Vivian Kazi ambaye ni Mtafiti Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa
Kimkakati na Machapisho wa Taasisi katika Nyanja za Jamii na Uchumi ESRF
alisema mradi huo wameuanza miaka mitatu iliyopita unaohusiana na uchumi
jumuishi kwenye mfumo wa chakula.
Alisema mradi huo wameufanya kwa kushirikiana na Tanzania,
Msumbiji pamoja na Zimbabwe na kuweza kuufanya katika kila nchi kuona namna
gani sera zao zinajikita au hazijikiti katika kusaidia kupunguza uharibifu au
upotevu wa mazao katika mchakato mzima tokea mazao yanapopandwa, kuvunwa mpaka
mlaji wa mwisho.
Pia aliongeza kuwa ni jinsi gani wanaweza kupunguza upotevu
huo kwa kutumia tena mabaki yote yanayotokana na chaakula kuanzia
kinapozalishwa hadi kinapofika mezani na kinaporudishwa tena kuzalishwa kwa
mara ya pili kwa maana kwamba mabaki yale kutumika kama mbolea lakini pia
vyakula vya wanyama na kadharika.
“Tumefanya utafiti huu karibu na Chuo Kikuu Ardhi tukijikita
zaidi upande wa sera ambazo zitaweza kushawishi watu wote wasiweze kutumia
chakula vibaya ama mabaki yanayotokana na chakula ili kuweza kuyatumia tena na
tena,” alisema Kazi.
Kuhusu, FANRPAN inaendelea kusaidia Tanzania kupitia
midahalo ya sera za kilimo na chakula, ikilenga ushirikishwaji wa jamii,
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mifumo endelevu ya chakula
kwa kushirikiana na taasisi za ndani kama ESRF.
Bi. Vivian Kazi, Mtafiti Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Kimkakati na Machapisho wa Taasisi katika Nyanja za Jamii na Uchumi ESRF, akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao kikifunguliwa. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt. Yasinta Nzogela, Bi. Vivian Kazi, Mtafiti Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Kimkakati na Machapisho wa Taasisi katika Nyanja za Jamii na Uchumi ESRF na Profesa Makarius Mdemu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi.
Profesa Makarius Mdemu kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi. akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990


No comments