WAZIRI WA KILIMO APIGA MARUFUKU WAFANYABIASHARA KUNUNUA KAHAWA KWA NJIA YA KANGOMBA
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Ruvuma akikagua mashamba ya kuchakata kahawa.
........................
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe (mb) amepiga marufuku wafanyabiashara
wanaonunua kahawa kwa njia ya Kangomba na kuagiza wakamatwe huku akisisitiza
kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa katika zao hilo umelenga kuteka soko la kahawa ya Tanzania kimataifa.
Amesisitiza kuwa serikali kwa sasa inawekeza katika kahawa kwa kugawa miche
na mbolea ya ruzuku hivyo,anatarajia kupigwa vita na wafanyabiashara kutokana
na kukemea kangomba lakini hatarudi nyuma kwa maslahi ya zao hilo.
Waziri Bashe amesema hayo katika muendelezo wa ziara yake Mkoani Ruvuma
mara baada ya kutembelea mashamba, viwanda vya kuchakata kahawa na skimu za umwagiliaji wilayani Mbinga na
Nyasa.
“Najua haya maamuzi yatakuwa na maumivu na yatakuwa na kelele, mimi kelele
nimezoea, kamateni wanaonunu kahawa kwa kangomba,”amesema.
Amesema, anatarajia vita kubwa dhidi ya wafanyabiashara wanaonunua kahawa
kwa njia ya Kangomba na hatarudi nyuma.
“Tutegemee kelele nyingi kutoka kwa
wafanyabiashara lakini sipo tayari kuona kangomba katika kahawa.Kelele zitakuwa
nyingi watapitishia kwa wakulima tujiandae lakini nasema ili kufikia soko la
kimataifa hatuwezi kuvumilia ununuzi usiofaa,”amesema.
Amesisitiza kuwa, hatua ya serikali kuwekeza katika zao hilo, imelenga
kuijengea ubora kahawa ya Tanzania kimataifa na kunufaisha wakulima.
“Tunatoa mbolea na miche kwa ruzuku na kuwezesha kilimo hiki kuhimili
ushindani dhidi ya kahawa za nchi nyingine,”amesema.
Akiwa katika miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa na Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji Waziri Bashe amesema“Nimejionea kiwango cha umasikini wa watu wetu
hapo mambo tumeanza kuyafanyia
kazi.Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hasan kwa kutupatia fedha
mwaka huu, nimemwambia Mbunge Injinia Stella Manyanya, tutafanyia kazi changamoto
za watu wetu.
“Tumeshatangaza na tumeshapata mkandarasi kwa skimu zenye hekta 8395
tutajenga barabara za ndani ya shamba,
madaraja na vigawa maji ndani ya shamba na usanifu umeshakamilika na mkandarasi
amepatikana”,amesema Waziri Bashe.
Pia Waziri Bashe ameitaka,kufanya usanifu na kuziingiza barabara za Lipingo
katika mpango wa utekeleza wa mradi huo wa Umwagiliaji.
“Nimegiza Tume ifanye usanifu, waingize kwenye mradi barabara zote mbili
hapa Tume inatekelez miradi ya zaidi ya Bilioni 25 kwa Wilaya ya Nyasa pekee haishindwi kujenga
hizo barabara zote,”amesema.
Aidha amesisitiza haja ya Skimu zilizopo katika Halmashauri ya Nyasa na
idadi ya skimu zitakazo anza kufanyiwa utekelezaji kwa haraka.
“Halmashauri ya nyasa kuna skimu nane na kwa kuanzia tutaanza kuzijenga
skimu mbili kuanzia mwaka huu wa fedha na ndani ya miaka 2 zote hizo zitakuwa
zimejengwa.Muwape ushirikiano wataalamu wanaotekeleza miradi”
“Pia Tume mfanye ujenzi wa ghala katika eneo la mradi na mashine ya kukoboa
mpunga ili wananchi waweze kuuza mchele
badala ya Mpunga,”amesema.
Ameongeza kuwa Wizara ina mpango wa kuanza kuzalisha wa mbegu karibu na
eneo la mradi wa Lundo katika kata ya Lipingo na kuanzisha vituo vya zana za
kilimo na kujenga kituo cha mbolea.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Manyanya, amesema Wilaya hiyo inahitaji
kukua kiuchumi na tegemeo kubwa ni kilimo cha mpunga hivyo wanatarajia miradi
ya umwagiliaji iwe chachu ya uzalishaji.








No comments