UTAFITI WA MFUMO WA KUHESABU SAMAKI MAJINI WAAKISI TAKWIMU ZA HAYATI MAGUFULI
Mhadhiri Msaidizi na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, Magoti Ernest Ndaro, akizungumza na Mwandishi wetu Dotto Mwaibale (hayupo pichani), wakati wa mahojiano maalumu kuhusu ubunifu wake wa mfumo wa kuhesabu vifaranga wa samaki katika Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika kwenye banda lao Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Usagara Jijini Tanga, Agosti 20, 2026.
.............................
UTAFITI na ubunifu wa kiteknolojia unaotumia Akili Unde (AI) katika kuhesabu samaki na vifaranga kwa usahihi umeibua mjadala mpya kuhusu uwezo wa teknolojia kubadili sekta ya ufugaji wa samaki nchini Tanzania.
Mfumo huo, unaojulikana kama AquaShield, umebuniwa na Mhadhiri Msaidizi na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Magoti Ernest Ndaro, na unalenga kutatua changamoto ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikikabili wafugaji wa samaki, ikiwemo kuhesabu vifaranga, kugundua magonjwa mapema na kupunguza hasara.
Ubunifu huo
pia umeibua kumbukumbu za Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli alipokuwa Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2010, ambapo
mara kwa mara aliwashangaza Watanzania kwa kutaja idadi na takwimu maalumu za
samaki na vifaranga.
Kwa baadhi
ya wananchi, uwezo huo uliwahi kuonekana kama jambo lisilowezekana, wakijiuliza
namna ambavyo kiongozi angeweza kujua idadi ya samaki waliopo kwenye maziwa au
vifaranga vilivyopo katika shughuli za uzalishaji.
Hata hivyo,
takwimu hizo zilihusisha taarifa za serikali na tafiti za kisayansi
zilizokusanywa kupitia ripoti za kiutafiti na doria zilizokuwa zikifanywa na
wataalamu wa sekta hiyo.
Tofauti ni
kwamba Magufuli alikuwa na uwezo wa kukariri na kutaja takwimu hizo kwa
msisitizo mkubwa katika hotuba na mikutano yake, jambo lililokuwa sehemu ya
mtindo wake wa uongozi na mawasiliano ya kisiasa.
Sasa, zaidi
ya muongo mmoja baadaye, teknolojia ya Akili Unde imeanza kutoa jibu la
kiteknolojia kwa swali lililokuwa likiwatatiza baadhi ya watu kuhusu namna ya
kupata idadi sahihi ya samaki na vifaranga.
Mfumo wa AquaShield unatumia teknolojia ya kamera na AI kutambua na kuhesabu samaki kwa haraka bila kuwagusa, huku pia ukiwa na uwezo wa kusaidia katika utambuzi wa dalili za magonjwa.
Mtafiti Magoti Ernest Ndaro Katika Kazi za NyanjaniMhadhiri Msaidizi na mtaalamu wa magonjwa ya samaki kutoka SUA, Magoti Ernest Ndaro, akiwa amevalia jaketi la uokoaji (life jacket) tayari kwa ajili ya kukusanya data na kufanya tafiti za nyanjani kwenye vizimba vya samaki.
..................................
UBUNIFU WAPATA MSHINDI WA PILI DUNIANI
Ubunifu huo
umefikia hatua ya kimataifa baada ya Mtafiti Magoti kuiwakilisha Tanzania na
kushika nafasi ya pili duniani katika tuzo za AI for Good Impact Awards 2026,
zilizofanyika Geneva, Switzerland, Julai mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kwenye banda la SUA wakati wa Maonesho ya Elimu, Ubunifu na Ujuzi yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Agosti 20, 2026, Magoti alisema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezeshaji wa serikali katika utafiti na ubunifu.
Alisema
serikali kupitia SUA imemwezesha kupata ajira, mshahara na ufadhili wa masomo,
hatua iliyompa nafasi ya kufanya tafiti mbalimbali hadi kufikia kugundua na
kuendeleza mfumo huo.
Magoti
alisema pia amefaidika na ruzuku za utafiti zinazotolewa ndani ya vyuo vikuu
vya umma pamoja na kutumia miundombinu ya maabara na vituo vya ufugaji samaki
vilivyojengwa kwa fedha za serikali.
