WANANCHI WAFURIKA MAONESHO NANENAANE KINYAMWEZI
................................
Na Mwandishi Wetu.
MAONYESHO ya Kilele cha Sikukuu ya wakulima, Nane Nane yaliyofanyika kwa mara ya kwanza katika Kituo cha Rasiliamali Kilimo, Kinyamwezi, Ilala, Dar es Salaam, yamevuka malengo na matarajio, baada ya wananchi wengi kujitokeza kwa lengo la kujifunza mbinu na ubunifu wa kilimo cha kisasa.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Afisa Kilimo wa Halmashauri wa Jiji la Dar es Salaam, Robert Lubote, wakati akizungumza katika kilele cha sikukuu hiyo.
Lubote alisema kuwa kwa mara ya kwanza kilele cha nane nane kimefanyika katika kituo cha rasiliamali kilimo Kinyamwezi kwa maelekezo ya Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jiji la Dar es Salaam, Herihuruma Mabelya.
Alisema kuwa maonyesho hayo yamevuka malengo kutokana na matarajio yao.
Lubote alisema kuwa malengo yao yalikuwa kwa watu 300 ambao wangeweza kufika katika maonyesho hayo kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimali za ubunifu wa kilimo cha kisasa.
"Matarajio yetu yamevuka malengo, zaidi ya watu 700 na wengine wanaendelea kufika kwa lengo la kujifunza mbinu na ubunifu wa kilimo cha kisasa,' alisema Lubote.
Alisema kuwa pamoja na maonyesho hayo yanafanyika kwa mara ya kwanza katika kituo hicho, lakini mwitikio wananchi umekuwa mkubwa.
Afisa huyo alisema kuwa lengo la mkurugenzi kuagiza maonyesho hayo yafanyike Kinyamwezi ni kutaka yafanane na yale yalifanyika kitaifa mkoani Morogoro.
Alisema kuwa mkurugenzi alikusudia mwananchi ambaye alipanga kwenda Morogoro ambako kilele cha Nane Nane kitaifa kilifanyika angeweza kufika Kinyamwezi na kujifunza mambo mbalimbali ya kilimo.
Pia alisema kuwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi waliofika katika maonyesho hayo watajipanga zaidi kwa mwakani.
Alisema kuwa maonyesho ya mwakani wataboresha zaidi.
Baadhi ya wananchi waliofika katika maonyesho hayo, alifurahia ubunifu wa kilimo cha kisasa unaofanywa na kituo hicho.
Mmoja wa wananchi hayo, Fedelis Katabalo, alisema ameweza kujifunza kilimo cha kisasa cha migomba, nyanya, viungo vya mboga, mpunga na aina mbalimbali ya mboga.
Alisema kuwa amepata mafunzo mazuri kutoka kwa wataalumu wa kilimo na atakwenda kufanyia kazi shambani kwake
Naye, Fatuma Abas, alimpongeza mkurugenzi wa Jiji kwa kuanzisha maonyesho katika kituo cha rasiliamali kilimo Kinyamwezi, kwani wameweza kupata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya kilimo cha kisasa.



No comments