WAKULIMA KIGOMA WAVUTIWA NA MBEGU ZA MAJARIBIO ZA KARANGA KUTOKA TARI
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mbegu za majaribio za zao la karanga zilizopelekwa mkoani Kigoma zimewavutia wakulima wengi kutokana na uotaji wake ambao umeonyesha kutokuwa na magonjwa na kustahilimi ukame.
Akizungumza na watafiti wa zao hilo hivi karibuni, Asia Nobela Mkulima wa Karanga kutoka katika Kijiji cha Mahembe halmashauri ya wilaya ya Kigoma alisema kuwa mbegu hizo ziliota haraka na kuwa na mwonekano mzuri shambani uliowavutia wakulima wengi na kuomba mbegu hizo.
“Kwanza ukipanda zinaota haraka hazina magonjwa ukipanda kitaalamu zinakaa kwa mstari hivyo kuwa na mwonekano mzuri shambani na pia zinakidhi mahitaji ya soko wanunuzi wengi wakiziona wanazitaka tunaomba tuongezewe mbegu ili tulime kwa wingi zaidi”
Nae Tatu Mwimo Afisa Kilimo Kata ya Mwanandiga alisema kuwa tuliletewa mbegu za majaribio ambapo kupitia mashamba darasa ambayo yamejumuisha wakulima wengi zaidi wa zao la karanga ambapo wamejifunza namna bora ya kulima karanga.
“Wakulima wengi waliitikia na kulima kulingana na mwongozo wa watalaamu kwakweli tumeona matokeo naamini kuwa hawa wachache watakuwa mabalozi wa wakulima wengine wa zao hilo” alisema Mwimo.
Kwa upande wake Mtafiti wa zao la Karanga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Naliendele Juma Mfaume alisema kuwa jitihada mbalimbali zinafanywa na kituo hicho ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima wengi wa zao hilo waweze kuongeza uzalishaji.
“Tumetoa mbegu kwaajili ya majaribio ambapo zimeenda kwa wakulima wa vijiji mbalimbali nchini ikiwemo vijiji vya Mahembe, Mwandiga na Kaganza ambapo tunafanya tafiti shirikishi katika mikoa hiyo ili kubaini ipi mbegu bora itakayowafaa wakulima wa zao la karanga ndani ya Wilaya hiyo” alisema Mfaume



No comments