MTAFITI DK. CECILIA CHINA; KUTOKA SHILINGI MILIONI 20 HADI SAFARI YA UCHUMI WA DOLA TRILIONI MOJA
Mtafiti Dk. Cecilia China ambaye ni mwanasayansi na Mhadhiri kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) na Mwanzilishi wa Kampuni ya Afritech Organe Leather Co.Ltd, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Agosti 19, 2026 katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Jijini Tanga kuhusu mafanikio makubwa baada ya kugundua maganda ya korosho kuzalisha kimiminika kinachojulikana kama Cashew Nut Shell Liquid (CNSL), ambacho hutumika kutengeneza dawa inayotumika katika usindikaji wa ngozi.
.........................
SERIKALI ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1986 ilichukua hatua muhimu ya kuimarisha
uratibu, ukuzaji na usimamizi wa tafiti za kisayansi na teknolojia kwa
kuanzisha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Sheria ya
Bunge Na. 7 ya mwaka huo.
Taasisi hiyo
ilirithi majukumu ya lililokuwa Baraza la Taifa la Utafiti wa Kisayansi
(UTAFITI) na kupewa jukumu la kuwa mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya
sayansi, teknolojia na matumizi ya matokeo ya tafiti katika kukuza maendeleo na
uchumi wa taifa.
Tangu
kuanzishwa kwake, COSTECH imekuwa kichocheo muhimu cha tafiti na ubunifu,
ambapo baadhi ya bunifu zimeingia katika uzalishaji na biashara, zikionyesha
namna uwekezaji katika sayansi na teknolojia unavyoweza kufungua fursa za
ajira, viwanda na biashara ya kimataifa.
Mtafiti Dk. Cecilia China na Afisa Masoko wa Kampuni hiyo, Emile Gabriel Isangya (kulia), wakionesha bidhaa za ngozi zinazotengenezwa na kiwanda chao.
..................................
Miongoni mwa
mifano hiyo ni wa Dk. Cecilia Rolence China, mtafiti kutoka Taasisi ya Sayansi
na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), mama wa watoto wawili, mjasiriamali
na mmiliki wa kampuni ya Kampuni ya AfriTech Organic Leather pamoja na kiwanda kilichopo
jijini Arusha.
Mwaka 2019,
Dk. Cecilia alikuwa miongoni mwa washindi wa Mashindano ya Ubunifu ya MAKISATU
na kupitia ushindi huo alipata ufadhili wa Shilingi milioni 20 kutoka Serikali
kupitia COSTECH. Uwekezaji huo wa awali katika wazo la ubunifu leo umefikia
hatua ya uzalishaji na biashara.
Dk. Cecilia
analenga kutumia maganda ya korosho kuzalisha kimiminika kinachojulikana kama
Cashew Nut Shell Liquid (CNSL), ambacho hutumika kutengeneza dawa inayotumika
katika usindikaji wa ngozi.
Ubunifu huo
unaunganisha sekta mbili muhimu za uchumi wa Tanzania—korosho na mifugo—katika
mnyororo mmoja wa thamani.
Mtafiti Dk. Cecilia China, akionesha vipande vya ngozi ambayo imekwisha andaliwa na kiwanda hicho tayari kuwa sokoni na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
.................................
Tanzania ilizalisha zaidi ya tani 528,000 za korosho katika msimu wa 2024/25, huku maganda yakifikia wastani wa asilimia 70 hadi 75 ya uzito wa korosho mbichi. Hii inaonesha ukubwa wa malighafi inayoweza kupatikana iwapo korosho zitachakatwa ndani ya nchi.
Kwa upande
mwingine, Tanzania ilikuwa na zaidi ya ng’ombe milioni 39.2 mwaka 2024, mbuzi
milioni 28.6 na kondoo milioni 9.7, huku uzalishaji wa ngozi ghafi ukifikia
tani 55,410.
Takwimu hizi
zinaonesha kuwa Tanzania tayari ina malighafi za kutosha, lakini changamoto
imekuwa ni kuongeza thamani kabla ya malighafi hizo kusafirishwa nje ya nchi.
