Header Ads

𝐔𝐙𝐀𝐋𝐈𝐒𝐇𝐀𝐉𝐈 𝐊𝐎𝐑𝐎𝐒𝐇𝐎 𝐖𝐀𝐏𝐀𝐀, 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀 𝐘𝐀𝐋𝐄𝐍𝐆𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐈 𝐌𝐈𝐋𝐈𝐎𝐍𝐈 𝐌𝐎𝐉𝐀 𝟐𝟎𝟑𝟎

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi Siku ya Korosho wakati wa Maonesho ya Wakulima Nanenane  na Maadhimisho  miaka 10 ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) yaliyofanyika Uwanja wa Maonesho wa Dk. John Malecela Jijini Dodoma akihutubia Agosti 6, 2026. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu TARI, Thomas Bwana na kulia ni Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Hamidu Mponda.

...............................

UZALISHAJI wa zao la korosho nchini umeendelea kuongezeka kutokana na juhudi zinazofanywa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa CBT, Hamidu Mponda, alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Francis Alfred, katika maadhimisho ya Siku ya Korosho yaliyofanyika kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane na maadhimisho ya miaka 10 ya TARI.


Maadhimisho hayo yalifanyika Agosti 6, 2026, katika Uwanja wa Maonesho wa Dk. John Malecela jijini Dodoma.


Mponda alisema uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 210,000 zilizozalishwa katika msimu wa 2021/2022 hadi kufikia tani 618,000 katika msimu wa 2025/2026.


Alisema ongezeko hilo limewapa matumaini ya kufikia lengo la kuzalisha tani milioni moja za korosho ifikapo mwaka 2030.


Mponda alisema baada ya kupata mafanikio makubwa katika kuongeza uzalishaji, CBT imeamua kuelekeza nguvu zaidi katika kuongeza thamani ya zao hilo ili wakulima, Serikali na wadau wengine wanufaike zaidi.


“Pamoja na zao hili kuleta tija kwa wakulima na kuongeza mapato kwa Serikali, haliwezi kutoa tija kubwa ikiwa tutaendelea kuuza korosho ghafi,” alisema.

 

Alisema katika msimu wa 2025/2026, kati ya tani 618,000 zilizozalishwa, tani 439,000 ziliuzwa nje ya nchi zikiwa katika hali ya korosho ghafi.


Kwa mujibu wa Mponda, hali hiyo inasababisha Tanzania kupoteza fursa mbalimbali ikiwamo ajira, mapato na manufaa ya kikodi ambayo yangeweza kupatikana kupitia uongezaji thamani wa zao hilo nchini.


Alisema CBT imekuja na mpango wa kuongeza thamani ya korosho kwa lengo la kuchagiza ulaji wa bidhaa zinazotokana na zao hilo, kupanua soko kwa wakulima, kukuza viwanda vya ubanguaji na kuongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na korosho.


Mponda alisema mpango huo pia utasaidia kuimarisha soko la ndani, hususan pale ambapo soko la nje litakuwa halina nguvu, hivyo kuhakikisha wakulima wanaendelea kupata soko la uhakika na motisha ya kuendelea kuzalisha na kubangua korosho.


“Kutokana na mafanikio hayo, leo imekuwa dhima yetu kuwaalika Watanzania kutumia bidhaa mbalimbali zinazotokana na korosho, ikiwa ni pamoja na kuimarisha afya zao kutokana na zao hili kuwa na tija,” alisema Mponda.

 

Aliongeza kuwa korosho ina virutubisho muhimu kwa mwili wa binadamu, hivyo kuwataka Watanzania kumuunga mkono mkulima kwa kuongeza matumizi ya korosho pamoja na bidhaa nyingine zinazotokana na zao hilo.Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa CBT, Hamidu Mponda, akizungumzia mafanikio ya zao la korosho na ongezeko la uzalishaji.Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa CBT, Hamidu Mponda, akiwa na Mkurugenzi  Uhaulisha wa Teknolojia TARI, Dk. Sophia Kashenge wakati wa Maadhimisho hayo.Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi Siku ya Korosho na Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora wa CBT, Hamidu Mponda, wakiangalia bidhaa zitokanazo na korosho zilizoandaliwa kwa ajili ya Maadhimisho hayo ambazo ni korosho, maziwa ya korosho, maandazi ya korosho, mvinyo wa korosho na nyinginezo.

Habari hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.

No comments

Powered by Blogger.