VETA, FIELD MASTERS KUSHIRIKIANA KUTOA MFUNZO YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Field Master, Michael Dennis wakionesha hati ya ushirikiano baada kusaini mkataba wa utoaji wa mafunzo ya kilimo cha umwagiliaji.
.......................................
Na Mwandishi Wetu, Dodoma.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Novemba 7, 2025 imesaini makubalino na kampuni ya Field Masters kwa ajili ya ushirikiano wa kutoa mafunzo ya kilimo cha umwagiliaji.
Makubaliaono hayo yamesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Field Master, Michael Dennis, kwenye ofisi za VETA Makao Makuu, jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Hati iliyosainiwa, makubaliano hayo yanalenga kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji; matumizi ya zana bora za kilimo na kuwawezesha vijana kujiajiri na kufanya ujasiriamali kupitia kilimo cha kisasa.
Aidha ushirikiano huo unalenga kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji na mfumo wa kilimo cha kisasa na uongezaji thamani ya mazao.
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore ushirikiano huo utatekelezwa kupitia chuo cha VETA Arusha (Oljoro).
"Vjana wengi wanapenda kufanya biashara ya kuuza mazao ya kilimo na siyo kuingia shambani kufanya shughuli za kilimo wao wenyewe, hivyo kupitia mradi huu vijana watajifunza kilimo cha kisasa, kilimo biashara, hivyo kuongeza hamasa ya kujihusha na kilimo moja kwa moja," amesema Kasore.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Field Masters, Michael Dennis amesema, ameona Tanzania ina fursa kubwa katika sekta ya kilimo, hivyo kampuni yake inalenga kuwezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa kwa kutumia zana bora za kilimo na kuacha na matumizi ya zana duni kama jembe la mkono.
“Watanzania wengi wanaishi kwa kutegemea kilimo. Kilimo ndo kinaajiri watu wengi. Hata hivyo, wengi wao wamekuwa wakilima kwa kutegemea mvua. Lakini watu wakijifunza kilimo cha umwagiliaji kwa kuchimba mabwawa ya kuhifadhia maji wanaweza kulima wakati wowote na kupata mazao kwa wingi na kunufaika zaidi na kilimo,” amesema.
Kwa upande wake, Isdory Mwalongo, Mchumi wa kampuni ya Field Masters amesema ushirikiano huo utaleta tija katika sekta ya kilimo, lakini pia manufaa kwa VETA kwani vijana watakaokuwa wanapta mafunzo kupitia mradi huo watakuwa wakifanya uzalishaji wa mazao wakiwa kwenye mafunzo na pia watakapohitimu wataweza kujiajiri.Picha ya pamoja baada ya kusaini mkataba huo.


No comments