HISTORIA FUPI YA MTI WA MATUNDA YAFAMIKAYO KAMA MAPERA
....................................
Na Mwandishi Wetu
MTI wa mpera ni miongoni mwa miti ya matunda inayofahamika na wengi hapa
nchini.
Mti huu hutoa matunda yanayofahamika kama mapera. Asili ya mti huu ni
Amerika ya Kati na Kusini licha ya kuwa siku hizi unapatikana sehemu mbalimbali
nchini na duniani kote.
Mmea huo kama ilivyo mimea mingine ya matunda, hustawi zaidi katika hali ya
hewa ya kitropiki. Hapa nchini Tanzania mti huu unasadikika uliletwa na
wakoloni waliotoka mashariki ya mbali waliokuja Afrika kwa madhumuni mbalimbali
ikiwemo suala la kueneza dini ya Kiislamu na Kikristo.
Mapera ni miongoni mwa matunda yenye kiwango kizuri cha vitamin C pamoja na
vitamin A na inaelezwa kuwa kiwango cha vitamin C kinachopatikana ndani ya pera
ni mara nne ya kiwango cha vitamin hiyo kinachopatikana kwenye chungwa.
Pia mapera yamesheheni virutubisho mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitamin
B2, E na K pamoja na madini ya chuma, ‘copper’, ‘potassium’ na ‘manganese.’
Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kuchapishwa na Jarida la Journal of Human
Hypertension mwaka 1993 ulieleza kuwa tunda aina ya pera hupunguza kiwango cha
msukumo mkubwa wa damu ndani ya mwili yaani 'High Blood Pressure' hii ni kwa
sababu ya madini ya potassium na vitamin C ambayo husaidia kuweka sawa msukumo
wa damu ndani ya mwili.
Faida haziishii kwenye tunda pekee, bali hata majani ya mti wake
yanapoandaliwa vizuri huweza kuwa tiba ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja
na malaria. Majani ya mpera yanapoandaliwa kama chai, yaani yakichemshwa
husaidia kuondosha sumu ndani ya mwili 'cholesterol' jambo ambalo husaidia
kulinda afya ya moyo wako pia.
Majani hayo hayo ya mpera pia huwasaidia wale wenye matatizo ya kuharisha,
ili kukabiliana na tatizo hilo mgonjwa wa kuhara huweza kuandaliwa maji
yatokanayo na majani ya mpera ambayo yamechemshwa na kunywa kikombe kimoja asubuhi
na jioni.
Vilevile majani ya mpera husaidia kutibu tatizo la vidonda vya tumbo, huku
likiwa na virutubisho vingi ambavyo husaidia kuimarisha fizi na kuongeza
vitamin B na A mwilini.
Majani ya mpera yenye uzito wa kilo moja yanapopondwa na kisha mgonjwa
akanywa lita moja ndani ya siku nzima husaidia kukinga seli za mwili dhidi ya
magonjwa mbalimbali.
Majani mateke ya mti huo yanapofungwa shingoni kwa mwenye tezi huweza
kuponyesha tatizo hilo pia na mwenye jipu akifunga sehemu husika hulifanya jipu
kuiva kwa haraka.
Pamoja na majani hayo kuwa msaada wa kutibu maradhi mbalimbali ,
halikadhalika juisi ya mapera nayo husaidia sana kutibu mgolo au bawasiri, figo
na hata kuondoa mafuta katika moyo.
Kimsingi mti wa mpera karibu kila sehemu yake ni tiba kwani hata mizizi
yake inapochemshwa na kutumia kwa kunywa huenda kuwasaidia wanawake wenye
matatizo ya hedhi au wenye matatizo ya kutokwa na maji yenye harufu mbaya
sehemu zao za siri.
Sanjari na hayo, watoto wadogo wenye matatizo ya kutopata choo zaidi ya siku
mbili, wakinyweshwa maji ya majani hayo baada ya kuchemshwa huwasaidia
kuondokana na shida hiyo, lakini ni vyema kuwasiliana na wataalam wa tiba asili
kabla ya kuamua kutumia majani hayo kama tiba kwa mtoto.



No comments