Ngozi ghafi
zinaweza kusindikwa na kuwa bidhaa zenye thamani kubwa zaidi kama viatu,
mikoba, mikanda, samani na bidhaa nyingine zinazohitajika katika soko la ndani
na la kimataifa.
Mtafiti Dk. Cecilia akisisitiza jambo wakati akizungumzia mafanikio ya utafiti alioufanya.
...............................
Dk. Cecilia
anajaribu kuweka sehemu ya suluhisho hilo ndani ya Tanzania kwa kuzalisha dawa
ya usindikaji wa ngozi kutokana na malighafi inayopatikana nchini.
Ikiwa
uzalishaji huo utafikia kiwango kikubwa cha kibiashara, manufaa yanaweza
kuonekana katika hatua mbalimbali kwa wakati mmoja. Maganda ya korosho yatapata
matumizi ya kiuchumi, wakulima watapata fursa mpya za kipato, viwanda vitapata
malighafi ya ndani na fedha zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje zitabaki
katika uchumi wa taifa.
Takwimu zinaonesha umuhimu wa hatua hiyo. Mwaka 2024, Tanzania ilisafirisha nje tani 6,689 za ngozi ghafi zenye thamani ya Shilingi bilioni 8.06. Hata hivyo, usindikaji wa ndani unaweza kuongeza thamani zaidi na kuimarisha mapato ya taifa.
Muonekano wa chupa zenye Vimiminika vilivyoandaliwa na kiwanda hicho kwa ajili ya kutengenezea ngozi.
................................
Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC) tayari kimetambua sekta ya bidhaa za ngozi zenye
thamani ya juu kuwa eneo muhimu la uwekezaji kutokana na uwezo wake wa kuongeza
ajira na kukuza viwanda.
Kwa mtazamo
huo, kazi inayofanywa na Dk. Cecilia haipaswi kuonekana kama uzalishaji wa dawa
pekee, bali ni sehemu ya kujenga ikolojia ya viwanda inayounganisha wakulima,
wafugaji, watafiti, viwanda na masoko ya kimataifa.
Dk. Cecilia
ameonesha nia ya kujenga kiwanda kikubwa mkoani Mtwara kutokana na ukaribu wa
malighafi ya korosho. Kiwanda hicho kinaweza kufungua nafasi za ajira kwa
wanawake na vijana katika ukusanyaji, usafirishaji, uzalishaji, ufungashaji na
shughuli nyingine za viwandani.
Mbali na
Mtwara, Dk. Cecilia anaangalia pia uwezekano wa kuwekeza katika Kanda ya Kati
inayojumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora, ambayo nayo imeanza
kuimarisha kilimo cha korosho.
Bidhaa kama mabegi, mikoba, pochi na nyinginezo zilizotengenezwa na kiwanda kinachomilikiwa na Dk. Cecilia zikioneshwa.
...............................
Akizungumzia mafanikio waliyofikia Dk. Cecilia anasema siyo haba kwani walianza na mtaji wa milioni 20 lakini sasa wamefisha mtaji wa shilingi milioni100.
Dk.Cecilia aliongeza kuwa kwa kuwa ndiyo wanaanza uzalishaji kwa msimu uliopita walikusanya maganda ya korosho kilo 3000 ambazo walizitumia kwa msimu mzima lakini msimu mpya wa mwaka huu wanatarajia kuongeza zaidi ya hapo.
"Uzalishaji kwa msimu uliopita ulikuwa mzuri, changamoto kubwa tuliyonayo ni ya kusafirisha hayo maganda kutoka Mtwara kuyapeleka Arusha na ndiyo maana tunafanya jitihada za kujenga kiwanda,' alisema.
WAKULIMA WAONA FURSA MPYA
Mkulima
Karimu Chipola kutoka Kijiji cha Mchichila wilayani Tandahimba anasema ubunifu
huo umeongeza thamani ya zao la korosho kupitia matumizi ya maganda ambayo
awali yalikuwa hayatumiki.
