MBUNGE WA JIMBO LA MLALO AKUTANA NA WAKULIMA WA MKONGE KUTATUA CHANGAMOTO ZAO
....................................
Na Mwandishi Wetu, Lushoto
Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashid Shangazi (MNEC) leo amekutana na Chama
Cha Ushirika wa zao la Mkonge Umba (UWAMU) akiambatana na Mkurugenzi wa Bodi ya
Mkonge Tanzania Ndugu Saddy Kambona , Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika
Mkoa wa Tanga Ndugu Henjewele John pamoja na Viongozi wa Idara ya Kilimo
Halmashauri ya Lushoto walioongozwa na Ndugu George Medeye.
Mhe. Shangazi ameitisha kikao hicho kilichofanyika katika Shule ya Msingi
Kwezigha Kata ya Mnazi kwa lengo la
kutatua changamoto zilizowasilishwa kwake na wadau wa mkonge Tarafa ya Umba
hususani changamoto ya kukosekana mitambo ya kuchakata zao hilo ndani ya
Ushirika katika kuongezea thamani, hatua ambayo itakuwa ikiongeza kipato chao.
Viongozi wamezungumza mambo mbalimbali kama ifuatavyo:-
1) MHE. MBUNGE SHANGAZI: Ameanza kwa kumkaribisha sana Mkurugenzi wa Bodi
ya Mkonge Tanzania na kumshukuru kwa kukubali kufika Mnazi kupokea changamoto
za wakulima ili kuzitolea ufafanuzi na majawabu.
Mhe. Rashid Shangazi aliendelea kwa kutaka taarifa ya kitakwimu ya idadi ya
wakulima wa mkonge hadi sasa, ukubwa wa eneo la kilimo na hali ya uzalishaji
kwa mwaka.
Mhe. Shangazi ameelekeza takwimu hizo zihuishwe haraka iwezekanavyo na
kuhakikisha wakulima wa mkonge wanaingia katika Chama cha Ushirika kwa lengo la
kuwa na nguvu ya uzalishaji na uuzaji wa pamoja kwa faida.
Vilevile, ameonyesha wasiwasi wake juu ya uimara wa Ushirika huo na
kufahamishwa ni kweli Ushirika unakabiliwa na changamoto za uendeshaji hasa
upande wa michango ya viingilio na ununuaji wa hisa ambapo kila mwanachama
anapaswa kuwa na hisa 5 zenye thamani ya Shilingi 100,000/=.
Hii imepelekea Mhe. Mbunge kusimamia kuwekwa kwa maazimio yaliyoonekana mwisho wa taarifa hii.
2) MKURUGENZI WA BODI YA MKONGE TANZANIA:- Akizungumza katika Kikao hicho,
Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania ndugu Saddy Kambona amepongeza jitihada
za Mbunge wa Jimbo la Mlalo katika kutafuta namna ya kuwainua wakulima wa Mkonge.
Kambona amezungumzia hatua mbalimbali anazofanya kutafuta mwarobaini wa
changamoto za wakulima wadogo wadogo wa Mkonge. Jitihada hizo ni pamoja na:-
A) Imeundwa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo, vyuo vikuu, na
Kilimanjaro Tools kuzunguka nchi nzima kukagua teknolojia inayotumika katika
viwanda vya uchakataji wa Mkonge ili waunde mtambo wa bei nafuu wa kuchakata
zao hilo kuwawezesha wakulima wengi kununua.
B) Imeundwa timu ya wataalamu kukutana na watu wa Benki (Bankers) kuona
namna watakuja na utaratibu nafuu wa kuwakopesha wakulima wa mkonge kwa
masharti nafuu tofauti na wakopaji kutoka Sekta nyingine.
C) Bodi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeendelea kuhakikisha
wakulima wanauza Mkonge wao kwa Bei nzuri kwa kutafuta masoko ya uhakika.
Mkugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania ametaja fursa mbalimbali zilizoko
katika zao hilo akisema,
(a) Mkonge ni zao linalofanya vizuri sana Katika kunyonya hewa ya Ukaa,
hivyo inaangaliwa namna ya kuwanufaisha wakulima wa zao hilo kupitia Biashara
ya Hewa ya Ukaa.