“Nilishiriki katika miradi mikubwa inayofadhiliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau, kama vile mradi wa DigiFish na taasisi ya Serikali ya Tanzania Fisheries Research Institute (TAFIRI). Hii ilinipa fursa ya kupata rasilimali za uendeshaji wa tafiti za nyanjani,” alisema.
Alisema
kabla ya kwenda kwenye jukwaa la kimataifa, alishiriki katika maonesho ya
kitaifa ya ubunifu yanayoratibiwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia pamoja na COSTECH, ambako alishinda tuzo na kupata fedha zilizosaidia
kuendeleza ubunifu huo.
Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, Magoti akionesha namna bora ya ufugaji wa vifaranga vya samaki.
...........................
Kwa mujibu
wa Magoti, safari yake ya kwenda Switzerland pia iliungwa mkono na Wizara ya
Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Ubalozi wa Tanzania
nchini humo.
Alisema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Switzerland, Hoyce Temu, walihudhuria na kumuunga mkono katika jukwaa hilo.
AI KUPUNGUZA VIFO VYA VIFARANGA
Magoti
alisema moja ya changamoto kubwa ambayo AquaShield inalenga kuiondoa ni vifo
vya vifaranga vinavyotokana na njia za jadi za kuhesabu.
Kwa muda
mrefu, wafugaji wamekuwa wakitumia mikono au vyombo vidogo katika kuhesabu
vifaranga, hali inayoweza kuwachosha, kuwajeruhi na kuongeza uwezekano wa kufa
kabla ya kufikishwa kwenye mabwawa au vizimba.
“Kwa kutumia kamera, mfumo unaweza kuhesabu maelfu ya samaki kwa muda mfupi bila kuwagusa. Hii inapunguza msongo na majeraha yanayotokana na uhesabuji wa mikono,” alisema.
Mbali na
kupunguza vifo, mfumo huo unalenga kumsaidia mfugaji kupata idadi sahihi ya
vifaranga anavyonunua.
Kwa njia za
zamani, mfugaji na mfanyabiashara mara nyingi walitegemea makadirio, hali
iliyoweza kusababisha makosa au migogoro ya kibiashara.
Kwa kutumia
AI, mfugaji anaweza kupata taarifa sahihi zaidi kuhusu idadi ya vifaranga,
jambo linalomwezesha kupanga matumizi ya chakula, dawa na gharama nyingine za
uzalishaji.
Watafiti kutoka SUA, Ally Abdi na Magoti Ndaro {kulia), wakijadiliana jambo katika banda lao.
UTAMBUZI WA
MAGONJWA
AquaShield pia inalenga kusaidia katika utambuzi wa mapema wa magonjwa ya samaki.
Magoti
alisema kwa njia za kawaida, mara nyingi wafugaji hugundua tatizo baada ya
samaki kuanza kufa kwa wingi au kuonyesha dalili zinazoonekana wazi.
Teknolojia
hiyo inalenga kutumia AI kutambua mabadiliko ya kitabia na ishara za awali za
matatizo ya kiafya, hivyo kumpa mfugaji tahadhari mapema ili achukue hatua
kabla hasara haijawa kubwa.
Kwa upande
wa biashara, Magoti alisema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kuongeza tija
kwa kupunguza hasara na kuongeza usahihi katika uzalishaji.
Alisema hali hiyo inaweza kuwawezesha wafugaji kuzalisha samaki wengi wenye afya na kuwa na uwezo wa kutimiza mahitaji ya masoko makubwa, yakiwemo hoteli na viwanda vya kuchakata samaki.
MAFUNZO KWA WAFUGAJI
Magoti
alisema tayari wameanza kutoa mafunzo kuhusu mfumo huo kwa wafugaji na wadau wa
sekta ya ufugaji wa samaki, ambapo zaidi ya wafugaji 126 kutoka mikoa ya Kanda
ya Ziwa wamefikiwa.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha ubunifu huo hauishii kwenye maabara au kwenye tuzo za kimataifa, bali unawafikia wananchi wanaofanya shughuli za ufugaji wa samaki.
