Header Ads

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MIRADI YA UMWAGILIAJI, YATAKA WANANCHI KUCHANGIA ADA

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kutembelea mradi wa ujenzi wa umwagiliaji unaofanyika wilayani Mkalama Mko wa Singida, Oktoba 2, 2026. Wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika.

Na Mwandishi Wetu, Singida

Kasi ya ujenzi wa miradi ya umwagiliaji imeiridhisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara ya kamati hiyo mkoani Singida, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, amesema wameridhika na kasi ya ujenzi wa miradi hiyo.

Mwanyika amesema, kutokana na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya miradi ya umwagiliaji inavyoendelea, kamati itaenda kulieleza Bunge na kutoa msukumo kwa Serikali ili iweze kutoa fedha na miradi hiyo kukamilika kwa wakati.

“Hatuna la kusema ‘Tumeridhika’ na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, tutaenda kuwapigania Bungeni. Tumepata nguvu ya kwenda kuwaombea fedha ili miradi hii mizuri inayogusa maisha ya mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla iweze kukamilika,” amesema.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo na wanachangia ada ya huduma za umwagiliaji.

“Wananchi, huu mradi ni wetu. Uendelevu wa fedha kuja hapa ni wa kudumu. Kwa miongozo ya Wizara chini ya sheria ambazo zinasimamiwa na Bunge, hii ada ni muhimu sana tulipe ili maboresho ya kazi iliyofanyika, ikiwemo mifereji, yaweze kuwa ya kudumu,” amesema.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Umwagiliaji na Zana za Kilimo), Athuman Kilundumya, amesema ziara hiyo imekuwa na tija na Wizara imeona Kamati hiyo ilivyo na nia ya kuijua miradi ya umwagiliaji, huku Serikali ikiwa tayari kusimamia maelekezo ya Bunge.

“Mmeona ubora wa kazi zilizofanyika na miradi mliyotembelea. Baadhi inatekelezwa na wakandarasi wa ndani na Tume imekuwa ikiisimamia ipasavyo kwa kushirikiana na Wizara ili kuweza kupata thamani ya fedha,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, ameihakikishia Kamati hiyo ya Bunge kuwa ujenzi wa miradi ya umwagiliaji unaenda kwa kasi na utaendelea kuleta tabasamu kwa wananchi.

“Miradi ya umwagiliaji inakwenda kwa kasi na itaacha tabasamu kwa wananchi kama Rais alivyoelekeza. Tume tumefarijika na ujio wenu na tutahakikisha mnatembelea miradi mingine,” amesema.

Amesema miradi inayotekelezwa ni zaidi ya 146 na kati ya hiyo, asilimia 70 ya wakandarasi wake ni Watanzania, hivyo Tume inatekeleza kwa asilimia 100 lengo la Serikali la kuwezesha wakandarasi wazawa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia Messos, amewataka wananchi wanaonufaika na miradi ya umwagiliaji kuacha kuuza maeneo ili kufikia lengo la Serikali, huku akisisitiza kuwa halmashauri hiyo imeanza kupima maeneo husika ili kupata mpango bora wa matumizi ya ardhi.

Amesema tayari wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 200 na kupata hati za kimila 900.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika akizungumza.


Mhandisi wa Mradi huo, Fanuel Mrema akielezea utekelezaji wa mradi huo kwa Kamati ya Bunge,


Mhandisi Ilema Ramadhani (kulia), akitoa maelezo ya mradi huo mbele ya kamati ya bunge.
Mwananchi anayeishi jirani ya mradi huo akiishukuru Serikali kwa kufanikisha mradi huo katika Wilaya ya Mkalama.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Asia Juma Messos, akizungumzia mradi huo.
Viongozi na wajumbe wa kamati ya Bunge wakitoka kutembelea mradi huo
Muonekano wa sehemu ya mradi huo.
............................................

Habari hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale Simu namba 0754362990
 

No comments

Powered by Blogger.