(b) Mabaki ya Mkonge yanatumika kuzalisha mkaa wa kupikia.
(d) Mabaki ya Mkonge ya yanaweza kutumika kuzalisha mbao za kutengeneza
samani (furniture).
Mkurugenzi ameshuhidia mabaki ya
Mkonge katika Tafara ya Umba yakitupwa na kuchomwa moto, hivyo anafanya Kila
liwezekanalo kuhakikisha yanawapatia fedha wakulima.
Hata hivyo, Mkurugenzi Kambona amesema pamoja na kwamba katani inahimili
mazingira magumu na kame, ni muhimu mashamba ya zao hilo yatunzwe kwa kulimiwa
na kutochoma moto ili uzalishaji uongezeke. Amesema wenzetu China wanapata
mavuno makubwa karibu mara 4 zaidi ya Tanzania kwakuwa walima mashamba yao na
kuyatunza wakati wote wa ujuaji hadi hatua ya kuvuna.
Ameongeza kuwakumbusha wakulima kwamba uvunaji wa Mkonge ufanyike Kila
baada ya mwaka 1 badala ya uvunaji unaoendelea sasa ambao majani yamesimama
wima hayasubiriwi yakitanua.
Aidha, wakulima wa Mkonge wameaswa kuzivumilia changamoto za sasa za
uzalishaji wa zao hilo akisema kupitia mipango na jitihada zinazofanywa na Bodi
ya Mkonge na Wizara ya Kilimo ni dhahiri mazuri yanakuja hivi karibuni kwani
maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Kilimo kiinakuwa
na tija kwa Mkulima na Taifa.
3) MRAJISI MSAIDIZI WA VYAMA VYA USHIRIKA TANZANIA:- Ndugu Henjewele wakati akitoa mafunzo kwa wakulima na kueleza faida za Vyama vya Ushirika amesema Chama cha Ushirika kinaundwa na ngazi tatu ambazo ni:-
1. Wanachama,
2. Bodi ya uongozi - yenye wajumbe kuanzia 5 hadi 9 wanaotokana na
wanachama hao, na
3. Watendaji - ambao wanaaajiriwa na Bodi.
Kama Ushirika ukiyumba ni matokeao ya Malindi yayo matatu kutotimiza wajibu wake ipasavyo.
Ndugu Henjewele alewela wazi utayari wake kurudi tena Tarafa ya Umba kutoa
Elimu zaidi kwa wakulima katika Ushirika wa UWAMU.
4) AFISA KILIMO WA HALMASHAURI (W) LUSHOTO:- Afisa Kilimo wa Halmashauri ya
Wilaya ya Lushoto ndugu George Medeye amesema uzalishaji wa zao la Mkonge
katika Tarafa ya Umba unaongezeka kwa kasi kubwa sana kwa kila mwaka kwani
mwaka uliopita 2023 uzalishaji ulikuwa zaidi ya Tani 1,200 wakati mwaka huu
2024 matarajio ni kuvuna zaidi ya kiasi
hicho ikizingatiwa kwamba kufikia mwaka 2024 Mkonge uliofikia hatua ya kuvunwa
ni Hekta 2,000 sawa na Ekari 5,000.
Ameongeza kusema idadi ya wakulima wa Mkonge mwaka 2023 ilikuwa 500,
takwimu zitakazokusanywa mwaka huu zitakuwa na ongezeko kubwa sana.
Medeye ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote ya Mkurugenzi wa Bodi ya
Mkonge Tanzania, Mhe. Shangazi pamoja na Viongozi wengine kuhakikisha baada ya
muda mfupi Mkonge unawatajirisha wakulima.
5) MENEJA BENKI YA CRDB LUSHOTO:- Meneja wa Benki ya CRDB ndugu John Mtani
amezungumza na wakulima katika Ushirika wa Mkonge UWAMU kuwatangazia fursa
mbalimbali zinazopatikana katika Benki yao akitolea mfano wa huduma za mikopo
ya Fahari Kilimo na Imbeju.
