Header Ads

FAHAMU SABABU YA KAKAO YA TANZANIA KUTOTUMIKA NYUMBANI

 

Muonekano wa zao la Kakao

.................................

Na Esther Namuhisa & Eagan Salla

'COCOA ni pesa kwangu, nikivuna napeleka kuuza, sijawahi kula chokoleti katika maisha yangu na kwanza hakuna hapa, tumezoea tangu enzi za mababu tunauza tu cocoa,' Simon ni mkulima kakao kutoka wilayani Kyela, mkoani Mbeya, nchini Tanzania. 

Mfumo wa kupeleka malighafi nje ya nchi bado uko vilevile tangu zao hili lianze wakati wa ukoloni. 

Wakulima hapa wanasema mashamba yao ya kakao wamerithi kutoka kwa babu zao. 

Utaratibu wa vyama vya ushirika uliowekwa na serikali bado unatumika. 

"Mkulima anakuja kuacha mzigo wake siku ya Alhamisi tunampa risiti tukisubiri siku ya mnada Jumatatu. 

Hakuna kiwanda cha kakao hapa, wateja wanakuja kununua na kusafirisha na hivyo ndivyo tumekuwa tunafanya biashara hii miaka yote. 

Tunatamani bidhaa yetu ya kakao iwe na nembo ya kyela badala ya kuuza malighafi kama tunavyouza lakini tunasubiri serikali ichukue hatua, mratibu wa chama cha ushirika wilayani Kyela aliiambia BBC. 

Ni kawaida kukuta mazao ya biashara kuwa na mashamba makubwa lakini hali ni tofauti kwa zao hili la cocoa ambalo linahesabika kuwa zao la kibiashara kwa miongo kadhaa. 

Miti ya cocoa yaani kakao ipo pembezoni mwa nyumba, karibu kila nyumba wilayani Kyela ina miti ya kakao. 

Kwa mfano kahawa huwa inalimwa pembezoni mwa nyumba pia lakini kuna mashamba maalum kwa ajili ya kilimo hicho. 

Kakao imeanza kulimwa nchini Tanzania mnamo miaka ya 1950, katika mikoa ya Morogoro, Tanga na Mbeya. 

Kilimo hiki kikiwa kinachangia pato la uchumi wa kilimo nchini humo. 

Tanzania ikiwa inategemea kilimo katika uchumi wake, sekta hii inatoa ajira kwa tatu ya nne ya idadi ya watu wa taifa hilo. 

Kwa mujibu wa utafiti wa Repoa, asilimia 80 ya kilimo cha kakao kinafanyika wilaya moja tu ya Kyela, mkoani Mbeya. 

kakao

Na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa ambayo yanazalisha kakao nzuri ya kipekee duniani na ikiwa ya asili na hivyo kuvutia soko kubwa la chokoleti duniani. 

Ally Jumbe ni Mbunge wa Kyela anasema; 

"Sisi cocoa hailimwi mashambani, ni zao ambalo lipo kwenye nyumba zetu na sio kwenye mashamba ya porini. 

Kila mtu katika nyumba hapa kuna miti ya cocoa, ni zao ambalo linatupa uchumi tunaoutegemea sana hapa, ndio maana tunaiita dhahabu ya kijani. 

Zao letu ni la zamani na lilianza zamani sana, lakini katika uzalishaji bado huwezi kutulinganisha na Ivory Coast, Ghana, Brazil kwa sababu wao wana cocoa nyingi na sisi tunayo kidogo lakini tuna kitu kimoja kikubwa katika cocoa yetu, ni kuwa cocoa yetu ni kipekee ya asili yaani organic ambayo haitumii dawa kuikuza",bwana Jumbe amefafanua. 

Anasema wanunuzi wengi wanaokuja kununua kakao hapo huwa wanasema wananunua ili kuzibulia cocoa nyingine. 

Aidha amesema ubora wa kakao ya Kyela ndio imepelekea zao hilo kuwa katika soko la dunia. 

Kama ni zao bora je kwanini haliendelezwi?

Muonekano wa kakao

Ally Jumbe anasema kwa kiwango kidogo kilichopo, si rahisi kwa muwekezaji kuja kuwekeza kwa kuweka kiwanda ndio maana mpaka sasa hakuna kiwanda, wala uendelezaji wa mashamba, kwa kuwa mashamba yanamilikiwa na wananchi katika nyumba zao. 

