WADAU WA KILIMO WAIOMBA SERIKALI KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAFUNZO YA KURUSHA DRONE, MALIPO YA LESENI KWA MWAKA
Na
Dotto Mwaibale, Dar es Salaam.
KILIMO
drone ni dhana mpya katika zama hizi, ambapo mkulima anaweza kulima mashamba
yake, kunyunyizia madawa na kubeba mazao yake kwa kutumia teknolojia hiyo ya kisasa ya drone.
Lakini
pamoja na mambo mengine katika kuendesha kilimo drone yanahitajika mafunzo ya
kuzitumia jambo ambalo ni la msingi tukizingatia kuwa teknolojia hiyo imetoka
nje ya nchi na kwa hapa nyumbani Tanzania ni ngeni.
Kutokana na umuhimu wa kilimo drone kila mtu
mwenye uwezo amekuwa na matamanio ya kufanya kilimo hicho lakini changamoto
kubwa iliyopo ni namna ya kupata na kumiliki drone ambayo kuipata kwake
kumekuwa na masharti mengi.
Kufuatia
changamoto hiyo baadhi ya wadau wa kilimo wanaiomba na kuishauri Serikali
iangalie namna ya kupunguza gharama hizo zikiwepo za utoaji wa mafunzo .
Hivi karibuni Serikali imetangaza kutoa mafunzo kwa
watanzania ambao watakuwa tayari kujifunza matumizi ya drone lakini kwa gharama
ya Sh. Milioni 1.4 kwa mwezi fedha ambazo ni nyingi.
“ Sio kila mtanzania hasa vijana wanauwezo wa kulipia milioni moja na laki nne kwa mafunzo hayo ya mwezi,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Jitu Son.
Son aliomba pia iangaliwe namna pia ya kutoa
mafunzo kwa waalimu wa Vyuo vya ufundi stadi VETA ili wao wawe na dhamana ya kutoa mafunzo kwa makundi mengine hasa ya vijana.
Alisema VETA wanaweza kutoa mafunzo hayo sio kwa ajili ya urubani wa waendesha drone tu bali wakaongeza masuala mengine kama upimaji na uchoraji (mapping ) , kufanya service na matengenezo madogo madogo (service and maintenance) ya drone na pia kuongeza ujuzi wa kupulizia dawa , mbolea na mbegu aina mbali mbali katika kilimo na hata kuwashirikisha wauza pembejeo, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania ,(TPHPA) na wauzaji wa Drones.
Son aliongeza kuwa kuna vijana waliomaliza VETA kozi ya Agromechanics wamepata uzoefu wa kurusha drone ya kilimo , kufanya service , kufanya upimaji na wako vizuri na wana ajira za muda katika kampuni za wenye huduma za drone kupiga dawa na mbolea.
Alisemma changamoto yao kubwa wanapata shida ya kutokuwa na leseni ambayo inatakiwa kulipiwa kila mwaka.
"Kampuni inawataka vijana hao wawe na mkataba ili wawabane wasiondoke na wafanye kazi kwa mshahara mdogo na wao wawalipie leseni na mafunzo," alisema Son.
Alisema wako wasomi ambao wanaleseni na wanalipia kila mwaka ila hawajui service na hawataki kazi za mikono kisa usomi wao ndio huwatumia vijana hao ambao hawana uwezo wa kulipia ada ya mafunzo na kulipia kila mwaka wanachohitaji wao ni kuwa vibarua wao,
Alisema ni fursa kwa vijana walioko katika tasnia hii ya drone za kilimo kupewa mafunzo zaidi kwenye fani yao na kupewa mikopo ya kikundi kununua drone za kutoa huduma ikiwa ni njia ya kuwawezesha.
Mdau mwingine wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) , Calvin Gwabara aliomba Serikali ipunguze takwa la kuwa na malipo
ya leseni ya kurusha drone ya kila mwaka ili watanzania waliowengi waweze
kurusha drone kwa ajili ya shughuli za kilimo na nyinginezo jambo
litakalosaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Drone zikifanya kazi ya shamba.

Drone ikishusha na kupakia mizigo ya shamabani kwenye gari.



No comments