USHIRIKA NDIYO MWELEKEO SAHIHI WA KUWEZA KUONDOA CHANGAMOTO KWA WAKULIMA
.....................................
Katika kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD 2024) Julai 6, 2024, mkoani Tabora, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ameeleza kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa katika Vyama vya Ushirika yamepelekea Taasisi nyingi za kifedha nchini kutaka kufanya biashara ya pembejeo za kilimo na vyama hivyo.
Ameeleza kuwa tasnia ya tumbaku mwaka 2023 kupitia Vyama vya Ushirika na baada ya kufanya mabadiliko ya mfumo wa ununuzi na uzalishaji wa tumbaku, uzalishaji umetoka wastani wa tani elfu 60,000 hadi tani 120,000 msimu huu wa kilimo ambapo mauzo yao yanatarajiwa kufikia zaidi ya Dola za Marekani 330,000. Ikimaanisha asilimia mia moja ya biashara hii ni kupitia Vyama vya Ushirika.
“Sekta ya korosho ilikufa, uzalishaji ukafika tani 180,000. Lakini leo hii Serikali inatoa ruzuku kupitia Vyama vya Ushirika yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 180 kwa wakulima wa korosho. Msimu wa kilimo uliopita uzalishaji wa korosho ulifika zaidi ya tani 330,000 na matarajio ya mwaka huu ni kufika tani 400,000 huku kiwango cha ubanguaji kikiwa kimeongezeka zaidi ya mara mbili,” ameongeza Mhe. Bashe.
Aidha, Chama cha Ushirika cha TANECU kilichopo Wilayani Newala kinatarajia kufungua kiwanda kikubwa cha kubangua korosho zaidi ya tani 3,000 na kufuata maelekezo aliyoyatoa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha mwaka 2026/27 Tanzania haiuzi korosho nje ya nchi bila kubanguliwa.
Waziri Bashe pia amewashukuru wanunuzi wa tumbaku kwani wakati mabadiliko ya zao la tumbaku yanaanza kulikuwa na vikwazo, lakini wanunuzi na Vyama vya Ushirika vilielewa. Mwaka huu 2024 Tanzania imekuwa nchi ya pili Afrika inayozalisha tumbaku kutoka katika kundi la wazalishaji wengine. Pamoja na changamoto za mvua za mwaka huu kuathiri shughuli za kilimo cha tumbaku kwa asilimia 30, lakini bado anaamini Tanzania itaendelea kuwa nafasi ya pili uzalishaji wa zao la tumbaku, Afrika.
Ameongeza kuwa kutokana na zao la tumbaku kuathiriwa na mvua msimu wa kilimo uliopita, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali kutoa shilingi bilioni 13 kwa wakulima wa zao la tumbaku kama ruzuku ili iwe ni sehemu ya kufidia gharama zao za uzalishaji. Fedha hizo zitalipwa kwenye akaunti ya mkulima na kiasi cha shilingi bilioni 13.3 kitatolewa kwa msimu ujao wa kilimo, ili kusaidia kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima wa tumbaku ambapo mbolea yote ya zao hilo imeagizwa na Serikali kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na itaanza kusambazwa kabla ya mwezi Agosti 2024. Aidha, fedha ya ruzuku itapelekwa TFC na mkulima atauziwa mbolea kwa bei ya ruzuku.



No comments