"Ila kuna matumaini kuwa siku zijazo tutaweza kuanza hata hatua za awali za uzalishaji. 

Mimi ndoto yangu ni kuongeza thamani katika cocoa ya kyela, si kwenye chakula peke yake bali kwenye pombe pia. 

Cocoa nyingi ni ya kurithi ndio maana walimaji ni wachache ingawa serikali ina mpango endelevu kwa vijana kupewa miche ya kakao hivyo miaka michache ijayo hali itakuwa tofauti.

 

Na mpango huo utaweza kusaidia kuanza kufanya uzalishaji mkubwa na hivyo kiwanda kinaweza kutengenezwa,"Jumbe ameeleza. 

Wakulima wanasemaje kuhusu kilimo hiki

Wakulima wengi ambao BBC ilizungumza nao walikuwa wanafurahia kupata pesa za kila wakati kutoka kwa zao hilo la cocoa, pesa ambazo zinawasaidia kununua bidhaa ndogondogo katika eneo hilo.

 

"Huwezi kufa na njaa Kyela, ukimiliki shamba la kakao ni ela" mkulima Shaban Namlike ambaye ni mwalimu pia. 

Anasema yeye aliweza kusoma shule binafsi kwasababu ya kakao na alivyopata ajira tu ilimbidi aanzishe mradi wa kakao maana anajua thamani yake. 

Wakati Jenoramu Kayeka , yeye anasema yeye ana hekari nne za zao la Cocoa. Anasema ukiachilia kuwa kila mtu analima kakao kyela ila hawajui cocoa inatumika kwa ajili gani, yeye anaweza kusoma akaelewa ila anaweza kuwa mmoja kati ya wakulima 200. 

Bwana Kanyika anasema Kilimo cha kakao ni kizuri lakini kina matatizo yake, Kwa miaka minne mapaka saba kunakuwa na uzalishaji mkubwa lakini kadri miaka inavyokwenda athari tunaanza kuziona na mabwana shamba bado hawapo karibu na sisi.

 

Hakuna mweye miche ya kakao ambayo ina miaka 12 bila uzalishaji kushuka.

 

Anasema , mkulima tegemeo lake kubwa ni cocoa na mara nyingine ubora unapungua kwasababu wengi wanalima ili wapate ela kwa haraka na kupata pesa ya kutumia nyumbani.

 

Hivyo soko linashuka kwasababu ya kukosa ufuatiliaji. Wazee wana ujuzi mkubwa zaidi kuliko vijana. 

Soko kubwa la kakao ya Kyela ni la nje ya nchi

Jones Mrusha ambaye ni mkulima na mfanyabiashara wa kakao anasema kikubwa kinachohitajika ni maandalizi na uelewa wa muda wa kuvuna na kuuza. 

Wengi wanauza kwasababu wanahitaji pesa hivyo muhimu kupata mafunzo kwa kuangalia ni wakati gani wanapaswa kufanya hivyo, yeye akiwa mfanyabiashara huwa anawashirikisha wakulima katika mafunzo ya kujua wakati gani haswa wa kuvuna. 

"Zao letu kimataifa lina soko kubwa , zaidi ya asilimia hamsini inauzwa nje ya nchi.

Hii inaweza kuwa hatari maana soko la kimataifa likiyumba kwetu katika kusafirisha basi uchumi wa Kyela utashuka. 

Ukilinganisha na kakao yetu na mataifa mengine, ubora wake ni mzuri ingawa mauzo ya mnada yanapoteza ufuatiliaji wa zao hilo kutoka shambani mpaka kwa mlaji. 

Na ili kupata cheti kuwa tuna zao organic ni lazima kuzingatia utarabu wa kimataifa. 

Kwa uzuri katika eneo la kyela na tukuyu wanatumia samadi ambayo ni ya asili na hawatumii dawa sana," Mrusha ameeleza. 

Unaweza kukuta dawa imetumika mara moja katika miaka 10 kama uvamizi wa wadudu umetokea na kuna miti ambayo ina miaka mingi katika nyumba za watu mbalimbali, ndio maana wanasema wamerithi.

Taarifa hii ni kwa hisani ya Nafasi,BBC Swahili

No comments

Powered by Blogger.