MEJA JENERALI MSTAAFU MUHUGA MFANO WA KUIGWA
............................
Na Claudia Kayombo
BAADA ya kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi Watanzania
(JWTZ), katika nyadhifa mbalimbali, ingekuwa sababu kwake ya kutojishughulisha
na jambo jingine la kujiingizia kipato.
Huenda angeweza kuwaza ajifanyie kazi rahisi na muda
mwingi akitumia kupumzika, kula na kunywa vinywaji laini kuupa burudani mwili
wake.
Lakini imekuwa tofauti kwa Meja Jenerali mstaafu,
Raphael Muhuga. Yeye aliwaza ajikite katika kilimo bora cha kisasa ufugaji wa
ng’ombe, samaki, mbuzi na kondoo pamoja na kuku wa kisasa.
Kwake hakuona kama kukumbatia pensheni ni jambo la
msingi badala yake akaona bora atumie nguvu na maarifa aliyojaliwa na Mungu, kuanzisha
kilimo na ufugaji ili kujiongezea kipato na kutoa fursa ya ajira kwa wengine wanaomzunguka.
Uzalishaji huo wenye tija anaufanya chini ya
mwamvuli wa Kampuni aliyoifungua ya RM Holding Limited, sanjari na kiwanda cha
kisasa cha kuzalisha mchele chenye mashine yenye uwezo wa kugawa madaraja manne
ya mchele, daraja la kwanza ndilo bora zaidi, daraja la pili, tatu na la nne
ambalo ni la mwisho.
Kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu
kama Sabasaba ambako bidhaa zake zilibamba vilivyo, Ofisa oparesheni wa miradi wa
kampuni hiyo , Carlos Muhuga, anasema kilimo hicho cha mpunga, baba yake Meja
Jenerali mstaafu Muhuga anakifanya Chita mkoani Morogoro huku kiwanda hicho cha
kuchakata mpunga na kuongeza thamani kwa maana mchele, kikijengwa Ifakara eneo
la Katindiyuka, mkoani humo.
Anasema kiwanda hicho ni kikubwa katika Bonde la
Kilombero kina uwezo wa kuchakata mpunga tani sita kwa saa moja na kuwa kina
stoo yenye uwezo wa kuhifadhi magunia ya mpunga 150.
Anasema ufugaji wa ng’ombe, mbuzi. Kondoo na kuku
unafanyika Kirasarawe II eneo la Vumilia
Ukooni, mkoani Dar es Salaam huku mabwawa makubwa sita ya ufugaji wa samaki yakiwa
mkoani Mwanza.
Ofisa oparesheni huyo anasema kupitia kilimo na
ufugaji, wametoa ajira za muda na za kudumu kwa watu zaidi ya 50 ambao wengi
wao ni wanawake.
Mstaafu huyo ambaye kampuni yake imeshiriki katika
Maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu ambayo yanatimiza miaka 50 tangu kuasisiwa
kwake mwaka 1976, naye ameungana na wajasiriamali mbalimbali nchini na nje ya
nchi kuonesha bidhaa zake bora anazozalisha ukiwamo mchele.
Carlos anasema mchele huo soko lake kwa kiasi
kikubwa lipo nchini na kwa kiwango kidogo unauzwa nje katika mataifa jirani
ikiwamo Rwanda.
Hata hivyo, Carlos akizungumza katika maonesho hayo
yaliyoanza rasmi Juni 28, mwaka huu, na kufikia tamati Julai 13, anasema kutokana
na kiwanda chao kuwa na mahitaji makubwa ya malighafi kwa maana ya mpunga,
wanalazimika pia kununua kutoka kwa wakulima wadogo wanaowazunguka.
Anatanabahisha kuwa Meja Jenerali Muhuga anazo eka
250 hadi 350 na kuwa licha ya kuwa na eneo kubwa mtaji ni mdogo na kueleza kuwa
mapato wanayopata bado hayakidhi mahitaji makubwa ya malighafi hiyo katika
kiwanda hicho.
Anasema soko la mchele kwa kiasi kikubwa
linapatikana hapa nchini licha ya kuwa wakati mwingine unauzwa kwa kiasi kidogo
nje ya nchi huku kuku na mifugo mingine nayo soko lake likipatikana hapa nchini.
“Wanunuzi wanakuja shambani kufuata kuku, kwa
ujumla hakuna shida kubwa ya soko la mazao ya kilimo na hata mifugo”, anasema.
Anasema licha ya upatikanaji wa soko lakini bado
bei ya mchele wakati mwingine inakuwa ni ya chini kutokana na mchele unaotoka
nje ya nchi kuuzwa nchini kwa bei nafuu.
Pia anabainisha kuwa gharama ya vipuri na mashine
mbalimbali za kilimo ni aghari sana ambapo kuna wakati inakuwa mzigo kwa mjasiriamali
kuweza kuzimudu gharama hizo. Aidha, kutokana na bei za mchele kutokuwa
linganifu kuna wakati mkulima anapata hasara.
Kuhusu mikopo ambayo inaweza kumkwamua mkulima
Carlos anasema siyo rafiki kwasababu haina riba nafuu ukilinganisha na
uwekezaji unafanywa katika kilimo.
Anasema Serikali ina nia njema na kazi zinazofanywa
na wajasiriamali hapa nchini kinachokwamisha ni watendaji wachache wasiosimamia
haki katika nafasi zao.
Anasema bidhaa zao zote mchele, maziwa, mayai nyama za kuku pamoja na samaki zinauzwa katika Supermarket yao iliyopo makao makuu eneo la Mbagala Tuangoma.




No comments