KILIMO BORA CHA MPUNGA WA NCHI KAVU
.........................................
MPUNGA ni miongoni mwa zao muhimu la chakula nchini Tanzania. Uzalishaji wa
mchele nchini kwa takwimu za mwaka 2016
ni zaidi ya tani milioni 2. Tija ya uzalishaji kwa mkulima ni wastani wa tani
1.5 -2.5 wakati katika skimu za umwagiliaji uzalishaji unaweza kufikia hadi
tani 6 kwa hekta moja.
Kilimo kilichozoeleka sana cha mpunga ni kile cha mabondeni ambapo
kinahitaji maji mengi. Katika zama hizi za mabadiliko ya tabianchi ambapo
kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mvua na maji kwa ajili ya shughuli
za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kilimo cha umwagiliaji, ni muda
muafaka kuanza kuhimiza kilimo kinachotumia maji kwa ufanisi hususan kutumia
mbegu za mpunga wa nchi kavu. Aina ya mbegu za mpunga wa nchi kavu ni fursa kwa
wakulima wengi zaidi kuzalisha mpunga bila kulazimika kuhitaji maeneo
yaliyozoeleka ya mabondeni.
Kilimo mpunga wan chi kavu ni kilimo gani? Bwana Johnson Tillya ambaye ni Afisa kilimo wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) anasema kuwa, kilimo cha mpunga wan chi kavu ni kile kinacholimwa maeneo yasiyo ya mabonde, na kinachotegemea mvua. Ni kilimo kinachoweza kulimwa sawa na maeneo yanayolimwa mahindi, kwa kifupi ni mpunga wa aina hii hauhitaji maji mengi.
Katika kuhimiza kilimo cha mpunga cha nchi kavu, ASA imeanzisha mashamba
darasa kwa ajili ya kutambulisha kilimo cha mpunga wa nchi kavu. Mashamba
darasa hayo yalitanguliwa na Mafunzo ya wakulima viongozi pamoja na wataalam wa
kilimo yaliyofanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Wakulima cha Mkindo.
Wakulima viongozi waliohudhuria mafunzo hayo walipewa malengo ya kuanzisha
vikundi vya wakulima katika vijiji walivyotoka ambao watalitakiwa kuwahamasisha
kuanzisha mashamba ya vikundi ambayo yatatumika kama mashamba darasa ya
kuwafundishia wana kikundi na wakulima wengine.
Jukumu jingine la kila mwanakikundi baada ya kupata mafunzo katika shamba
darasa ilikuwa ni kueneza elimu waliyoipata kwa angalau wakulima wengine
watano. Kupitia utaratibu huo wakulima
wengi zaidi wanaweza kufikiwa kwa kupewa elimu ya kilimo bora cha mpunga wan
chi kavu kupitia wakulima wenzao waliokwishapatiwa mafunzo kama hayo awali.
Katika mpango huu wa kuhimiza kilimo bora cha mpungu wa nchi kavu, ASA
imekuwa na jukumu la kutoa mbegu na Kampuni ya Mbolea Tanzania ilitoa mbolea
kwa kila kikundi.
Mbegu za nchi kavu za mpunga ni zipi? Bwana Tillya alisema mbegu zilizosambazwa kwa wakulima ni NERICA 1, NERICA 2, NERICA 4 na NERICA 7. Sifa za uzaaji wa aina za mpungu wa nchi kavu ni zipi? Bwana John Teofili, mkulima mwezeshaji wa kijiji cha Tawa alizitaja aina za mbegu za mpunga za nchi kavu na uwezo wake wa kuzaa kama ifuatavyo: NETICA 1 ina uwezo wa kutoa mavuno kilo 1,800 kwa eka, NERICA 2 kilo 1,600 kwa eka, NERICA 4 kilo 2,000 kwa eka, na NERICA 7 kilo 2,000 kwa eka.
Katika ziara ya kutembelea vikundi vya wakulima vinavyoendesha majaribio ya
kilimo cha mpunga wa nchi kavu, vijiji vya Kiloka, Tawa, Kisaki na Dala
vilitembelewa. Vijiji hivyo vinapatikana Morogoro vijijini katika safu za
Milima ya Ulugulu. Msafara huo ulijumuisha Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Morogoro Vijijini, Mkoa wa Morogoro, Wakala wa Mbegu za Kilimo na Wizara ya
Kilimo Mifugo na Uvuvi. Aidha, Waandishi wa habari wa baadhi ya vyombo vya
habari walishiriki ziara hiyo ili kuona mafanikio yaliyopatikana katika
kuendesha majaribio ya aina ya mpunga wan chi kavu.
Ziara hiyo ilihitimishwa na Siku ya Wakulima ya tarehe 1 Juni, 2017 iliyofanyika katika
kijiji cha Mtamba, kata ya Mtamba, Tarafa ya Matombo, wilaya ya Morogoro
Vijijini.
Source : Wizara Ya Kilimo


No comments