Mtani amesema sifa mojawapo ya Ushirika kukopeshwa na Benki ya CRDB ni kuwa
na Akaunti ya Benki hiyo.
Ameendelea kusema Benki ya CRDB inatoa fursa kwa wakulima kufungua Akaunti
ambazo hazina gharama ya uendeshaji. Hivyo CRDB ni Benki inayojali Malindi
mbalimbali bila kusahau wakulima wa Mkonge.
6) MAKAMU M/KITI WA UWAMU:- Ndugu Abdallah Kumbi ameeleza furaha yake
kutokana na yote yaliyowasilishwa na Mhe. Rashid Shangazi Mbunge, Mkurugenzi wa
Bodi ya Mkonge Tanzania, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tanga, pamoja na
Viongozi wengine akisema awali alikuwa akiwalaumi viongozi hao kwakuwa alikuwa
anakosa taarifa sahihi na mipango mizuri iliyowasilishwa katika kikao.
Ndugu Kumbi Abdallah ameahidi kutoa ushirikiano kwa Mhe. Mbunge na viongozi
wote kuelekea katika mabadiliko makubwa ya Ushirika na Uzalishaji wa Mkonge.
7) MENEJA WA UWAMU:- Ndugu Bakari Huseni Sefu amesema ushirika wa UWAMU
umepata nafasi kutembelea vyama vya Ushirika wa Mkonge Magoma - Korogwe na
kubaini wenzao wakiwa na mafanikio Makubwa sana kiasi cha kuuaga umasikini.
MAAZIMIO YA KIKAO:
Miongoni mwa maazimio ya kikao ni pamoja na:-
(1) Kila mwanachama wa UWAMU akamilishe malipo ya Tsh. 10,000/= ya
kiingilio cha kujiunga na Chama kabla ya Desemba 2024.
(2) Kufungua Akaunti katika Bank ya CRDB kwa ajili ya kuongeza wigo wa
kukopesheka.
(3) Kukamilisha taarifa ya sasa ya idadi ya wakulima wa Mkonge, idadi ya
Hekta zinazolimwa Mkonge na kiasi cha uzalishaji kwa mwaka.
(4) Kila Afisa Ugani katika Tarafa ya Umba awe anajishughulisha na Kilimo
cha Mkonge kama shamba darasa kwa wengine na awasilishe ripoti ya uzalishaji
wake.
(5) Afisa Kilimo Wilaya afuatilie swala la mashine ya kuchakata Mkonge kwa
mwekezaji aliyeahidi kusaidia mashine moja.
(6) Afisa Kilimo Wilaya aandike andiko kwenda kwa Mkurugenzi wa Stakabadhi
Ghalani kuomba ghala la kuhifadhia Mkonge (Warehouse) Tarafa ya Umba.
(7) Afisa Kilimo Wilaya ashirikiane na Diwani wa Mnazi kutafuta eneo la
Ghala la Mkonge ndani ya Kata ya Mnazi.
(8) Ushirika wa UWAMU Kufanya mkutano kila baada ya miezi 03 badala ya
Mkutano 01 unaoelekezwa kwa mujibu wa Sheria. Lengo ni kuharakisha kuimarika
kwa Ushirika huo na utekelezaji wa haraka wa maazimio. Hivyo kutakuwa na kikao
mwezi Desemba, 2024.
Mhe. Mbunge amehitimisha kwa kumshukuru Mkurugenzi wa Bodi ya Mkonge
Tanzania ndugu Saddy Kambona kwa utayari wake mkubwa kuwasaidia wakulima wa
Mkonge Kupitia Chama cha Ushirika UWAMU.
Vilevile, Mhe. Mbunge amewashukuru wakulima wa Mkonge kwa kushiriki kikao
hicho kuwasilisha kero zao na kupokea
yale yaliyowasilishwa na viongozi kutoka juu.
Kubwa zaidi, Mhe. Rashid Shangazi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa uhai mkubwa Wizara ya Kilimo
katika uzalishaji na masoko chini ya Waziri wake Mhe. Hussein Bashe.
No comments