MKULIMA ILI AVUNE KWA TIJA ANATAKIWA KUACHA MASALIA YA MAZAO YA JAMII YA MIKUNDE SHAMBANI
.....................
Na Mwandishi Wetu
Ofisa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Theresia
Jacob amesema ili mkulima avune kwa tija wanatakiwa kuacha masalia ya mazao ya
jamii ya mikunde shambani, ili kusaidia udongo kuwa na rutuba.
Theresia amesena hayo leo Jumatatu Julai 29, 2024 katika mjadala wa X Space
(zamani Twitter) ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited
(MCL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ikiwa na mada inayosema
‘Fahamu faida za kiafya za ulaji vyakula jamii ya kunde, karanga na mbegu za
mafuta.’
“Kuacha masalia shambani ni moja ya namna bora ya kuboresha udongo na
kuurutubisha ambao unaweza kumfanya mkulima kulima kwa tija na kupata mazao ya
kutosha,” amesema Theresia.
Amesema kudhibiti magonjwa na wadudu kwa kutumia mbinu bora za kilimo, watu
wataweza kulima eneo dogo na kupata mazao mengi ya jamii ya mikunde na mafuta.
Miongoni mwa changamoto zinazowakumba wakulima wa mazao ya jamii hiyo ni
mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame, mafuriko, wadudu na magonjwa
mbalimbali yanayosababisha kuathiri mimea ikiwa shambani.
Kukosa mitaji, uwepo wa miundombinu hafifu katika baadhi ya maeneo nayo ni
changamoto inayofanya wengi washindwe kusafirisha mazao yao, jambo linalofanya
wapoteze mazao na ubora wake kupungua.
(Taarifa hii ni kwahisani ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited
(MCL))



No comments