DKT. BITEKO ATOA WITO KWA VIONGOZI KUWATUMIA MAAFISA USHIRIKA
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (Mb) ametoa wito kwa Viongozi wa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuwatumia Maafisa Ushirika katika kazi zao kwani wapo wananchi wengi wanaohitaji huduma zao.
Akifunga Maashimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD 2024), Mkoani Tabora amewataka viongozi hao kutambua kuwa katika Vyama vya Ushirika kuna Watanzania milioni nane wanaohitaji huduma za Ushirika, hivyo Maafisa Ushirika washirikishwe kwenye mipango ya Mikoa na Wilaya.
“Ukimwambia Mkuu wa Mkoa niletee wataalam wako atakuletea Afisa Elimu, Kilimo, Afya, TARURA, TANESCO, Maji unakaa kikao Afisa Ushirika humuoni. Nao Maafisa Ushirika baada ya kuona hawaalikwi, wameamua kutengeneza ratiba zao, ushirika kwa hali hiyo hauwezi kukua,” ameeleza Mhe. Biteko.
Ameelekeza Wizara ya Kilimo kuwa na mpango wa makampuni yanayofanya biashara ya mazao ya tumbaku, korosho, kahawa ili kurudisha sehemu ya mauzo yao (CSR) kwenye jamii husika kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo. Na kutoa mfano wa wanunuzi wanaonunua tumbaku hapa nchini mauzo yote ni Dola za Marekani milioni 300 sawa na shilingi bilioni 700, zikiwa ni fedha za mzunguko unaotoka kwa wakulima hivyo ni vema sehemu yake ikarudi kuwekeza kwenye miradi mbalimbali.
Ametoa wito kwa wakulima kuwa na bima itakayowawezesha kugharamia pale wanapopata majanga mfano mvua za El Nīno, kuondoa dhana ya kuwa ni matajiri pekee wanaostahili kuwa na bima. Hivyo, elimu ya bima iendelee kutolewa na wakulima wengi wajisajili ili bima iweze kuwasaidia.Ameipongezi Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kuwa wabunifu na kuona mkulima naye anastahili huduma ya bima.
Hadi sasa, kuna jumla ya Vyama vya Ushirika 7,446 vyenye jumla ya wanachama zaidi ya milioni 8 vilivyosajiriwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwemo sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa Watanzania kwa zaidi ya asilimia 70.



No comments