WADAU WATOA MAONI
Mtaalamu wa
ukuzaji viumbe maji kutoka Morogoro, Ally Abdi, alisema ubunifu huo una manufaa
makubwa kwa Taifa kwa sababu unaweza kupunguza muda unaotumika kuhesabu samaki
na vifaranga pamoja na kupunguza vifo.
“Mwanzo wafugaji walikuwa wakifanya makadirio kati ya wafanyabiashara na mfugaji ili kila mmoja apate faida, kwani hakukuwa na uhakika wa idadi halisi ya vifaranga anavyonunua. Hali hiyo ilimlazimu mfugaji wakati mwingine kuongezewa vifaranga kama fidia iwapo baadhi vingekufa,” alisema.
Abdi aliwataka wafugaji na wananchi kwa ujumla kuendelea kuifahamu na kuitumia teknolojia hiyo, akisema inaweza kuokoa muda na kuuwezesha kutumika katika shughuli nyingine za uzalishaji.
Mkuu wa
TAFIRI Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Taus Khitentya, alisema utafiti huo unaweza
kuwa mkombozi kwa wafugaji na wavuvi wa Kanda ya Ziwa, ambako shughuli za
ufugaji wa samaki zinaendelea kukua.
Kwa upande
wake, mfugaji wa samaki kutoka Shirati mkoani Mara, Peter Mwera, alisema mfumo
huo unaweza kuongeza thamani katika ufugaji wa samaki kwa kupunguza muda
unaotumika katika kuhesabu samaki na vifaranga kwa njia za kawaida.
“Tunaomba wabunifu wa mfumo huo kuusambaza maeneo mbalimbali ili ufahamike kwa wafugaji wa samaki,” alisema.
Mwera pia
aliwataka COSTECH na serikali kwa ujumla kuendelea kuwawezesha wabunifu ili
tafiti na teknolojia zinazobuniwa nchini ziweze kuleta mabadiliko katika sekta
mbalimbali.
Mfugaji wa
samaki mkoani Mara, Cecelia Masaba, alisema mfumo huo unaweza kuwasaidia
wafugaji kupata uhakika wa idadi ya vifaranga wanavyonunua.
Watafiti kutoka SUA, Ally Abdi na Magoti Ndaro wakiwa kwenye banda lao.
...................................
“Kwa mfumo huu mpya wa kuhesabu vifaranga kwa njia ya AI, utaturahisishia kazi ya kujua idadi kamili ya vifaranga tunavyonunua,” alisema.
Masaba alisema kupata idadi sahihi ni muhimu kwa mfugaji kwa sababu kunamsaidia kukadiria gharama za chakula, huduma na mapato yanayotarajiwa.
Kwa mfano, alisema mfugaji anayetarajia kununua vifaranga 20,000 anahitaji kuwa na uhakika kwamba kweli amepokea idadi hiyo ili aweze kupanga kwa usahihi gharama za ulishaji na uzalishaji.
TEKNOLOJIA
YAIFUNGULIA TANZANIA MILANGO
Ushindi wa
AquaShield katika jukwaa la kimataifa la AI for Good Impact Awards 2026
umeongeza mwonekano wa ubunifu wa Tanzania katika matumizi ya Akili Unde
kutatua changamoto za sekta ya kilimo na ufugaji.
Kwa mtazamo
huo, utafiti wa Magoti unaonyesha namna ambavyo teknolojia inaweza kuunganisha
utafiti wa kisayansi na mahitaji halisi ya wafugaji, huku ukifungua fursa ya
Tanzania kujenga uwezo zaidi katika teknolojia za AI.
Kutoka
kwenye takwimu ambazo zamani zilihitaji tafiti, sampuli na wataalamu hadi
kwenye mfumo unaoweza kutumia kamera na Akili Unde kutoa taarifa kwa haraka,
sekta ya ufugaji samaki sasa inaingia katika hatua mpya ya matumizi ya
teknolojia.
Na kwa
Tanzania, safari hiyo inaweza kuwa mwanzo wa kutumia ubunifu wa ndani kutatua
changamoto za ndani na wakati huo huo kushindana kwenye majukwaa ya kimataifa.
Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990



No comments