“Sisi wakulima tunashukuru sana kwa sababu tunaamini zao letu limeongezewa thamani na hivyo tunaweza kupata kipato kingine,” alisema Chipola.
Mdau wa
kilimo cha korosho, Dk. Fotunatus Kapinga, anasema lengo la tafiti ni kuhakikisha
zina manufaa kwa jamii.
“Utafiti uliofanywa na Dk. Cecilia umeonesha mafanikio makubwa na unaweza kumwezesha mkulima kupata faida zaidi kuliko kutegemea korosho pekee hasa baada ya zao hilo kuongezwa thamani kupitia utafiti huo,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk. Amos Nungu, akiwa na Dk. Cecilia wakati wa mkutano na wanahabari.
...............................................
Kuhusu COSTECH ; Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ni mshauri mkuu wa Serikali ya Tanzania katika masuala yote yanayohusu sayansi, teknolojia, na ubunifu kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Taasisi hii ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 7 ya mwaka 1986.
Kupitia Serikali COSTECH imekuwa ikitoa rasilimali fedha kwa ajili ya kuwezesha ufadhili wa bunifu mbalimbali.
...........................
Kijana Mohamed Namkwacha anasema amepata ajira kupitia ukusanyaji wa maganda ya korosho yanayosafirishwa kwenda Arusha.
“Awali hatukujua kama maganda haya yana thamani. Baada ya kupewa elimu na Dk. Cecilia, niliona ni fursa na nikaanza kujishughulisha na kazi hii,” alisema.
Kwa upande
wake, Mohamed Makusi anasema katika msimu uliopita walikusanya tani tatu za
maganda ya korosho kwa kushirikiana na vijana 10, wakiwamo wanawake watatu.
“Tunapongeza watafiti na COSTECH kwa kuleta bunifu zenye tija. Tunaiomba Serikali kuendelea kusaidia tafiti hizi ziwafikie wananchi badala ya kubaki kwenye makabati,” alisema Makusi.
SINGIDA YAJIPANGA KWA UWEKEZAJI
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatma Mganga, alimpongeza Dk. Cecilia kwa
ubunifu wake na kumkaribisha kuwekeza mkoani humo.
Alisema Mkoa
wa Singida umejipanga kuimarisha kilimo cha korosho, hasa katika Wilaya za
Manyoni na Itigi, na umeweka mazingira rafiki kwa wawekezaji katika sekta za
kilimo na viwanda.
“Mkoa wa Singida una ardhi yenye rutuba, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda na miundombinu mizuri ya barabara. Tunawakaribisha wawekezaji kuja kutumia fursa hizi,” alisema Dk. Mganga.
Dira ya
Maendeleo ya Taifa ya 2050 inalenga kujenga uchumi wa dola trilioni moja wenye
ushindani na tija. Uchumi huo hautajengwa na mradi mmoja au kiwanda kimoja,
bali na maelfu ya mawazo yatakayogeuzwa kuwa bidhaa, kampuni na viwanda.
Safari hiyo imeanza kupitia uwekezaji katika sayansi, teknolojia na ubunifu. Na wakati mwingine, mwanzo wake unaweza kuwa mdogo kama Shilingi milioni 20, lakini matokeo yake yakawa makubwa zaidi kwa taifa katika siku zijazo.
Muonekano wa Jengo la Makao Makuu ya Bodi ya Korosho Tanzania (CBT)......................................
Kuhusu Bodi ya Korosho Tanzania
Bodi ya korosho Tanzania ni Taasisi ya Umma iliyo chini ya
Wizara ya Kilimo iliyoundwa chini ya sheria ya Tasnia ya korosho Sura ya 203
Toleo la Mwaka 2023, inayoipa jukumu la usimamizi wa Tasnia ya korosho kwenye
mnyororo mzima wa thamani kuanzia kwa mkulima hadi kwa mlaji wa mwisho.
Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990



No comments