Header Ads

TFC YASAMBAZA MBOLEA TANI 100,000 MSIMU WA KILIMO WA 2024/ 2025

   Mkurugenzi  Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Bw. Samuel Mshote akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Machi 13, 2025 jijini Dar es Salaam.

................................

Dotto Mwaibale na Angelina Mganga

KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) katika kipindi cha msimu wa kilimo cha 2024/2025  imeweza kusambaza tani 100,000 za mbolea aina tofauti tofauti.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi  Mkuu wa kampuni hiyo,  Samuel Mshote wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Machi 13, 2025.

Alisema mbolea iliyosambazwa tani 30,000 ilikuwa kwa ajili ya kupandia, tani 25,000 ya kukuzia na kuwa wanaendelea kuipokea kutoka nje ya nchi pamoja na tani 15,000 aina ya UREA kwa ajili ya kunenepesha mazao. 

Mshote alisema TFC ni Taasisi ya Serikali inayojitegemea ambayo ilianzishwa mwaka 1968 chini ya Sheria ya Makampuni (Companies Ordinance CAP 212)

Alisema kampuni hiyo inatimiza malengo yake kwa kufanya kazi kwa misingi ya kibiashara na kuwa inafanya uwekeza ili iweze kupata faida na kuwa kazi yake kubwa ni kuzalisha mbolea na viatilifu.

Alisema malengo makuu ya kampuni hiyo ni kuzalisha mbolea, kuagiza kutoka nje ya nchi na kuwauzia wakulima wa ndani ili wapate mbolea iliyo bora na yenye kukidhi mahitaji.

Alitaja malengo mengine ya kampuni hiyo ni kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana katika kipindi chote cha mwaka na kwa bei nafuu. 

 “ Malengo mengine ni ya kimkakati ya kuhakikisha tunaingiza na kufunga kiwanda kwa ajili ya kuchanganya mbolea ambazo zitaendana na afya ya udongo ya maeneo tofauti tofauti ya nchi yetu ili kuweza kuwahudumia wakulima kuwapatia mbolea zinazoendana na afya ya udongo katika maeneo wanayolima ili kuongeza tija,” alisema Mshote.

Aidha, Mshote alisema wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazoweza kuleta maendeleo kupitia pembejeo, mbolea pamoja na madawa yake.

Mshote aliongeza kueleza kuwa kampuni hiyo pia inatoa huduma za pembejeo za mbolea kwa ajili ya zao la Tumbaku ambapo jumla ya tani 61,000 ya mbolea aina ya NPK 101824 zilipelekwa, tani 10,700 za CAN pamoja na UREA tani 2021.

Alisema  kwa kipindi chote cha usambazaji wa mbolea wameweza kusamba jumla ya tani 73,000 na kwenye mazao ya kawaida wamepeleka tani 75,000 na  kueleza kuwa kwa kampuni hiyo ni historia kwani hawajawahi kusambaza mbolea kwa kiasi hicho kwa wakulima wa kawaida na wa zao hilo la Tumbaku.

Mkurugenzi Mshote alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuifufua kampuni hiyo na kusaidia kupata uongozi kwa maama bodi ya ya Wakurugenzi, Menejimenti pamoja na kuiamini na kuwapatia mtaji wa fedha ili iweze kujiendesha kibiashara.

Alisema fedha hizo zimetolewa ili wakulima wapate mbolea na kufanya kilimo chenye tija na kuleta usalama wa chakula nchini lakini pia kutimiza malengo makubwa ya Serikali ya kilimo kichangie pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 20/30. 

Aidha, Mshote amemshukuru Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kwa kuwa nao bega kwa bega na kutoa miongozo mbalimbali, ushauri na maelekezo ya namna gani yakufanya kazi kwa ubunifu na kuweza kuwafikia wakulima wengi na kupata mbolea na viatilifu na kuvisambaza kote nchini kwa weledi na ubora wa hali ya juu.

“ Tuna muhakikishia waziri wetu kuwa TFC  inafanya vizuri kazi na inalinda fedha za umma na inapata faida na kuweza kujiendesha kibiashara,” alisema Mshote.

Akielezea hali ya usambazaji wa mbolea alisema kampuni inaisambaza nchi nzima kupitia maghala , vituo vya mauzo na kuwa kuna maeneo wana maghala yenye uwezo  wa kuhifadhi mbolea hadi tani 100,000.

Alisema maghala hayo Mkoa wa Mwanza (Mjini) ,Mbeya (Mbalizi), Sumbawanga, Njombe, Makambako, Ruvuma, Songea na  Tunduma.

 Pia alisema kuwa wana jumla ya mawakala 600,000 ambao wanatumika kusambaza mbolea za Ruzuku za Serikali pamoja na  kusajili vyama 29 vya ushirika kwa ajili ya kusambaza mbolea kwa wakulima.

Alisema mahitaji makubwa ya mbolea yapo  katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Mbeya, Songwe, Makambako, Iringa, Morogoro, Songea na Sumbawanga.

Alisema matumizi ya mbolea kwenye kilimo yameongezeka kutoka tani 360,000 hadi kufikia tani 800,000  kwa mbolea zinazosambazwa kwa ruzuku za serikali.

Mkurugenzi  Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Samwel Mshote akisisitiza jambo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.
Wanahabari wakiwajibika wakati wa mahojiano hayo.
 

No comments

Powered by Blogger.