Header Ads

DK. MPANGO AIPONGEZA TARI KWA JARIBIO LA KWANZA LA ZAO LA VIAZI MVIRINGO

Makamu wa Rais  Mstaafu Dk. Philip Mpango, (wa tatu kusho) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Thomas Bwana (wa pili kulia) wakionesha viazi mviringo ambavyo vimetokana na jaribio la kwanza la mbegu ya viazi mviringo lililofanywa na TARI na kuonesha mafanikio makubwa katika shamba la Dk. Mpango ililopo Kijiji cha Mayamaya, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi  Uhaulisha wa Teknolojia TARI, Dk. Sophia Kashenge, Mtafiti wa mbegu hiyo, Dk.Owekisha Kwegizela na Afisa Mawasiliano Mkuu TARI, Eveline Mpasha.

.....................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Makamu wa Rais  Mstaafu Dk. Philip Mpango, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kwa kusimamia jaribio la kwanza la Mbegu ya viazi mviringo ambalo limeonesha mafanikio makubwa katika shamba lake lililopo Kijiji cha Mayamaya, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Kutokana na mafanikio hayo Dk. Mpango amewataka wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa ya kulima zao hilo pindi utafiti utakapokamilika.

“ Wakazi wa  Dodoma sasa tuanze kuchangamkia hii fursa na TARI wako tayari kutusaidia kwa kutupatia mbegu bora zinazofaa zaidi na hii itatusaidia kuwa na chakula na kipato kwa ajili ya kusaidia watoto wetu kwenda shule. Dodoma siyo nusu jangwa, ni maarifa tu ya kupata na kuvuna maji kwa ajili ya kuendeleza kilimo, hatuwezi kuendelea kwa kutegemea mtama, mahindi, zabibu au alizeti pekee lazima tuongeze na mazao mengine” alisema  Dk. Mpango.

Jaribio hilo la kwanza lilichukua  siku 104 za majaribio shambani hadi kuvuna limedhihirisha kuwa zao la viazi mviringo linaweza kustawi katika mazingira ya  Mkoa wa Dodoma na kuufanya kuwa na fursa mpya ya zao la chakula na biashara ambalo linaweza kuwasaidia wananchi wa mkoa huo kuondokana na umasikini.

Akiongelea  kuhusu jaribio hilo na matokeo yake,  Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Thomas Bwana amemshukuru Dk. Mpango kwa kukubali TARI kuweka jaribio  la viazi mviringo katika shamba lake  na kueleza kuwa  TARI imepanga kuweka majaribio ya zao hilo kwa wakulima wadogo wanaolima kwa kutegemea mvua.

Katika hatua nyingine Dk. Bwana ameongeza kuwa  TARI itaendelea na majaribio ya utafiti wa mazao katika maeneo mbalimbali nchini  ili kuondoa dhana iliyojengeka ya  ikolojia  hii ni ya mazao fulani pekee na kuwaomba wananchi hususani wakulima  kuwakaribisha TARI kuweka majaribio ya utafiti katika mashamba yao.

Kwa mujibu wa Mtafiti Kiongozi  wa zao la viazi mviringo kutoka kituo cha TARI - Uyole Dk. Owekisha Kwigizila, mbegu hiyo  mpya ya TARI ina sifa ya kukomaa kwa muda mfupi wa takribani siku 90, kustahimili ukame na baadhi ya magonjwa pamoja na kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 35 hadi 40 kwa hekta moja.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mayamaya walioshiriki katika zoezi la uvunaji wa viazi hivyo wameonesha kustaajabishwa na kustawi kwa zao hilo katika Kijiji hicho cha Mayamaya na kueleza kuwa hiyo ni mara yao ya kwanza kuona zao hilo la viazi likilimwa  na kustawi Mkoani Dodoma na kuonyesha shauku kubwa ya kujaribu kulima zao hilo katika mashamba yao,

Utafiti huo wa zao la viazi Mkoani Dodoma bado unaendelea ili kukamilisha hatua zote muhimu kabla ya mbegu hiyo kuingizwa rasmi sokoni.

Mafanikio hayo yanaendelea kuthibitisha kuwa Dodoma inaweza kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kupitia nguvu ya utafiti, ubunifu na teknolojia za kilimo  na kubadilisha maisha ya wakulima wa  Mkoa wa Dodoma.

Makamu wa Rais  Mstaafu Dk. Philip Mpango na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Thomas Bwana wakionesha viazi mviringo ambavyo vimetokana na jaribio la kwanza la mbegu ya viazi mviringo lililofanywa na TARI na kuonesha mafanikio makubwa katika shamba lake lililopo Kijiji cha Mayamaya, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
 

No comments

Powered by Blogger.